Siku tano tu, TFF yavuna Sh10 milioni

KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) chini ya Mwenyekiti Wakili Kiamoni Kibamba juzi ilifunga zoezi la uchukuaji na urudishaji fomu kwa kuwania nafasi ndani ya shirikisho hilo katika uchaguzi utakaofanyika Agosti 7, lakini unaambiwa siku tano tu TFF imevuna fedha.
Uchaguzi huo umepangwa kufanyika jijini Tanga na hadi juzi jumla ya wagombea sita wa nafasi ya Urais na 26 wanaotaka Ujumbe wa Kamati ya Utendaji walikuwa wamerudisha fomu, huku wanne wa nafasi ya urais wakishindwa kufanya hivyo na kujiengua, huku TFF ikivuna zaidi ya Sh10 milioni.
Hadi linafungwa zoezi hilo kabla ya jana Jumapili ulianza mchujo kwa kupitia fomu za wagombea zaidi ya 30 kati ya 36 waliochukuwa fomu ambapo baadhi hawakurudisha fomu hizo.
Hata hivyo baadhi ya wagombea walijitoa wenyewe kwani hawakurudisha fomu hizo wakiwemo wagombea wanne nafasi ya rais ambao ni Rahim Kagenzi, Deogratias Mutungi, Abbas Tarimba na Zahoro Haji.
Zoezi hilo lilianza Juni 8 hadi 12 ikiwa ni siku tano tu zilizotumika na moja ya sharti la uchukuaji fomu hizo ilikuwa ni lazima mgombea alipie pesa, ambapo kwa nafasi ya Urais wagombea walilipa Sh 500,000 na walijitokeza 10 ikiwa na maana TFF ilivuna Sh 5 milioni.
Kwa nafasi ya Ujumbe wagombea walikamuliwa Sh 200,000 na jumla yao ilikuwa 26 ikiwa na maana walilipa jumla ya Sh 5.2 milioni na kufanya jumla ya fedha ilizovuna TFF kwa siku hizo tano za zoezi la kuchukua na kurudisha kuwa Sh 10.2 milioni.
Wagombea Urais wanasubiri mchujo kwa sasa ni Wallace Karia anayetetea kiti, Ally Saleh, Evans Mgeusa, Hawa Mniga akiwa mgombea pekee wa kike, mchambuzi wa gazeti hili, Oscar Oscar na nyota wa zamani wa kimataifa wa Yanga na Taifa Stars, Ally Mayay.
Wajumbe ni wa Kanda namba 1 (Dar es Salaam, Lindi, Morogoro, Mtwara na Pwani) ni Athuma Kambi, Elisony Mweladzi, Jimmy Msindo, Lameck Nyambaya, Michael Petro, Muharam Mazoka, Liston Katabazi, Saady Kimhji na Hosseah Lugano.
Kanda namba 2 (Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga) ni Khalid Mohammed, Zakayo Mjema na Thabithy Kandoro
wakati Kanda namba 3 (Iringa, Mbeya, Njombe, Ruvuma na Songwe) ni Abousufian Sillia, James Mhagama, Joseph Ngunangwa, Ulisaja Elias, Denis Manumbu na Mohammed Mashango.
Kanda namba 4 (Dodoma, Shinyanga, Simiyu na Singida) ni Hamisi Kitila, Mohammed Aden, Osuri Kosuri na Mrisho Kibwigiri wakati Kanda namba 5 (Geita, Kagera, Mara na Mwanza) ni Salum Chama na Vedastus Lufano.
Kanda namba 6 (Katavi, Kigoma, Rukwa na Tabora) ni Blassy Kiondo, Issa Bukuku na Kenneth Pesambili. Majina hayo yapo mezani mwa kamati iliyoanza kuyapitia jana hadi kesho Jumanne kabla ya Jumatano kutangaza waliopenya ili kusubiri kusailiwa na taratibu nyingine za kwenda Tanga kusubiri maamuzi ya wapiga kura kwenye Mkutano Mkuu wa Uchaguzi.