Shime aanza kuichambua Ethiopia
Muktasari:
- Kocha wa Twiga Stars, Bakari Shime, amesema jukumu la kwanza ni kuifuatilia Ethiopia na kutambua ubora na udhaifu wake ili kuandaa mikakati itakayoiwezesha Tanzania kufanya vizuri katika hatua hiyo.
BENCHI la ufundi la timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, litaanza kuichambua Ethiopia kwa lengo la kubaini mbinu na mfumo wake wa uchezaji kabla ya timu hizo kukutana katika raundi ya tatu ya kuwania tiketi ya Olimpiki za Los Angeles 2028.
Kocha wa Twiga Stars, Bakari Shime, amesema jukumu la kwanza ni kuifuatilia Ethiopia na kutambua ubora na udhaifu wake ili kuandaa mikakati itakayoiwezesha Tanzania kufanya vizuri katika hatua hiyo.
Twiga Stars ilifuzu raundi ya tatu baada ya kuiondoa Botswana kwa jumla ya mabao 7-0. Tanzania ilianza kwa ushindi wa bao 1-0 ugenini, lililofungwa na Opah Clement, kabla ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 6-0 katika mchezo wa marudiano uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Mabao ya Tanzania katika mchezo huo yalifungwa na Aisha Mnunka, Hasnath Ubamba, Ester Maseke, Opah Clement, Mary Siyame na Enekia Lunyamila.
“Tunajiandaa kwa ajili ya hatua inayofuata. Tayari tunawafahamu wapinzani wetu, hivyo tutafanya kazi ya kuwafuatilia na kujua namna wanavyocheza ili tujiandae vizuri kukabiliana nao,” amesema Shime.
Ethiopia nayo ilitinga raundi ya tatu baada ya kuiondoa Rwanda kwa jumla ya mabao 2-1. Iliibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini kabla ya kulazimisha sare ya bao 1-1 nyumbani.
Timu hiyo ina wachezaji wawili wanaocheza Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania, ambao ni Senaf Wakuma wa Simba Queens na Mesay Temesgen wa Yanga Princess. Temesgen alifunga bao moja katika michezo miwili ya hatua iliyopita.
Akizungumzia ushindi dhidi ya Botswana, Shime alikiri kuwa timu yake ilipata wakati mgumu katika dakika za mwanzo, hasa katika kuanzisha mashambulizi kutoka eneo la ulinzi. Hata hivyo, amesema alifurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake kipindi cha pili.
“Dakika 20 za mwanzo tulipata tabu katika namna ya kuondoka na mpira kuanzia nyuma. Tulipanga kuanzisha mashambulizi kutoka chini, ndiyo maana tulipata shida, lakini kipindi cha pili kilikuwa bora zaidi na tulimiliki mpira.
“Jambo zuri ni kwamba tumefunga mabao mengi na kupata nafasi nzuri ya kusonga mbele,” amesema.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, raundi ya tatu ya mashindano hayo itachezwa kati ya Februari 23 na Machi 6, 2027, kwa mfumo wa nyumbani na ugenini. Raundi ya nne imepangwa kufanyika Oktoba 4 hadi 12, 2027, huku raundi ya tano ikitarajiwa kuchezwa Novemba 23 hadi Desemba 4, 2027.
Twiga Stars italazimika kuvuka hatua tatu zilizobaki ili kufuzu Olimpiki za Los Angeles 2028, ambako Afrika itawakilishwa na timu mbili pekee. Mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika Julai 11 hadi 29, 2028.