Shauri yenu, mtajuta nyie!
Muktasari:
PENYE udhia penyeza rupia, huo ni usemi unaoeleza kwamba mahala penye matatizo ukiweka fedha, matatizo hayo yatawekwa kando na mafanikio au maendeleo yatapatikana.
PENYE udhia penyeza rupia, huo ni usemi unaoeleza kwamba mahala penye matatizo ukiweka fedha, matatizo hayo yatawekwa kando na mafanikio au maendeleo yatapatikana.
Hii inaonyesha kwamba katika hali yoyote ile, fedha inaweza kubadilisha hadhi na kuondoa mkwamo wowote katika jambo na kufanya mambo yaende kwa urahisi zaidi.
Timu 16 za soka zinashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara na karibu zote zina tatizo la fedha kwani zile wanazopata kutoka kwa wadhamini; Vodacom na Azam Media, hazitoshelezi mahitaji kwa msimu mzima.
Hata hivyo, kuna utofauti wa hali za timu hizo, kwani baadhi ya timu hali zake ni mbaya zaidi zikiwa zinategemea wadhamini hao tu na nyingine zina afadhali kwa vile zina wadhamini wa ziada.
Moja ya timu zinazoshiriki ligi hiyo na ambayo mara kwa mara wachezaji wake wamekuwa katika hali ngumu ni Ndanda ya Mtwara. Ina tatizo kubwa la ukosefu wa fedha kwa vile haina wanachama wala wafuasi ambao wana uwezo wa kuichangia.
Licha ya hali hiyo, Ndanda imekuwa ikishiriki katika ligi hiyo bila ya kuwa na mgogoro wa kiuongozi na imekuwa ikiyakabili matatizo yake ili kuweza kusonga mbele.
Hata hivyo, kuna timu ya Ligi Kuu ambayo imeukanusha usemi wa ‘Penye udhia penyeza rupia’ kwa vile licha ya klabu hiyo kupata bahati ya mtende kwa kupata udhamini mkubwa wa fedha, imekuwa kama njia ya kukaribisha migogoro ya uongozi.
Stand United, timu ambayo imetokana na wahudumu wa kituo cha mabasi cha Shinyanga ilipigana hadi kuingia Ligi Kuu Bara na baada ya kuchechemea na kunusurika kushuka daraja katika msimu wa kwanza, ilibahatika kupata mdhamini katika msimu wake wa pili.
Hapo kila shabiki wa soka nchini akijenga fikra kuwa Stand United iliyokuwa haina migogoro wakati haina fedha, sasa itafanya maajabu makubwa baada ya zaidi ya Sh2 bilioni kuingia katika klabu hiyo kutoka kwa Kampuni ya uchimbaji madini ya ACACIA.
Mambo yamekwenda tofauti kwani fedha hizo hazikuondoa udhia bali ndizo zimeleta machafuko na mtafaruku ndani ya klabu hiyo ambayo ingeweza kufanya vizuri zaidi kuliko inavyofanya sasa katika Ligi Kuu Tanzani Bara.
Kwa uwezo wake wa fedha, kundi zuri la wachezaji ilionao wakiwemo vijana hodari na kocha mwenye uzoefu wa hali ya juu, Patrick Liewig, Stand United ingekuwa na hali ya utulivu na amani bila shaka ingekuwa inachuana kileleni na timu za Yanga, Azam na Simba za jijini Dar.
Hata hivyo, kutokana na mvutano wa uongozi uliopo ambao dalili zake ni kila mmoja kutaka umiliki wa fedha hizo ambazo ziko chini ya mamlaka ya Liewig, timu sasa ipo katikati mwa msimamo wa Ligi Kuu.
Juhudi kadhaa zimekuwa zikichukuliwa katika kutafuta ufumbuzi mgogoro wa Stand United kwa hiyo wakati umefika sasa wadau wa timu hiyo wasahau tofauti zao ili kurudisha amani na iweze kufanya vizuri zaidi katika Ligi Kuu Tazania Bara.
Hili jambo la kuepuka migogoro si kwa Stand peke yake, bali inapaswa kutiliwa maanani na wadau wa timu zote kwani kwenye migogoro hakuna mafanikio kwani hata wadhamini wataikimbia timu ambao haina amani kwani haiwezi kufikisha lengo lao.
Siku zote amani na kutokuwepo migogoro kunaleta mafanikio kwenye timu na kuinua kiwango cha soka kwa kusaidia kutoa wachezaji wazuri kwa ajili ya timu ya taifa, Taifa Stars.
Njia mojawapo ya kuepusha migogoro ya uongozi au ile inayowahusisha wanachama ni kwa klabu kufanya mambo yake kwa uwazi bila ya kuwepo siri zozote zisizokuwa za lazima ili kila mmoja aridhike.
Mara nyingi viongozi wanajisahau na kufanya mambo kama klabu hizo ni za kwao binafsi na hakuna wa kuwahoji na kukaa muda mrefu bila ya kuitisha mikutano ya wanachama na kutoa taarifa za mapato na matumizi.
Fedha inapaswa itumike vizuri ili klabu ifike kilele cha mafanikio na kwa namna yoyote ile, rasilimali hiyo isigeuke kuwa chanzo cha uhasama na migogoro ndani ya klabu na kuvuruga maendeleo yake.
Moja ya njia ya kuleta mafanikio ndani ya klabu ni kuwepo kwa uongozi wa pamoja na siyo kwa mtu mmoja au kikundi kidogo kuhodhi madaraka na wao ndo kuwa na uamuzi wa kila jambo.
Klabu haipaswi kuongozwa na mtu mmoja kwa vile ni mali ya umma kwa hiyo ni lazima kuwe na uongozi shirikishi ambao utamshirikisha kila mwanachama kutoa mchango katika uamuzi na maendeleo ya klabu yake.
Ni rahisi kukiwepo uongozi wa pamoja kwa klabu kuzikabili na kuzishinda changamoto zote zinazotokea bila ya kutumia nguvu kubwa na kuleta ufanisi kwani ikumbukwe kwamba umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.
Uongozi wa mtu mmoja kujionyesha kwamba yeye ni kifaru na anajua kila kitu na hataki kusikia la kuambiwa hauwezi hata siku moja kuleta mafanikio ya maana na ya kupigiwa mfano katika klabu.
Njia sahihi ni kwa viongozi waliochaguliwa na wanachama wenyewe kuongoza klabu kwani wao ndio walioaminika na ndio waliopewa dhamana hiyo na wanachama walio wengi.
Ni vyema klabu zikajitahidi kuepuka migogoro ya aina yoyote kwani kikwazo kikubwa cha maendeleo yao na kwa kawaida migogoro hukimbiza wadhamini ambao katika maisha ya sasa ya uendeshaji wa mpira wa miguu hawaepukiki kwani gharama zimekuwa juu.
Mbali na gharama za kusajili wachezaji na benchi la ufundi pia klabu inakabiliwa na gharama kubwa za uendeshaji wa timu licha ya kutakiwa pia itumie gharama kubwa na kukuza vipaji kwa kuziendeleza timu zao za vijana.
Gharama hizo klabu haziwezi kuzikidhi kwa kutegemea michango ya wanachama wao au wadhamini wa Ligi ambao kiasi walichotoa hakitoshi kulipa gharama za kuendesha timu hizo.
Ni vizuri klabu zikaendeleza timu zake za vijana na kila msimu zikawa na uwezo wa kuwapandisha wachezaji kadhaa kwa timu yao ya kwanza badala ya kutegemea kusajili wachezaji wapya wengi kutoka nje ya timu yao.
Siku zote penye migogoro yote haya hayawezi kufanyika hata kama fedha ya wadhamini ipo kwani kutakuwa hakuna utulivu kwa kupanga mipango endelevu bali kila kiongozi atakuwa anafanya juhudi ya kutafuta mbinu za kujilinda Ili abaki kwenye uongozi.
Baya zaidi hata kama wadhamini wapo, migogoro inaweza kuwafukuza na kuondoa wadhamini wao kwani faida waliokuwa wanataka waipate ya kuwatangaza haiwezi kupatikana kwenye migogoro.
Ni vyema klabu zote zikawa na mipango endelevu ya kujiendesha na kuepuka migogoro na ikiwepo dalili ya kutaka kutokea waisuluhishe na kuitafutia ufumbuzi kwenye vikao husika na kujenga dhana ya kuaminiana na kusameheana inapotokea tatizo, la sivyo ni majuto mbeleni.
Masoud Sanani ni Mwandishi wa Habari Mwandamizi amewahi kufanya kazi Televisheni Zanzibar, Uhuru na Mzalendo, Business Times ( Mhariri Mwanzilishi wa Spoti Starehe ) na Mwananchi. Alikuwa Mkurugenzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania ( TEF).
E-mail [email protected]
Simu 0712-020020.