Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shamba la Bibi hadi kieleweke CECAFA U-20

UHURU Pict

Muktasari:

  • Mechi ya kwanza itawakutanisha Rwanda dhidi ya Ethiopia saa 8:00 mchana, kabla ya Djibouti kukutana na Sudan saa 11:00 jioni na baadaye Burundi kumalizana na Kenya saa 2:00 usiku.

MICHUANO ya Afrika Mashariki na Kati CECAFA U-20 inatarajiwa kuendelea Alhamisi ya Septemba 17 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, huku Rwanda, Ethiopia, Djibouti, Sudan, Burundi na Kenya zikishuka uwanjani kuwania pointi muhimu za kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele.

Mechi ya kwanza itawakutanisha Rwanda dhidi ya Ethiopia saa 8:00 mchana, kabla ya Djibouti kukutana na Sudan saa 11:00 jioni na baadaye Burundi kumalizana na Kenya saa 2:00 usiku.

Rwanda na Ethiopia zilizopo Kundi A pamoja na wenyeji Tanzania, zitaanza siku hiyo kwa mechi inayoweza kutoa picha ya ushindani uliopo kwenye kundi hilo. Ethiopia si timu ya kubezwa, kwani imewahi kutwaa ubingwa huo mara tatu, mwaka 1995, 1996 na 2005.

Kwa upande wa Rwanda, ingawa haina historia kubwa ya mataji katika mashindano hayo kama Ethiopia, ilionyesha uwezo wake kwenye michuano iliyopita ya 2024 kwa kuifunga Djibouti 5-1, kabla ya baadaye kutandikwa 3-0 na Tanzania katika hatua ya makundi, ilitoka sare ya 0-0 na Kenya.

UHU 01

Hivyo, pambano la Rwanda na Ethiopia linakuwa muhimu si kwa pointi pekee, bali pia kwa Tanzania ambayo itakutana na Rwanda Septemba 19 na Ethiopia katika mechi ya mwisho ya makundi.

Baada ya hapo, Djibouti na Sudan zitakutana saa 11:00 jioni katika Kundi B, ambalo pia lina Uganda. Sudan inaingia ikiwa na kumbukumbu nzuri dhidi ya Djibouti kutokana na ushindi wa 3-1 kwenye CECAFA U-20 ya mwaka 2024.

Djibouti yenyewe ilipata wakati mgumu kwenye mashindano ya 2024, ikifungwa 7-0 na Tanzania na baadaye 5-1 na Rwanda, jambo linalofanya mechi dhidi ya Sudan kuwa kipimo muhimu cha kuona kama imeboresha kiwango chake mwaka huu.

Sudan nayo ina historia nzuri katika soka la vijana ukanda huu na kwenye mashindano ya 2024 iliifunga Rwanda 1-0, kabla ya kupoteza 1-0 dhidi ya Tanzania na baadaye 4-0 dhidi ya Kenya. Hivyo mechi ya Alhamisi itakuwa nafasi ya timu hiyo kuanza upya mbio zake za kutafuta nafasi ya nusu fainali.

UHU 02

Mechi ya mwisho saa 2:00 usiku, Burundi na Kenya zitafunga ratiba kwa mechi ya Kundi C, ambalo pia lina Sudan Kusini na hapa kuna mechi ya kuvutia zaidi.

Kenya ni moja ya vigogo wa mashindano haya ikiwa na mataji mawili ya CECAFA U-20, ya mwaka 1975 na 1999, huku mwaka 2024 ikifika fainali na kupoteza 2-1 dhidi ya Tanzania.

Burundi nayo ina historia kwenye mashindano ya 2024 ilifika hatua ya nusu fainali baada ya kumaliza ya pili kwenye Kundi B ikiwa na pointi sita, ikishinda Ethiopia 3-2 katika mchezo wake wa mwisho wa makundi. Hata hivyo, ilifungwa na Kenya katika hatua ya nusu fainali.

Kwa hiyo, mchezo wa Burundi na Kenya unaweza kuwa mmoja wa michezo migumu ya siku hiyo kutokana na historia ya Kenya kwenye mashindano hayo na uwezo ambao Burundi iliuonyesha kwenye toleo lililopita.

Kocha wa Kenya, Gilbert Selebwa amesema mchezo wao wa kwanza utakuwa mgumu kutokana na mahitaji ya timu zote mbili.

"Tumekuwa na changamoto kwenye kikosi lakini kwa waliopo sasa tunaamini tumekuwa na maandalizi kiasi hivyo tutapambana kuhakikisha tunabeba pointi kwenye mechi ya kwanza ambayo ni muhimu japo itakuwa ngumu kutokana na ubora wa wapinzani wetu."