Shalulile kutua rasmi Yanga kesho
Muktasari:
- Kamwe amezungumza hayo katika Mkutano Mkuu wa Yanga unaofanyika leo Jumapili ya Agosti 2, 2026, kwenye Ukumbi wa The Super Dome, Masaki, jijini Dar es Salaam.
MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga, Peter Shalulile, anatarajiwa kuwasili nchini kesho Jumatatu ya Agosti 3, 2026, kwa ajili ya kujiunga rasmi na timu hiyo atakayoitumikia kwa msimu wa 2026-2027.
Akizungumza jijini, Dar es Salaam, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, amesema mchezaji huyo atatambulishwa rasmi kesho Jumatatu kuanzia saa 5:00 usiku, ambapo tukio hilo litakuwa mubashara kupitia Azam TV.
Kamwe amezungumza hayo katika Mkutano Mkuu wa Yanga unaofanyika leo Jumapili ya Agosti 2, 2026, kwenye Ukumbi wa The Super Dome, Masaki, jijini Dar es Salaam.
Shalulile ambaye ni raia wa Namibia, alitambulishwa kuwa mchezaji wa Yanga, Julai 27, 2026, baada ya mkataba wake na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kumalizika.
Mshambuliaji huyo amejiunga na mabingwa hao wa Tanzania baada ya kuhitimisha safari yake ya miaka sita ndani ya Mamelodi Sundowns, akiwa amefunga jumla ya mabao 136 katika mashindano yote.
Mbali na kufunga mabao hayo 136, pia Shalulile aliisaidia Mamelodi Sundowns kutwaa mataji mbalimbali ikiwemo Ligi Kuu ya Afrika Kusini mara tano, Ligi ya Mabingwa Afrika na African Football League, akiwa ni mchezaji mzoefu anayesubiriwa zaidi na mashabiki wa Yanga kwa ajili ya kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji.