Serikali yatoa Bil 104 kuandaa AFCON 2027
Muktasari:
- Makonda aliyasema hayo leo, Septemba 24, 2026, katika mkutano na waandishi wa habari uliohusu maandalizi ya AFCON, Miss World pamoja na masuala ya ugawaji wa mirabaha kwa wasanii.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amesema Serikali imelipa Sh 104 bilioni kwa ajili ya kuandaa na kupata haki ya matangazo kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Makonda ameyasema hayo leo, Septemba 24, 2026, katika mkutano na waandishi wa habari uliohusu maandalizi ya AFCON, Miss World pamoja na masuala ya ugawaji wa mirabaha kwa wasanii.
Makonda amesema fedha hizo zimelipwa kama sehemu ya gharama za Tanzania kupata haki ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo, akieleza kuwa Serikali inalenga kuhakikisha nafasi hiyo inatumika zaidi ya michezo na kuwa fursa ya kuitangaza Tanzania duniani.
“Serikali imelipa shilingi 74 bilioni pesa ya kuwa mwenyeji tu wa mashindano ya AFCON. Bilioni 30 kwa ajili ya kupata haki ya matangazo, kama nchi tumelipa fedha hizo ili tupate uhalali na waone sehemu sahihi,” amesema Makonda.
Amesema Tanzania inatarajia kutumia nafasi hiyo kuwafanya wageni watakaokuja nchini kuiona nchi na fursa zilizopo, hususani katika uwekezaji, huku akisisitiza kuwa mashindano hayo yanaweza kuwa chachu ya kufungua nafasi za ajira kwa vijana.
“Ili watakaokuja waone Tanzania, waone sehemu sahihi ya kuwekeza na vijana wapate ajira,” amesema Makonda.
Tanzania ni miongoni mwa waandaaji wenza wa mashindano ya AFCON 2027, ambayo yatashirikisha nchi za Uganda na Kenya.