Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makonda: Sh2 bilioni za mirabaha kuanza kugawiwa kwa wasanii

MAKONDA Pict

Muktasari:

  • Makonda ameyasema hayo leo Septemba 24, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya AFCON 2027, Miss World na ugawaji wa mirabaha.

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kugawa Sh2 bilioni za mirabaha kwa wasanii na kwamba fedha hizo zinatarajiwa kuanza kutolewa Novemba mwaka huu.

Makonda ameyasema hayo leo Septemba 24, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya AFCON 2027, Miss World na ugawaji wa mirabaha.

Makonda amesema fedha hizo ni sehemu ya mirabaha inayokusanywa kwa ajili ya kuwapatia wasanii mapato yanayotokana na kazi zao, akisisitiza kuwa Serikali inaendelea kuweka utaratibu wa kuhakikisha wanufaika wanapata haki yao baada ya kutumia muda na nguvu katika kuzalisha kazi za sanaa.

“Ndugu wasanii mjiandae, fedha zenu mwezi wa 11 zitatoka. Tutawatangazia tarehe ili mchukue pesa ambazo mmezizalisha” alisema Makonda 

Alisema Serikali inaendelea na mchakato wa kuhakikisha fedha hizo zinagawanywa kwa utaratibu unaotambua mchango wa wasanii, huku akieleza kuwa sheria imeweka utaratibu wa namna ya kugawana fedha zinazotokana na matumizi ya kazi za wasanii.

Makonda alisema hatua hiyo inalenga kuongeza kipato cha wasanii na kuhakikisha wanaendelea kunufaika kutokana na kazi walizozalisha kwa muda mrefu, akisisitiza kuwa fedha hizo ni sehemu ya haki yao baada ya kuvuja jasho katika kazi zao.

Akizungumzia maandalizi ya Miss World, Makonda alisema Wizara imesaini mkataba na waandaaji wa Miss Tanzania na kwamba idara husika inaendelea kukamilisha mchakato wa kuunda kamati itakayoratibu maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa shughuli hizo mwakani.

Alisema Tanzania inatarajiwa kupokea washiriki kutoka nchi 126, hivyo Serikali inataka maandalizi yaanze mapema ili kuhakikisha fursa zitakazotokana na ujio huo zinawanufaisha Watanzania.

Makonda alisema matukio makubwa ya Miss World yatafanyika Dar es Salaam, Zanzibar na Arusha, huku washiriki wakipelekwa katika maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii. Pia alisema Serikali inalenga kutumia mashindano hayo kukuza utamaduni wa Tanzania, ikiwamo kila mshiriki kutambulisha kabila moja la Tanzania.

Alisema pia kutakuwa na juhudi za kukuza Kiswahili kupitia Miss World, ikiwamo wimbo wa mashindano hayo kutafsiriwa kwa Kiswahili na kupelekwa katika mataifa mbalimbali ili kusaidia kuitangaza lugha hiyo kimataifa.

Makonda alisema viongozi na wadau mbalimbali wa sanaa na utamaduni, akiwamo Mustafa Hassanali na Lamata Leah, wanapaswa kushirikishwa katika mchakato huo ili kutoa mawazo yatakayosaidia Tanzania kutumia fursa hizo kujenga uchumi.

“Sisi Serikali tunapambana kuhakikisha kila fursa inawanufaisha wananchi na Watanzania washiriki kutoa maoni yao kupitia kamati itakayoundwa,” alisema.