Serikali yaombwa kuitazama Pickleball
SERIKALI na wadau wa michezo nchini wametakiwa kuongeza juhudi za kuendeleza mchezo wa pickleball ili kuukuza, kuongeza umaarufu wake na kufungua fursa za ajira kwa vijana.
Wito huo umetolewa na wachezaji, waamuzi na wadau wa mchezo huo wakati wa mashindano ya Smash and Save, yaliyoandaliwa na Rotary Dar es Salaam kwa lengo la kukusanya fedha za kuwezesha upatikanaji wa madawati katika shule mbalimbali nchini.
Mashindano hayo yalifanyika juzi katika viwanja vya Tanzanite, Mikocheni, Dar es Salaam, ambapo wadau hao wamesema Tanzania imeanza vizuri katika mchezo huo tangu ulipoanza kutambulishwa nchini katika miaka ya hivi karibuni.
Mdau, mdhamini na mchezaji wa pickleball nchini, Dk. Sajad Habib Rai, amesema Tanzania ina vipaji vingi katika mchezo huo, hivyo kinachohitajika ni kuwapa vijana wanaoupenda nafasi na msaada ili waweze kuimarisha uwezo wao.
“Ukweli ni kwamba pickleball imekuja kwa kasi nchini. Ukiangalia viwanja mbalimbali ambako mchezo huu unachezwa, utaona mwamko mkubwa wa vijana. Watu wana moyo na mapenzi na mchezo huu. Kinachohitajika ni kuwashika mkono ili kupata wachezaji bora watakaoliwakilisha Taifa katika mashindano mbalimbali,” amesema Dk. Sajad.
Ameongeza kuwa, kama mdau wa mchezo huo, amekuwa akijitolea kusaidia juhudi za vijana wanaopenda pickleball, ikiwamo kuandaa mashindano maalumu kwa lengo la kuibua na kukuza vipaji.
Dk. Sajad aliitaka Serikali, hususan Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo, kutafuta njia za kuwafikia na kuwaunga mkono wachezaji wa pickleball ili kujenga msingi imara wa maendeleo ya mchezo huo nchini.
Kwa upande wake, mwamuzi wa pickleball, Mohammed Raajan, ambaye Agosti mwaka huu alikwenda Vietnam kuchezesha fainali za dunia za mchezo huo, amesema Tanzania inaweza kufanya vizuri kimataifa iwapo itaweka mikakati madhubuti ya kuendeleza mchezo huo.
Raajan aliomba Serikali na wadau kuongeza uwekezaji katika ujenzi wa viwanja maalumu vya pickleball ili kuvutia watu wengi zaidi kushiriki na kukuza ushindani miongoni mwa wachezaji.
Naye kocha wa pickleball nchini, Abdallah Manyua, amesema Tanzania ina uwezo wa kufikia mafanikio makubwa, ikiwamo kushindania taji la dunia, iwapo mchezo huo utapewa kipaumbele na wadau pamoja na wadhamini.
Manyua alisisitiza kuwa uwezeshaji wa kutosha utasaidia kukuza vipaji, kuongeza ushindani na kuwapa wachezaji nafasi ya kujiandaa kwa mashindano ya kimataifa.