Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mandeke kutoka Simba hadi michuano ya UEFA

Muktasari:

  • Hiyo imetokea kwa Mtanzania Abdu Omari Mandeke ambaye ni mmoja wa vijana wa Kitanzania wanaotafuta nafasi ya kuendeleza vipaji vyao nje ya nchi.

WAKATI mwingine mambo hutokea haraka sana tofauti na vile ambavyo inatarajiwa. Kutoka timu ya vijana ya Simba hadi kuwa kwenye orodha ya wachezaji ambao watatumika katika michuano midogo ya Ulaya ‘UEFA Conference League 2026/2027’ akiwa na miamba ya soka la Latvia, Riga FC.

Hiyo imetokea kwa Mtanzania Abdu Omari Mandeke ambaye ni mmoja wa vijana wa Kitanzania wanaotafuta nafasi ya kuendeleza vipaji vyao nje ya nchi.

Akiwa na umri wa miaka 19, tayari amepitia hatua kadhaa katika maisha yake ya soka akianzia kwenye mfumo wa vijana wa Simba kabla ya Nigeria na baadaye kutua Latvia ambako anaendelea kupigania nafasi yake katika klabu ya Riga FC.

Safari yake imeanza kuvutia kutokana na maendeleo anayoyapata ndani ya klabu hiyo, ambayo inashiriki mashindano ya ndani ya Latvia na UEFA Conference League msimu wa 2026/27. Hata hivyo, kwa sasa changamoto kubwa kwa kiungo huyo ni kuendelea kujithibitisha katika kikosi cha pili huku akipigania nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.

SIMBA MWANZO

Kabla ya Ulaya, Mandeke alikuwa sehemu ya mfumo wa soka la vijana wa Simba, akicheza katika kikosi cha chini ya miaka 17. Hiyo ilikuwa moja ya hatua muhimu katika safari yake, ikimpa nafasi ya kujifunza misingi ya soka la ushindani na kujiandaa kwa changamoto kubwa zaidi.

Baadaye alijiunga na Grassrunners FC ya Nigeria, hatua iliyomfungulia njia ya kuendelea na safari yake nje ya Tanzania. Kutoka Tanzania hadi Nigeria, kisha Latvia, ni safari inayoonyesha namna wachezaji vijana wanavyoweza kutafuta mazingira mapya ya kukuza vipaji vyao na kupanua wigo wa uzoefu wao. Hata hivyo, kufika Ulaya si mwisho wa safari. Kwa Mandeke, hatua inayofuata ni kuendelea kufanya vizuri mazoezini na kwenye mechi anazopata nafasi ya kucheza ili kujijengea nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Riga FC.


NAHODHA WA KIKOSI CHA PILI

Mandeke anatumika zaidi katika kikosi cha Riga FC II, kikosi cha pili cha klabu hiyo kinachoshiriki ligi ya daraja la pili ya Latvia inayojulikana kama Futbola Pirma Liga.

Katika kikosi hicho, kiungo huyo amekuwa akitumika zaidi katika eneo la kiungo mkabaji, akicheza majukumu yanayohusisha kukaba, kuzuia mashambulizi ya wapinzani na kusaidia timu kujenga mashambulizi kutoka nyuma. Taarifa za maendeleo yake pia zinamtaja kama nahodha wa kikosi hicho, jukumu linalohitaji nidhamu, uwajibikaji na uwezo wa kuongoza wenzake uwanjani.

Kwa mujibu wa takwimu, Mandeke amefikisha mechi 21, mabao matatu na asisti moja katika ligi hiyo. Takwimu hizo zinaonyesha kuwa pamoja na kucheza zaidi katika eneo la kiungo mkabaji, ana uwezo wa kuchangia pia katika hatua za mwisho za mashambulizi.

Wasifu wake unamtaja kama mchezaji anayeweza kucheza kiungo mkabaji na kiungo mshambuliaji, jambo linaloweza kumpa kocha chaguo zaidi katika kupanga kikosi kulingana na mahitaji ya mchezo.

Kwa mchezaji wa umri wake, kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika ligi ya ushindani ni sehemu muhimu ya maendeleo. Mechi hizo zinampa nafasi ya kujifunza kasi ya soka la watu wazima, kufanya maamuzi chini ya presha na kutekeleza majukumu ya kiufundi na kiulinzi.


AMEANZA KUGUSA KIKOSI CHA KWANZA

Pamoja na majukumu yake katika kikosi cha pili, Mandeke amepata nafasi ya kucheza katika Kombe la Latvia akiwa na Riga FC.

Katika mchezo dhidi ya Leevon PPK, uliofanyika Julai 10, 2026, Riga FC ilishinda mabao 3-2. Rekodi za Shirikisho la Soka la Latvia zinaonyesha kuwa Mandeke alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Riga katika mchezo huo na alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 23. 

Kupata nafasi katika mashindano ya kombe ni hatua inayoweza kumsaidia kijana huyo kuonyesha uwezo wake katika mazingira ya ushindani tofauti na yale anayokutana nayo kwenye ligi ya kikosi cha pili. Pia, kunampa uzoefu wa kucheza mechi ambazo matokeo yake yanaweza kuamua safari ya timu katika mashindano.

Kwa Mandeke, changamoto ni kutumia nafasi hizo kuonyesha kuwa anaweza kushindana na wachezaji wengine wanaowania nafasi katika kikosi cha kwanza. Katika soka la kulipwa, maendeleo ya mchezaji hupimwa kwa kiwango chake, nidhamu, uwezo wa kuelewa mbinu za kocha na namna anavyotekeleza majukumu anayopewa.


CONFERENCE LEAGUE

Riga FC ni miongoni mwa klabu zinazoshiriki UEFA Conference League msimu wa 2026/27, mashindano ya klabu barani Ulaya yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA).

Katika mchezo wake wa kwanza wa hatua ya ligi, Riga FC ilitoka sare ya mabao 1-1 dhidi ya Kairat Almaty ya Kazakhstan, Oktoba 15, 2026. Kairat ilitangulia kwa bao la penalti la Marc Gual dakika ya tano, kabla ya Riga kusawazisha kupitia Salah-Eddine Oulad M’hand dakika ya 12. 

Hata hivyo, Mandeke hakuwa miongoni mwa wachezaji ambao walitakiwa kutumika  kwenye kikosi cha siku ya mchezo huo. Hivyo, bado anasubiri nafasi ya kuingia katika kikosi kitakachotumika katika michezo ijayo.

Kwa kijana anayejenga jina lake barani Ulaya, kufika hatua ya kuwania nafasi katika mashindano ya UEFA ni fursa ya kuendelea kujifunza na kupanua uzoefu wake. Lakini kucheza mashindano hayo kutahitaji kwanza kupata nafasi katika kikosi rasmi cha mechi na baadaye kuaminiwa na benchi la ufundi kuingia uwanjani.

Kwa mfumo wa UEFA Conference League, timu 36 hushiriki hatua ya ligi. Timu nane za juu hufuzu moja kwa moja hatua ya 16 bora huku zinazomaliza nafasi ya tisa hadi ya 24 zikicheza mechi za mchujo kuwania nafasi zilizobaki. Timu zinazomaliza nafasi ya 25 hadi ya 36 huondolewa katika mashindano ya Ulaya.

Kwa Riga FC, lengo ni kufanya vizuri katika mechi zake ili kuendelea na safari ya mashindano. Kwa Mandeke, wakati huo huo, lengo la karibu ni kuendelea kupambana ili kuweka rekodi katika michuano hiyo.


UZOEFU TIMU YA TAIFA

Safari ya Mandeke haijajengwa kwenye soka la klabu pekee, aliwahi kucheza timu ya  taifa ya Tanzania chini ya miaka 20.

Uzoefu huo ni sehemu nyingine muhimu ya maendeleo yake kwa kuwa mashindano ya kimataifa ya vijana huwapa wachezaji nafasi ya kukutana na mitindo tofauti ya uchezaji na kujifunza kukabiliana na wapinzani wenye uwezo mbalimbali.

Pia, nyota huyo amewahi kushiriki katika mashindano ya vijana ya Gothia Cup nchini Sweden mwaka 2019, 2022 na 2023, pamoja na mafunzo ambayo aliwahi kupata Hispania kwenye Klabu ya Celta Vigo 2022.

Uzoefu wa aina hiyo unaweza kumsaidia mchezaji kuzoea mazingira mapya, lakini mafanikio ya muda mrefu yanahitaji zaidi ya kushiriki mashindano.

Nidhamu, afya, maendeleo ya kiufundi, uwezo wa kuelewa mbinu za kocha na kupata dakika za kucheza ni miongoni mwa mambo yatakayochangia safari yake.