Serengeti Boys kibaruani leo dhidi ya Somalia
Muktasari:
- Serengeti Boys inatarajiwa kukabiliana na Somalia katika mchezo wake wa pili wa Kundi C, unaotarajiwa kuwa na ushindani kutokana na umuhimu wa pointi tatu kwa timu zote mbili.
Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, leo Jumatatu, Oktoba 12, 2026 itakuwa na kibarua cha kusaka ushindi mwingine itakapokutana na Somalia katika mchezo wa Kundi C wa kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (AFCON U-17) za mwaka 2027, utakaochezwa kwenye Uwanja wa Pele, Kigali, Rwanda.
Serengeti Boys inatarajiwa kukabiliana na Somalia katika mchezo wake wa pili wa Kundi C, unaotarajiwa kuwa na ushindani kutokana na umuhimu wa pointi tatu kwa timu zote mbili.
Kama itafanikiwa kushinda mchezo huo, Serengeti itafuzu hatua ya nusu fainali, huku Somalia ikilenga kusaka ushindi ili kuzindua kampeni zake vizuri.
Katika mchezo wake wa kwanza wa hatua ya makundi, Serengeti Boys ilianza kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kenya. Mabao hayo yalifungwa na Dismas Athanas na Godfrey Somi.
Kwa upande wa Somalia, mchezo huo utakuwa wa kwanza katika kundi hilo, jambo linaloongeza umuhimu wa pambano hilo kwa timu zote mbili katika harakati za kusaka nafasi ya kusonga mbele.
Serengeti Boys inaingia katika mchezo huo ikiwa na dhamira ya kuendeleza mafanikio ya mwaka jana, ilipotwaa taji hilo. Mafanikio hayo yanaongeza hamasa kwa vijana hao kupambana kwa nguvu ili kutetea heshima yao na kuhakikisha wanapata nafasi ya kushiriki fainali hizo mwakani.
Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Mario Rivera Campesino, amesema licha ya timu yake kuanza kwa ushindi dhidi ya Kenya, bado anaamini wachezaji wake wana uwezo wa kuonyesha kiwango bora zaidi.
Campesino amesema makosa yaliyojitokeza katika mchezo uliopita yamefanyiwa kazi ili kuimarisha timu yake kabla ya kukutana na Somalia.
“Tunajua ugumu wa mechi hiyo kwa sababu Somalia nao watakuja kucheza ili wakusanye pointi zote na kuanza vizuri, lakini makosa tuliyoyafanya kwenye mechi iliyopita tumeyafanyia kazi na tunaamini tutaonyesha mchezo mzuri,” alisema.