SEKILOJO: Nini Samatta! Utajiri wa soka ulivyonipiga chenga
Muktasari:
Rais wa Dinamo na watu wake hawakutaka Sekilojo arudi Tanzania na badala yake ajiunge moja kwa moja na timu yao. Yanga waligoma.
Dar es Salaam.Jana Jumamosi, staa wa zamani wa Yanga, Sekiloja Chambua alieleza jinsi alivyopata dili tamu za kucheza soka la kulipwa, lakini mabosi wa Jangwani wakambania.
Sasa achana na dili hizo mbili, zikaja dili zingine tamu kabisa huku Durban, lakini Sekilojo akafanya utoto ambao mpaka sasa anaujutia na leo anafunguka mazito zaidi.
Tunazurura katika mitaa ya Johannesburg kisha tunarudi kutembea Sandton tukipita katika maduka mbalimbali. Tunafika katika hoteli ya Sandton Sun kwa ajili ya kupoza koo kidogo. Sekilojo anakumbuka dili nyingine mbili ambazo zilimpita kwapani kama masikhara. Zote za kuja Afrika Kusini.
Ndani ya jezi za njano na kijani, Yanga ilisafiri mpaka Durban kucheza pambano la michuano ya Afrika dhidi ya Moroka Swallows. Sekilojo alikuwa aking’ara vilivyo katika jezi ya Yanga na tayari alikuwa ameshaonwa na viongozi wa klabu ya Dinamo ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Timu hiyo ilikuwa inafundishwa na kocha wa zamani wa Simba, Ettiene Eshete ambaye alikuwa ni raia wa Ethiopia. Sekilojo anakumbuka vema jinsi ambavyo alianza kulichafua dili hili kwa mikono yake mwenyewe akionyesha tabia za kitoto.
“Hawa jamaa walikuwa wananitaka na walituma ujumbe kwamba wangekuja hotelini pale Durban kesho yake saa nne asubuhi. Nilianza kuonyesha kukosa uweledi kwa mimi mwenyewe kwanza kutojali muda. Baada ya kuwasubiri hawa viongozi nikaenda kufanya shopping nikiwa na wachezaji wenzangu,” anasimulia Sekilojo. Anaamini kwamba kitendo hiki asingekifanya kama ingekuwa leo.
“Tulizurura katika maduka kumbe huku nyuma alikuja Rais mwenyewe wa klabu ya Dinamo kuzungumza na mimi. Awali, alisema angemtuma kocha na mwakilishi lakini akaja mwenyewe kutoka Johannesburg kwa ajili ya kufunga dili. Nilijisikia vibaya kurudi na kumkuta Rais wa timu akinisubiri. Nilikuwa nimeshachelewa miadi na halikuwa jambo zuri,” anasema Sekilojo.
“Baadaye nikaambiwa kwamba tayari viongozi wa Yanga (katika utawala ule ule wa Rashind Ngozoma Matunda) walikuwa wameshakubaliana. Nikaongea nao kidogo na wao wakata nibaki pale pale Afrika Kusini.
“Ilikubaliwa kwamba Yanga ilipwe dola 5,000 kama klabu na mimi binafsi nilipwe dola 5,000. Wakati huo zilikuwa pesa nyingi sana. Mshahara wangu ilibidi uwe dola 1,200. Nilipige hesabu kwa pesa za hapa Afrika Kusini Rand tukapata hiyo hesabu za Dola 1,200. Mazungumzo yakafika hapo. Ningeanza kupata utajiri zamani sana,” anaongeza Sekilojo.
Halafu kioja kikatokea. Wakati mazungumzo haya yakimalizika kwa amani huku pande zote mbili zikiwa zimekubaliana Yanga walikuwa wamebakiza mechi chache za Ligi. Rais wa Dinamo na watu wake hawakutaka Sekilojo arudi Tanzania na badala yake ajiunge moja kwa moja na timu yao. Yanga waligoma.
“Mpaka leo nina hasira na hili jambo. Yale yalikuwa maisha yangu, klabu zilikuwa zimekubaliana. Kwanini Yanga wanibanie nije kucheza tena katika Ligi? Walikuwa wanapata pesa nzuri katika lile dili na mimi nilikuwa Napata pesa nzuri na mshahara mzuri. Niliumia sana,” anasema Sekilojo.
Nini kilitokea baada ya hapo? “Wenzetu wale wana mipango mingi. Baada ya hapo nikasikia tu kwamba, nafasi yangu ilikuwa imechukuliwa na mchezaji kutoka Ghana. Dili likafa hapo hapo. Watu wa Yanga hawakuwa na nia ya kuniuza. Muda mwingi walikuwa wananibembeleza nibaki tu klabuni,” anaongeza.
Sekilojo anadai aliendelea kuihudumia Yanga kwa uaminifu mkubwa huku akiwa mmoja kati ya wachezaji mastaa klabuni. Dili hazikukauka kwake. Na zote zilimuandama zaidi kutoka kusini mwa Afrika.
Katikati ya siku moja kuelekea mwishoni mwa miaka ya 1990 alipokea simu akiwa nyumbani kwa staa mwingine wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein maeneo ya Mbagala. Mzungumzaji wa upande wa pili wa simu alikuwa anamtaka Sekilojo afike katika hoteli ya New Afrika kwa ajili ya mazungumzo ya mkataba na klabu moja ya Afrika Kusini.
“Nakumbuka nilikwenda mimi na Edibily (Lunyamila) ambaye alinisindikiza. Kufika pale kumbe aliyekuwa mwenyeji wangu ni Bosi Mkuu wa Magereza Afrika Kusini. Alikuwa amefika Dar es Salaam kwa ajili ya kikao cha wakuu wa Magereza nchi za SADC,” anasimulia Sekilojo.
Umri wa Sekilojo umesogea. Kwa sasa anagusa miaka 50 ingawa anaonekana bado kijana. Baadhi ya kumbukumbu zinaanza kupotea katika kichwa chake. Anaisahau timu ambayo Bosi huyu alimletea mezani kwake.
“Nilipokutana naye akaniambia kuna timu inanitaka Afrika Kusini na yeye alikuwa kiongozi wa hiyo timu. Ilikuwa timu mpya. Tayari walikuwa na tiketi yangu ya ndege kama tungekubaliana pamoja na barua kwa ajili ya viongozi wangu wa Yanga. Alitaka akaongee na viongozi wangu,” anasema Sekilojo.
“Wakati ule Mwenyekiti wangu alikuwa mzee Ngozoma Matunda na kwa kweli nilijua kwamba, asingeweza kuelewana lugha na bosi huyu kwa sababu Mzee Ngozoma alikuwa hawezi kuongea Kiingereza. Nikaamua nimpeleke kwa Francis Kifukwe, ambaye ingawa hakuwa kiongozi lakini alikuwa anaifadhili Yanga na alikuwa anaaminika. Masahibu yalianzia hapo.”
“Kifukwe alionyesha kukubali lakini akalazimisha kwamba, lazima nicheze mechi ya Jumatano iliyofuata dhidi ya Mtibwa. Hiyo ndio ilikuwa siku nilitakiwa Afrika Kusini. Nilijaribu kulazimisha, lakini Kifukwe alikuwa na sauti kubwa.
“Mara zote watu wa Yanga walikuwa wakinibembeleza na kuniambia kuwa nilikuwa mwenzao na ninahitajika sana klabuni. Huwa najilaumu sana kwanini sikuwa nafanya maamuzi magumu. Kiasi ulikuwa uzembe wangu lakini jamaa (viongozi wa Yanga) walikuwa wanatutengeneza tuwe mashabiki badala ya kuwa wachezaji..” anasikitika Sekilojo.
Tupo Afrika Kusini na huyu ndiye Sekilojo ambaye alikosa dili nne za kucheza soka la kulipwa Afrika Kusini. Kabla hata Mbwana Samatta hafikirii kwamba, siku moja angekuwa staa mkubwa pale Ubelgiji. Kabla hata Simon Msuva hafikirii kwamba siku moja angecheza Yanga na kuibuka staa mkubwa Ligi Kuu Morocco. Kabla hata Abdi Banda hajaenda kucheza soka la kulipwa.
Namuuliza Sekilojo safari yake ya soka iliyoanzia Mbeya kisha akatua Dar es Salaam kucheza Yanga. Haikuwa safari rahisi sana. Alikutana na mikasa ya kutatanisha. Moja kati ya mkasa wa kutatanisha ulitokea Tukuyu, Mbeya. Mchezaji mwenzake ambaye alikuwa rafiki yake wa karibu alifariki uwanjani wakati wakicheza mechi. Hawezi kusahau kabisa. Nini kilitokea?
Usikose mfululizo wa makala hizi za kusisimua za staa wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, Sekilojo Chambua akizungumza na mwandishi Edo Kumwembe nchini Afrika Kusini, kesho Jumatatu.