SEKILOJO : Nilishuhudia mchezaji mwenzangu akifia uwanjani-3
Muktasari:
- Ebu songa naye akue utamu zaidi wa mikasa yake, ambayo kila akiikumbuka huwa mnyonge kwani kama siyo mizengwe pengine leo angekuwa Sekilojo Chambua mwingine kabisa, akigusia mkasa wa kusikitisha uliomkuta mchezaji mwenzake aliyefia uwanjani, kivipi? Endelea naye...!
JANA katika mfululizo wa makala za nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Sekilojo Chambua, tuliona namna alivyofichua alivyopishana na mamilioni ya fedha kwa sababu ya utoto uliokuwa unamsumbua sambamba na kuwekewa zengwe na mabosi wake.
Ebu songa naye akue utamu zaidi wa mikasa yake, ambayo kila akiikumbuka huwa mnyonge kwani kama siyo mizengwe pengine leo angekuwa Sekilojo Chambua mwingine kabisa, akigusia mkasa wa kusikitisha uliomkuta mchezaji mwenzake aliyefia uwanjani, kivipi? Endelea naye...!
“WAKATI ule mwenyekiti wangu alikuwa Mzee Ngozoma Matunda na kwa kweli nilijua, asingeweza kuelewana lugha na bosi huyu kwa sababu Mzee Ngozoma alikuwa hawezi kuzungumza Kiingereza. Nikaamua nimpeleke kwa Francis Kifukwe, ambaye ingawa hakuwa kiongozi lakini alikuwa anaifadhili Yanga na alikuwa anaaminika. Masahibu yalianzia hapo.”
“Kifukwe alionyesha kukubali lakini akalazimisha lazima nicheze mechi ya Jumatano iliyofuata dhidi ya Mtibwa. Hiyo ndio ilikuwa siku nilitakiwa Afrika Kusini. Nilijaribu kulazimisha, lakini Kifukwe alikuwa na sauti kubwa.
“Mara zote watu wa Yanga walikuwa wakinibembeleza na kuniambia nilikuwa mwenzao na ninahitajika sana klabuni. Huwa najilaumu sana kwanini sikuwa nafanya maamuzi magumu. Kiasi ulikuwa uzembe wangu lakini jamaa (viongozi wa Yanga) walikuwa wanatutengeneza tuwe mashabiki badala ya kuwa wachezaji,” anasikitika Sekilojo.
Tupo Afrika Kusini na huyu ndiye Sekilojo ambaye alikosa dili nne za kucheza soka la kulipwa Afrika Kusini. Kabla hata Mbwana Samatta hafikirii siku moja angekuwa staa mkubwa pale Ubelgiji. Kabla hata Simon Msuva hafikirii siku moja angecheza Yanga na kuibuka staa mkubwa Ligi Kuu Morocco. Kabla hata Abdi Banda hajaenda kucheza soka la kulipwa.
Namuuliza Sekilojo safari yake ya soka iliyoanzia Mbeya kisha akatua Dar es Salaam kucheza Yanga. Haikuwa safari rahisi sana kwani anakumbuka mkasa uliwahi kumkuta mchezaji mwenzake aliyefia uwanjani.
ASHUHUDIA RAFIKIE AKIFIA UWANJANI
Sekilojo alianza kucheza soka kama masihara. Ni katika viwanja vya mch angani pale Mbeya. Tofauti na fikra za wengi, Sekilojo hakwenda Mbeya kucheza soka. Alikwenda kuishi na kaka yake, Yona Chambua ambaye alikuwa ni mtoto wa baba yake Mkubwa.
Mpira ulikuwa damuni kwake tangu akiwa mdogo. Ilianzia katika familia. baba yake, Johnson Chambua alikuwa mchezaji katika vikosi vya Mikoa ya Kilimanjaro na Tanga. Aliwahi pia kushiriki katika kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania katika Michuano ya Gossage ambayo kwa sasa inajulikana kama Chalenji.
“Huyu kaka yangu alikuwa anafanya mambo ya ufundi wa magari pale Mbeya akanichukua. Nilitoka upareni Tanga kumfuata Mbeya kwa ajili ya kuishi naye sio kucheza mpira. Alitaka nifanye kazi kama yake. Bahati nzuri nikaangukia katika soka kama masihara,” anasema.
“Nilianzia timu moja ya eneo letu inaitwa Majengo. Kuna mechi ambayo nilikwenda kama shabiki nikaishia kuingia kipindi cha pili na kufunga mabao mawili. Tulicheza na timu iliyoitwa Mbeya Kids ambayo ilikuwa chini ya Bosi wa Soka Mkoa wa Mbeya, Joel Mwakasala.
Tulifungwa mabao 3-2 lakini watu walishangazwa na kiwango changu kwa sababu nilikuwa mgeni na hawakunijua.”
Ukurasa wa maisha ya soka ya Sekilojo ulifunguliwa jioni hiyo. Baada ya mechi ilizuka vurugu kubwa kwa sababu mmiliki wa Mbeya Kids, Joel Mwakasala (Kwa sasa ni marehemu) ambaye alikuwa na uwezo wa kifedha alitaka kumchukua ajiunge na timu yake, lakini hapo hapo wahuni wa timu yake Majengo wakakasirika na kuanzisha vurugu.
“Mwishowe kabisa nikaamua kujiunga na timu ile kwa sababu ilikuwa na huduma nzuri na posho. Kaka yangu akahama Mbeya kurudi Dar es Salaam. Hapo ilibidi nibaki Mbeya na Mzee Mwakasala ambaye alikuwa anamiliki nyumba ya kulala wageni, Burudani Guest House ilibidi anifanye kuwa msimamizi wa ile sehemu, huku akinipa chumba cha kulala.”
Ni katika timu hiyo ndipo Sekilojo alipokutana na mchezaji mwenzake kijana, Lawrence Mwangomo ambaye alikuwa ameletwa katika timu na Mzee Mwakasala akitokea Shule ya Mwakaleli. Kwa sababu kwao kulikuwa Kyela, Mwangomo alichangia chumba kimoja na Sekilojo huku wakijenga urafiki mkubwa. Wachezaji wengine walikuwa wanalala makwao kwa sababu walikuwa wenyeweji wa Mbeya Mjini.
Katika tukio ambalo Sekilojo hawezi kulisahau ni pale umauti ulipomkuta Lawrence katika pambano moja la Ligi Daraja la Tatu kati ya Mbeya Kids iliyobadilishwa jina na kuitwa Ngorongoro, dhidi ya Boma FC ya Kyela ambayo mmoja kati ya wachezaji wake alikuwa beki mahiri wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Willy Martin ‘Gari Kubwa’.
“Nasikia uchungu mpaka leo. Kwanza kabisa mechi yenyewe ilijaa utata mwingi. Pambano la kwanza liliahirishwa kwa sababu kipa wa Boma aligongwa na gari asubuhi ya mechi. Yalijaa mazingira mengi ya kishirikina. Ikaamuriwa pambano likachezwe Kimbira Tukuyu baada ya wiki mbili.”
“Mechi ilikuwa ina upinzani mkali. Nilikuwa nacheza namba nane, Lawrence alikuwa anacheza namba sita. Ndani ya dakika tano tulionekana hatujajipanga vema. Ghafla wakati mpira ukiwa umeondoka katika eneo letu, Lawrence akaanguka bila ya kuguswa na mtu. Alikuwa peke yake wakati anadondoka. Hatukuona tukio kama kubwa sana, hivyo tukakusanyika upande mwingine wa uwanja na kuanza kupeana maelekezo kuhusu mechi.
Ghafla kocha wa timu yetu na msaidizi ambao walikuwa wameingia uwanjani ule kumtazama Lawrence wakaanza kupiga kelele.”
“Kila aliyesogea eneo lile alishika kichwa na kukimbia. Nilikuwa kijana mdogo, naogopa. Lawrence akakimbizwa hospitalini. Mechi ilivunjika palepale. Alipofikishwa hospitalini akafariki. Wachezaji wote tulikuwa tumepigwa ganzi.”
Sekilojo anakumbuka vema jinsi ambavyo kuna jitihada za mwisho za imani za kishirikina zilitumika kujaribu kumrudisha Lawrence duniani, lakini ilishindikana.
“Kuna mtu ambaye alikuwa ni kama mganga wa timu naye alijaribu kufanya imani za kishirikina kujaribu kumrudisha Lawrence duniani ilishindikana. Mwili wake ulikuwa wa moto na wengi tulihisi huenda bado yuko hai au amefariki kimazingara. Baadaye ilishindikana kabisa.Roho iliniuma sana. sikujua nini cha kufanya. Tukarudi Mbeya mjini. Kumbuka tulikuwa tunaishi chumba kimoja. Nguo zake na vitu vyake vyote bado vilikuwa chumbani,” anasimulia Sekilojo.
Kilichofuata kwa Sekilojo na wenzake ni kesho yake Sekilojo na timu nzima kurudi Tukuyu tena kwa ajili ya kwenda kumzika rafiki yao Lawrence nyumbani kwao Kyela. Hofu kubwa ilikuwa ni kwa Mzee Mwakasala. Alimchukua Lawrence kuichezea timu yake bila ya ruhusa ya wazazi.
Alipomaliza mtihani wa kidato cha nne akamchukua katika timu yake Mbeya mjini bila ya kuwasiliana na wazazi wake. leo alikuwa anawapelekea maiti, angewaambia nini? Angewaambia nini? Wangemuelewa?
Usikose mwendelezo wa makala haya ya kusisimua ya staa wa zamani wa Yanga, Sekilojo Johnson Chambua akizungumza na Mwandishi wa Gazeti la Mwanaspoti, Edo Kumwembe jijini Johannesburg, Afrika Kusini. Itaendelea kesho Jumanne...!