Segeja aweka rekodi mpya Kigamboni United
Muktasari:
- Segeja amejiunga na Kigamboni United msimu huu akitokea Coastal United ya Tanga, ambayo aliitumikia baada ya kujiunga nayo katika dirisha dogo la usajili la Januari 21, 2026. Kabla ya hapo, alikuwa akiichezea Tanzania Prisons ya Mbeya.
MSHAMBULIAJI wa Kigamboni United, zamani B19 FC, Abdulkarim Segeja, amefikisha mabao tisa katika Ligi ya Championship msimu wa 2026/27 na kuweka rekodi mpya ya ufungaji katika historia yake ya mashindano hayo, akiivunja rekodi yake ya mabao nane aliyoiweka akiwa na Copco FC ya Mwanza msimu wa 2023/24.
Segeja amejiunga na Kigamboni United msimu huu akitokea Coastal United ya Tanga, ambayo aliitumikia baada ya kujiunga nayo katika dirisha dogo la usajili la Januari 21, 2026. Kabla ya hapo, alikuwa akiichezea Tanzania Prisons ya Mbeya.
Mshambuliaji huyo alijiunga na Tanzania Prisons akitokea Copco FC ya Mwanza, iliyokuwa ikishiriki Ligi ya Championship. Akiwa na timu hiyo msimu wa 2023/24, alifunga mabao nane, rekodi ambayo sasa ameivunja baada ya kufikisha mabao tisa akiwa na Kigamboni United.
Segeja, ambaye pia amewahi kuzitumikia timu mbalimbali ikiwemo TRA United, amefikisha idadi hiyo ya mabao sawa na Oscar Paul wa Tanzania Prisons na Ramadhan Hashim Kalanje wa KMC FC.
Wachezaji hao wanamfuata kinara wa ufungaji, Hamdan Sarhani wa Transit Camp, aliyeongoza orodha hiyo akiwa na mabao 12.
Kiwango cha Segeja msimu huu kinaonekana pia katika mchango wake kwa timu, kwani amefunga mabao tisa kati ya 12 yaliyofungwa na Kigamboni United katika ligi hadi sasa.
Kigamboni United inashika nafasi ya nane kwenye msimamo ikiwa na pointi 16, huku mabao ya Segeja yakiwa sehemu kubwa ya mafanikio ya timu hiyo katika safu ya ushambuliaji.