Dar City, Patriots zatinga kibabe BAL
Muktasari:
- Dar City ilianza mchezo vizuri ikitawala robo ya kwanza ikitengeneza tofauti ya hadi pointi 17 ikionyesha timu hiyo ingeweza kumaliza mchezo ndani ya muda wa kawaida, lakini haikuwa hivyo.
DAR CITY imepata ushindi mgumu dhidi ya Munali Suns ya Zambia kwa pointi 102-99 katika mchezo wa nusu fainali ya Elite 16 Road to Basketball Africa League (BAL) 2027, Division East na kufuzu fainali iliyowapa tiketi ya kwenda kushiriki Ligi ya Kikapu Afrika (BAL 2027) kwa msimu wa pili mfululizo.
Dar City ilianza mchezo vizuri ikitawala robo ya kwanza ikitengeneza tofauti ya hadi pointi 17 ikionyesha timu hiyo ingeweza kumaliza mchezo ndani ya muda wa kawaida, lakini haikuwa hivyo.
Munali Suns ilirejea kwa nguvu, ikitumia upungufu wa Dar City katika kujilinda na kuongeza presha katika mashambulizi yake hatua iliyofanya timu hiyo ya Zambia kupunguza pengo hatua kwa hatua na hatimaye kulazimisha sare ya pointi 87-87 mwishoni mwa muda wa kawaida.
Ziliongezwa dakika tano, Dar City ilihitaji kurejesha umakini, kupunguza makosa na kutumia uzoefu wa wachezaji wake muhimu. Hatimaye ilipata pointi zilizohitajika na kuondoka na ushindi wa 102-99.
Ushindi huo unaonyesha uwezo wa Dar City kupambana katika mazingira yenye presha kubwa, pia unaacha maswali kuhusu namna timu hiyo inavyoweza kulinda uongozi mkubwa inapokuwa mbele kwa pointi nyingi.
Kwenye mchezo huo, wachezaji Jean Jacques Boissy, Tyler Bey na Nisre Zouzoua waliibeba Dar City, wakichangia kwa pamoja pointi 74 kati ya 102 zilizopatikana.
Nusu fainali ya pili, Patriots ya Sudan Kusini iliichapa Namuwongo Blazers ya Uganda kwa pointi 98-80 na kufuzu kucheza fainali dhidi ya Dar City, mchezo uliochezwa jana Jumapili, huku zote zikiwa na tiketi ya BAL 2027.