SCUD WA YANGA: kiboko ya Simba sasa mfugaji wa kisasa_2
Said Sued Scud
Muktasari:
Unaweza kushangaa kwani licha ya kufanya maajabu kwa kuifunga Simba mara mbili katika msimu mmoja, Scud alichezea Yanga kwa msimu huo mmoja tu, ulipomalizika alikwenda kuichezea Milambo ya Tabora aliyodumu nayo kwa miaka mitano.
KATIKA toleo la Jumanne iliyopita, mshambuliaji wa zamani wa Yanga aliyekuwa kiboko ya Simba, Said Sued ‘Scud’ alizungumzia jinsi alivyoondoka katika klabu hiyo baada ya msimu mmoja wa mafanikio. Endelea…
Unaweza kushangaa kwani licha ya kufanya maajabu kwa kuifunga Simba mara mbili katika msimu mmoja, Scud alichezea Yanga kwa msimu huo mmoja tu, ulipomalizika alikwenda kuichezea Milambo ya Tabora aliyodumu nayo kwa miaka mitano.
Habari zilizotawala wakati huo ni kwamba Scud alikuwa mwenye maringo hasa baada ya kuifunga Simba mara mbili, rekodi yake hiyo ya kuvutia ilimpa heshima ya kipekee mbele ya mashabiki wa Yanga.
Hali hiyo ilitokana na ukweli kwamba enzi hizo mechi za Yanga na Simba zilikuwa na mvuto wa kipekee, ilikuwa ni Simba na Yanga hasa. Lakini Scud anasemaje kuhusu kuondoka kwake Yanga.
“Kila kitu huwa naamini ni mipango ya Mungu na siwezi kumlaumu yeyote kutokana na jambo hilo,”anasema Scud.
Scud anasema, anachokumbuka baada ya ligi kumalizika alikwenda kwa bosi wake anamtaja kwa jina la Ramesh Patwa ili apewe tiketi ya ndege ya kurudi kwao Kigoma.
Alipewa tiketi kama kawaida na fomu ya usajili ili aijaze kwa ajili ya msimu ujao akaipokea, hata hivyo alishapewa taarifa, alikuwa kwenye mpango wa kusajiliwa na kuachwa kwa kile kilichodaiwa kuwa alikuwa na maringo.
“Nilipotoka nje nilikutana na Abbas Mchemba na Dadi Fares wote walikuwa wachezaji wa African Sports ya Tanga na kuniambia kuwa wanakwenda Tabora kusajili Milambo, tuliachana hapo mimi nikaelekea nyumbani,” anasema Scud ambaye ni kaka wa kuzaliwa wa mshambuliaji wa Coastal Union, Hussein Sued.
“Wakati huo niko na fomu yangu, lakini kumbe wale wachezaji niliokutana nao Dadi na Mchemba walipeleka taarifa Milambo ambayo ilimtuma mchezaji wao wa zamani Wastara Baribari anifuate Kigoma. Tulizungumza na kukubaliana ndipo nikaenda Milambo na kusajiliwa rasmi,”anaeleza Scud na kuwataja aliosajiliwa nao kuwa ni Jobe Ayoub, Said John na huo ukawa mwisho wake Yanga.
Anasema, hapo alicheza misimu mitano na baada ya hapo, alirudi kwao Kigoma na kusajiliwa na National sasa ni Mbanga FC iliyokuwa Daraja la Pili.
Akizungumzia sababu ya kustaafu soka anasema kuwa aliamua tu: “Sikupatwa na majeraha yoyote hadi kustaafu, niliamua mwenyewe tu.”
Baada ya mazungumzo hayo mwandishi alimshawishi Scud amtembeze zizini kwenye mifugo yake na kujionea kilichokuwepo, naye bila kusita alifanya hivyo.
Walikuwepo ngomb’e 10 na kati yao, wanne ni wadogo (ndama) na wengine ndiyo wakubwa.
Ngombe ambao walikuwa na uwezo wa kutoa maziwa ni wanne na humo ndani alikuwepo kijana mmoja anayeitwa, Hussein Suleiman aliyekuwa anakamua.
Scud anasema, ana uwezo wa kupata maziwa yasiyopungua lita 40 kwa siku baada ya kukusanya ya asubuhi na jioni.
Maziwa hayo ni biashara, lita moja anauza Sh. 1500 na bado anapata ya kutumia nyumbani, katika biashara ya maziwa, Scud ana uwezo wa kukusanya Sh. 60,000 kwa siku sawa na Sh 1.8 milioni kwa mwezi.
“Yapo maziwa ambayo nayatoa kwa kuuza rejareja lakini wengi wa wateja wangu ni watu wanaochukua na kulipa kwa makubaliano ya mwezi au wiki,” anasema na kuongeza kuwa fedha zinazopatikana ndizo zinazoendesha maisha yake na kusomesha watoto.
Sababu ya kuwa mfugaji
Gharama ya ng’ombe mkubwa wa maziwa mwenye ubora ni kuanzia Sh. 1.5 Milioni kwa sasa.
“Nilianza kufuga kama miaka mitano iliyopita. Nilianza na ng’ombe mmoja lakini sikumbuki nilimnunua kiasi gani,” anasema na kufafanua kuwa mtaji huo aliupata kutoka kwenye biashara yake ya kulangua mafuta ya magari (oil) aliyokuwa anauza Mwanga sokoni.
Aliyemshawishi afuge akaachana na biashara ya oil ni Alhaj Haruna Shaaban Msangi ambaye alikuwa meneja wa tawi wa kampuni ya ORS Kigoma alikokuwa akinunua oil. “Namshukuru Msangi kwani ndiye aliyenishauri jambo hilo, nikanunua ng’ombe mmoja,” anasema Scud.
“Ng’ombe huyo alikuja akazaa, wakazaana lakini tangu nianze hadi leo kama nisingekuwa nawatoa, wangekuwepo zaidi ya ng’ombe 16 lakini wengine nimekuwa nawatoa kwa kuwauza na wengine, nachinja. “Huwa nawachinja kama sadaka kwa Mwenyezi Mungu, si unajua Mungu ndiyo ametupa na yeye tunatakiwa kumkumbuka kwa kile alichotujalia.”
Kuhusu ukulima, Scud anasema, huwa analima mahindi na mihogo kwa ajili ya chakula: “Marehemu mama alituachua shamba kama ekari 20, lakini nalima kulingana na nguvu ninazokuwanazo kwa wakati huo.”
“Naweza kulima ekari tano hivi, mbili zinaweza kuwa za mahindi na nyingine mihogo au nikaongeza, inategemea na nguvu ninazokuwa nimepata kwa wakati huo,”anaeleza Scud.
Soka la sasa na enzi zao
“Mpira wa sasa ni pesa, zamani tulikuwa tunacheza kwa wito hakukuwa na pesa, tulikuwa tunacheza kwa mapenzi ya moyoni,’’ anasema.
“Wachezaji wa sasa unaona hawajitumi, wanacheza mpira utafikiri hawana malengo sijui inakuwaje lakini huenda ni kizazi tu.
“Enzi zetu kulikuwa na watu wenye majina, ukimsikia mtu kama Madaraka SelemanI ukimuona hauishiwi hamu kumtazama lakini sasa utamsikia mchezaji jina kubwa lakini uwanjani ndiyo hivyo.”
Scud anakwenda mbali na kuwaponda washambuliaji kwa kusema: “Enzi zetu ukiwa mshambuliaji, una hamu ya bao, wakati wote unatafuta nafasi ya kufunga.”
“Straika anacheza dakika 45 hajapiga shuti golini, anaingia ndani ya 18 mara nne, tano lakini hatishi sijui kwa nini,”anahoji Scud.
“Wakati tunacheza, tukiwa katika maandalizi yetu, kwanza tulikuwa tunauliza hivi huyu fulani kwenye nafasi hii vipi, unapata ushauri kutoka kwa watu mbalimbali.
“Haitoshi, tulikuwa tunafanyia kazi kabla, uzuri na ubora wa huyo mpinzani wako ili kwenda naye sawa, wasiwasi wangu kwa hawa wenzetu sijui kama huwa wanafanya hivyo.”
Yanga ikiboronga
Anasema, kutokana na mapenzi ya dhati aliyonayo Scud kwa Yanga, huwa anakosa amani anapoishuhudia klabu yake hiyo ikifungwa.
“Yaani inaniuma sana, unajua Yanga naipenda kutoka moyoni kiasi ambacho, mara nyingine nashindwa kuangalia mechi zao kwa sababu ya kuhofia presha,”anasema Scud.
“Yaani niwe naangalia mechi halafu tufungwe, nakosa amani na siku hiyo huwa hapalaliki.”
Magoso alimnyima raha
Kila mbabe ana mbabe wake, hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa mkali huyo wa mabao baada ya kutamka kuwa, Fikiri Magoso wa Simba ndiyo beki pekee aliyekuwa anamtishia amani walipokutana.
“Magoso ndiye beki namba moja niliyemhofia kila tulipokutana, alikuwa na uwezo, ana nguvu, kasi na akili na kila kitu,’’ anasisitiza.
Jina la Scud
Wakati jina la Scud lilivuma enzi zake Said mwenyewe akizungumzia jina hilo anasema: “Hadi leo hata ukiniuliza nani hasa aliyenitungia jina hilo sikubahatika kumjua, lakini nakumbuka tu nilikuwa naitwa kwa jina hilo kwa sababu ya mabao hasa baada ya kuifunga Simba.