Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SABEBE: Soka haliendelei wapigaji wengi-1

Abdallah Saleh "Sabebe", mwenye jezi nyekundu.

Muktasari:

UNAMKUMBUKA yule straika wa zamani wa Coastal Union aliyekuwa umbile dogo lakini mbishi sana, aliyetamba nchini miaka ya 1990-2000 kwa kutupia mabao?

UNAMKUMBUKA yule straika wa zamani wa Coastal Union aliyekuwa umbile dogo lakini mbishi sana, aliyetamba nchini miaka ya 1990-2000 kwa kutupia mabao?

Mwonekano wake uwanjani ulimtofautisha na wenzake sababu ya rangi yake. Alikuwa shombe fulani, lakini alikuwa akipiga soka kweli kweli. Namzungumzia, Abdallah Saleh maarufu kwa jina la utani kama Sabebe.

Mkali huyo wa kimataifa aliyewahi kuzichezea timu za taifa kuanzia zile za vijana hadi Taifa Stars anaishi jijini Tanga, akiendesha shughuli zake za kila siku kujitafutia riziki. Mwandishi wa makala haya aliyekuwa jijini humo hakuona vema kutoka bila kumsaka straika huyo na kufanya naye mazungumzo.

Mkali huyo aliyekuwa akitumia mguu wa kushoto na kuwasumbua mabeki wengi wakali sambamba na kuwatungua makipa waliotamba enzi akicheza alifunguka mengi na kubwa alieleza sababu ya soka la Tanzania kushindwa kusonga mbele. Sabebe alisema hali hiyo imechangiwa sana na wapigaji wengi ambao akili zao zipo kujinufaisha tu.

 

KIVIPI?

Sabebe aliyekuwa mmoja ya wachezaji wa chache waliowahi kutamba nchini bila kuzichezea Simba na Yanga, akiwa kwenye nyumba yake iliyopo Barabara ya 15 ambako nje yake kuna duka ya bidhaa za vyakula.

Hapo alikuwa akipiga soga na watu wengine ambapo aliweka bayana kinacholifanya soka la Tanzania lisisonge mbele na kumfanya kujitenga kabisa na familia ya soka licha ya kwamba alicheza kwa mafanikio na kutajwa kila kona ya nchini.

“Soka linaendeshwa kijanjajanja sana, halina mpango ya kufikia malengo na mafanikio, lipolipo kwa sababu wapigaji wamekuwa wengi mno katika sekta hiyo.” anasema.

Anasema tofauti na miaka ya nyuma wakati akicheza soka halikuwa na fedha wala vitu vya maana, lakini ulikuwa ukiona tofauti hata ya kiuchezaji kwa kusaka mafanikio. Sio sasa wanachezaji wanalipwa vizuri, lakini cha kushangaza hakuna mabadiliko yoyote.

“Hili ndilo linalonifanya hata nisipende kwenda uwanjani kuangalia soka, hutokea bahati mbaya tu kushuhudia mechi za ligi kupitia kwenye runinga na kile ambacho huwa nakiona kinashangaza sana, hakuna soka wala nini,” anasema.

Sabebe anasema wachezaji wanaokuzwa majina yao na vyombo vya habari hawachezi soka kulingana na sifa wanazopewa.

“Hata wachezaji wa kigeni wanaosajiliwa au kuletwa nchini hawana kitu cha zaida kulinganisha na wazawa, lakini kwa vile kuna watu wanapiga cha juu wanatulazimisha tuamini ni wakali, wakati hawaleti mabadiliko yoyote.”

 

KIZUNGUMKUTI

Sabebe anafunguka zaidi na kueleza namna usajili wa wachezaji wa kigeni kwa klabu kubwa za Simba, Yanga na Azam ulivyojaa ujanjaujanja.

“Nashangaa klabu zinahangaika kusajili wachezai wa kigeni ambao hawana msaada na wala watu hawashtuki, wachezaji hao wanafanya au kucheza soka kama wazawa tu, na hii inatokana na ubabaishaji wa viongozi,” anasema.

Anasema viongozi wengi sio wabunifu na watu wa soka zaidi ya kufikiria namna ya kuvuna fedha kwa hila kupitia usajili wa wachezaji hao wa kigeni na hata wakati mwingine wa hapa hapa nyumbani.

“Ipo wazi sehemu ya usajili imekuwa ndiyo watu wanayopiga hela, anatafutwa mchezaji wanayemjua, halafu wanakatiana asilimia 10 (10%) basi. Hawana uchungu wa kutafuta wachezaji watakaosaidia timu.

“Profesheno anapokuja nchini ni kwa ajili ya kucheza na siyo kukaa benchi, lakini hapa kwetu wanasajiliwa wachezaji wa benchi au hata kama anapewa nafasi ya kucheza ujue viwango vyao havina tofauti kabisa na wazawa,” anafunguka.

 

MAKOCHA PIA

Sabebe anasema hata kwenye suala la makocha wa kigeni wengi wanaoletwa nchini, ni madudu tupu.

“Iko hivyo pia kwa makocha, klabu zinatafuta makocha ambao wataweza kuwaendesha siyo wale wenye uwezo ambao wataendesha timu kiprofesheno. Utaona, akitokea kocha mwenye msimamo kamwe hawezi kudumu katika timu.

“Yule mdhaifu anayekubali kupangiwa timu, ndiyo anayeweza kudumu. Sitaki kuamini kuwa timu zinashindwa kutafuta wachezaji au makocha wenye uwezo huo kwa sababu ya gharama isipokuwa ni hiyo mizengwe yao tu.

“Ukiangalia na kufuatilia kwa umakini, Ligi ya Tanzania ndiyo inayolipa kwenye soka Afrika Mashariki na nchi nyingine, hivyo wanao uwezo wa kusajili mahali kwingine kokote na kupata wachezaji watakaolibadilisha soka letu, lakini watu hawapo makini.”

 

AGOMEA WAGENI JIRANI

Sabebe anasema hajui soka la Tanzania limeingiliwa na nini kiasi cha kufikia hatua ya kusajili wachezaji wa kigeni kutoka nchi za Afrika Mashariki.

“Wachezaji wetu wengi ni kutoka, Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya kidogo na wanaotoka Afrika Magharibi ni wachache sana. Maoni yangu viongozi wa hizo timu, wangeangalia mbali. Nawashauri waende Amerika ya Kusini katika nchi za Colombia, Equador huko kuna wachezaji wengi wenye ubora, wa bei chee na wana uchungu na maisha.”

“Wakija hapa lazima watapambana na watafanya vizuri tu, watasaidia hata hicho kilio chao cha upangaji wa matokeo. Hawa jirani zetu wana mambo mengi, wanapokuja hapa wanajua ni sehemu ya kujizolea pesa tu.

“Kabla ya kuja wanapambana sana ilimradi wasajiliwe na wakipata nafasi wanakaza mechi mbili tatu na baada ya hapo wanakuwa wa kawaida tu,” anasema Sabebe.

Sabeba anasema pia soka la Tanzania na mataifa hayo ya jirani viwango havitofautiani sana, na kushangaa inakuwaje Wakenya waje kucheza Tanzania, lakini Watanzania wakwame kucheza katika taifa hilo na mengine ya jirani.

“Huu ni upuuzi, waliopo kwenye soka wazinduke na kufanya mambo kama watu wenye mipango ya kuinua soka la Tanzania sio kuchumia matumbo,” anasema.

 

WAZIRI WA ULINZI

Pamoja na kukerwa na suala la usajili wa wachezaji wa kigeni, badala ya kuwa na mipango ya kuendeleza vipaji vya Tanzania ili vije kulinufaisha taifa kwa siku za usoni, Sabebe anawavulia kofia baadhi ya nyota hao wa kigeni.

“Ukiangalia Azam, timu ninaamini ina uwezo wa kusajili itakavyo na kuweza kufanya vizuri kama ilivyo TP Mazembe kwa sababu ina pesa, wachezaji walioitendea haki ni Waivorycoast tu, ambao nao sasa wanaanza kuonekana kama wa kawaida kwa sababu hawana washindani na watu wa kucheza nao kikosi na hata kwenye Ligi Kuu.”

“Mtu kama Pascal Wawa ‘Waziri wa UIinzi’, Kipre Tchetche ni wachezaji wazuri na kama wangepatikana watano kama hao katika kikosi hicho na hata timu nyingine wangekuwa na manufaa kwa soka la Tanzania,” anasema.

Unadhani kwa nini amewataja Kipre Tchetche na Wawa na sio Donald Ngoma au Thabani Kamusoko wa Yanga ama Justice Majabvi au Hamis Kiiza wa Simba? Tukutane Jumanne ijayo upate majibu kwani simulizi la Sabebe litaendelea tena hapa.