Saada Mabere: Msituhukumu kwa mavazi yetu
Muktasari:
- Kauli ya beki huyo inakuja wakati baadhi ya wachezaji wa kike wamekuwa wakikabiliwa na maoni na mijadala kuhusu mwonekano wao, mavazi wanayovaa na hata namna wanavyozungumza.
BEKI wa Yanga Princess, Saada Mabere amewataka watu kuacha kuwahukumu wachezaji wa kike kutokana na mavazi au mwonekano wao, akisisitiza kuwa wanapaswa kutambuliwa na kuthaminiwa kwa vipaji na uwezo wao wa kucheza soka.
Mabere amesema aina ya mavazi anayovaa mtu haipaswi kutumiwa kama kipimo cha kutathmini uhalisia wake, akieleza kuwa mwanamke anaweza kuvaa mavazi yanayoonekana kuhusishwa na wanaume bila kupoteza uhalisia wake.
Kauli ya beki huyo inakuja wakati baadhi ya wachezaji wa kike wamekuwa wakikabiliwa na maoni na mijadala kuhusu mwonekano wao, mavazi wanayovaa na hata namna wanavyozungumza.
"Huwa sipendi watu wanavyotuchukulia kwa sababu ya kuvaa mavazi ya kiume. Siyo kwamba mavazi hayo yanakutoa kwenye uhalisia wako. Tunaamini mavazi ni mavazi tu, unaweza kuvaa na ukaendelea kuwa katika uhalisia wako. Watu waamini katika vipaji vyetu badala ya kutuangalia kwa mambo mengine," amesema Mabere.
Beki huyo alisisitiza kuwa wachezaji wanapaswa kupimwa kwa mchango wao ndani ya timu, nidhamu na uwezo wa kutekeleza majukumu wanayopewa na makocha, badala ya kupewa majina ya kudhalilisha kama ‘jike dume’ kwa sababu ya mwonekano wao au kucheza mchezo wa soka ambao kwa muda mrefu umehusishwa zaidi na wanaume.
Mabere, aliyesajiliwa na Yanga Princess msimu huu akitokea Ruangwa Queens iliyoshuka daraja msimu uliopita, amekuwa akipata nafasi ya kuanza katika kikosi hicho, akicheza pamoja na nyota wa kimataifa akiwamo Igwe Uzoamaka.
Akizungumzia nafasi yake katika kikosi hicho, Mabere amesema uzoefu alioupata katika mashindano mbalimbali umemsaidia kuhimili ushindani na kupata nafasi ya kucheza mbele ya wachezaji wenye majina makubwa.
"Ni uzoefu tu nilionao unaonifanya niweze kucheza mbele ya wachezaji wakubwa wa Yanga. Nimecheza mashindano mengi makubwa ya kimataifa," amesema.