Shalulile na rekodi ya Okello
BAADA ya mshambuliaji wa Yanga, Peter Shalulile kufikisha idadi ya mabao saba, asisti moja aliyoyafunga katika mechi alizocheza tangu amejiunga na Yanga, imeelezwa anaweza kufikia au kuvunja rekodi ya staa wa zamani wa timu hiyo, Allan Okello.
Msimu wa 2025/26, Okello ambaye kwa sasa anacheza AS FAR Rabat ya Morocco alimaliza na mabao 14, lakini kinara wa mabao 17 ni aliyekuwa mshambuliaji wa Singida BS, Mossi Ndumumwe anayechezea MC Algier.
Mechi alizofunga Shalulile, Novemba Mosi dhidi ya Kagera Sugar dakika 26, dhidi ya Simba Oktoba 10, dakika 4, dhidi ya Fountain Gate FC dakika 26 Agosti 31, dhidi ya JKT Tanzania dakika 63, iliyopigwa Agosti 24, Agosti 15 dhidi ya Namungo alifunga dakika ya 90 na Polisi Tanzania iliyochezwa Novemba 21.
Jambo ambalo staa wa zamani wa timu hiyo na Taifa Stars, Mohamed Hussein “Mmachinga” alisema endapo akicheza kwa umakini na utulivu, anaweza kufikia mabao ya Okello.
“Shalulile anacheza kwa presha kubwa, anataka kuonyesha alichofanya alikotoka, lakini akitulia na kuongeza umakini inawezekana ila nje na hapo itakuwa hadithi,” alisema.
Staa mwingine aliyechangia hilo ni kiungo wa zamani wa timu hiyo, Adeyum Ahmed Saleh ambaye kwa sasa anacheza Mbuni FC alisema: “Shalulile ni mshambuliaji mzuri, anahitaji utulivu na asicheze kwa presha kubwa, tuliyocheza timu hizo tunaelewa presha inavyokuwa kutoka kwa mashabiki, akipata utulivu anaweza kufikia na akazidi idadi ya mabao 14 yaliyofungwa na Okello.”
Nyota wa kimataifa wa zamani aliyewahi kukipiga Yanga, Mtibwa Sugar na Taifa Stars, Abdi Kassim ‘Babi’ alisema: “Inawezekana Shalulile kuyafikia na kuzidi mabao 14 yaliyofungwa na Okello, jambo la msingi kulinda kiwango chake na kuzidisha bidii ya mazoezi, kutokana na ushindani wa namba katika nafasi anayocheza.
Aliongeza: “Ni mchezaji aliye na uwezo wa kufunga kipindi cha kwanza na cha pili, kikubwa ni yeye afokasi zaidi na kufunga kuliko presha ya mashabiki kutokana na ukubwa wa jina lake.”