Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Robertinho, Gamondi mtegoni Tanga

LEO Uwanja wa Mkwakwani pale jijini Tanga kipyenga cha kwanza kwa ajili ya mechi za Ngao ya Jamii kuashiria kufunguliwa kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2023/24 kitapulizwa na Yanga itakuwa ikicheza na Azam FC kisha kesho Simba na Singida Fountain Gate zitakutana, lakini kubwa zaidi ni makocha wa timu hizo nne kuwa mtegoni wakiwaza watoke vipi.

Msimu huu mechi za Ngao ya Jamii zitakuwa tofauti kidogo kwani zitachezwa kwa muundo wa mtoano ikihusisha timu nne na mechi zitapigwa kama ilivyoelezwa hapo juu kisha mshindi kati ya Yanga na Azam atakutana na mshindi kati ya Simba na Singida katika fainali na hapo ndipo bingwa atapatikana.

Mechi hizo ni kama zimekuwa mtego kwa makocha wa timu hizo nne kutokana na kila mmoja kutumia ‘siasa za soka’ katika kueelezea maandalizi yake na kila mmoja amehitaji muda zaidi ili kutengeneza timu.

Si Miguel Gamondi wa Yanga, Youssouph Dabo wa Azam, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ wa Simba, wala Hans van der Pluijm, kila mmoja katika mahojiano waliyofanya wamekiri kuhitaji muda zaidi ili kujenga vikosi vyao.

Hata hivyo, wakati makocha hao wakihitaji muda ili kuimarisha timu zao kimbinu, muda wenyewe hautaki kuwasubiri na tayari umeamuru kuanzia leo kila kocha atuonyeshe kile alichokifanya kwenye kambi ya maandalizi ya msimu mpya sambamba na usajili wake.

Jambo hilo ni kama mtego kwa makocha kwani kutokana na asili ya soka la Tanzania, huenda makocha wawili hadi watatu kati ya wanne hao wakakalia kuti kavu kama timu zao hazitafanya vizuri au hawatawatumia vyema wachezaji waliosajiliwa ambao baadhi yao ni vipenzi vya viongozi, mashabiki na wengine wa makocha hao hao.

Hizi hapa sababu zinazomfanya kila kocha kati ya wanne hao kujiuliza atoke vipi kwenye michuano hii ya Ngao ya jamii kutokana na hali halisi ya timu yake na matarajio ya wengi.


GAMONDI - YANGA

Mashabiki wa Yanga wanahitaji kumwona Gamondi akiendeleza alipoishia Nabi, hawako tayari kuona timu ikitolewa mapema kwenye Ngao ya Jamii ikiwa wamebeba taji hilo kwa misimu miwili mfululizo na hii ni presha ya kwanza kwa Gamondi.

Presha ya pili kwa kocha huyo ni kupanga kikosi chake. Gamondi ni mpya na ameikuta Yanga ikiwa na wachezaji kadhaa waliotengeneza uimara wa timu hiyo kwa msimu uliopita, pia imesajili mastaa wapya kwa muda aliokuwa nao atakuwa tayari amepata kikosi cha kwanza.

Hata hivyo, katika eneo hili, presha kubwa inakuja kutoka kwa viongozi na mashabiki wa Yanga kwani kuna baadhi ya wachezaji ni vipenzi vyao, hivyo kama Gamondi ataona hawafai na kuwaweka nje na kwa bahati mbaya timu ikapoteza basi kazi anayo.

Mastaa wapya kwa Yanga msimu huu ni Nickson Kibabage, Jonas Mkude, Gift Fred, Kouassi Attohoula Yao, Pacôme Zouzoua, Hafiz Konkoni, Maxi Nzengeli na Mahlatse Makudubela ‘Skudu’.


ROBERTINHO - SIMBA

Mwamba huyu kutoka Brazil, Simba imemtega kiaina kwa kumpa asilimia kubwa ya mahitaji aliyotaka katika msimu ujao ikiwemo wachezaji na wasaidizi wa benchi la ufundi na kinachofuata sasa anawaza atoke vipi akianza na mechi za Ngao ya Jamii.

Lengo la Simba msimu ujao ni kubeba kila kombe itakaloshiriki ndani ya nchi na kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa hivyo ni dhahiri Ngao ya Jamii ni moja ya lengo lao na Robertinho anatakiwa kupambana kuhakikisha Simba inatwaa taji hilo. Hii ni presha ya kwanza kwa kocha huyo.

Presha ya pili, ni Wekundu hao kutaka mapinduzi kisoka baada ya kuvumilia misimu miwili iliyopita hivyo kama Robertinho ataanza kwa kudondosha Ngao ya Jamii tayari ataingia kwenye mfumo kwani itakuwa ngumu kwa Simba kuendelea kumvumilia ilihali amepewa kila kitu.

Tatu ni kupanga kikosi na kuwapa nafasi wachezaji, kama ilivyo kwa karibu timu zote za Bongo, kuna wachezaji ambao ni vipenzi vya mashabiki, wengine vipenzi vya makocha na wengine uongozi hivyo kama Robertinho atashindwa kuendana na mdundo huu basi huenda akakutana na presha asiyoidhania.

Wachezaji wapya waliosajiliwa Simba msimu huu ni, David Kameta ‘Duchu’, Hussein Bakari ‘Kazi’, Abdallah Hamis, Shaban Chilunda, Che Malone Fondoh, Willy Onana, Kramo Aubin, Fabrice Ngoma, Luis Miquissone na Hussein Abel.


DABO - AZAM

Azam haitaki masihara kabisa msimu ujao kwani ilianza maandalizi hata kabla msimu jana haujaisha na ilimshusha kocha mkuu mpya Msenegal Dabo ili kukisoma kikosi na kufanya usajili, pia kupunguza watu ili awe na jeshi moja litakalotii kauli na kufuata maelekezo yake.

Baada ya hapo Azam ikajiwekea malengo ya kutwaa makombe yote ya ndani ikianza na Ngao ya Jamii, pia ikitaka kufuta uteja kutoka kwa Simba na Yanga na hapo ndipo presha ya kwanza inapanda kwa Dabo kwani anahitajika leo kuifunga Yanga ili kutotia doa mkataba wake.

Presha nyingine kwa Dabo ni juu yake dhidi ya vigogo wa Azam. Kocha huyo kila alichoomba amepewa ndani ya timu hiyo kuanzia wachezaji, benchi la ufundi na hata mazingira ya kambi, hivyo ni kama mabosi wa Azam wamemfanyia hivyo makusudi ili pale atakaposhindwa kufikia malengo wamuulize nini hakupewa. Huenda Ngao ya Jamii ikafungua au kufunga imani ya viongozi na wadau wa Azam juu ya kocha huyo.

Wachezaji wapya waliosajiliwa na Azam katika dirisha hili ni Feisal Salum ‘Fei Toto’, Alassane Diao, Cheikh Sidibe, Djibril Syllah na Yanick Bangala.


PLUIJM - SINGIDA FG

BAADA ya kuiwezesha Singida kumaliza msimu wake wa kwanza Ligi Kuu katika nafasi nne za juu, sasa Pluijm ameeingia kwenye presha ya mwanzo wa msimu atakayoanza kuipata kesho kwenye mechi dhidi ya Simba.

Mabosi wa Singida wanaamini, timu yao kutokana na usajili iliofanya inaweza kushindana na Simba, Yanga na Azam na kupata ushindi hivyo mtego wa kwanza kwa Pluijm ni kushinda dhidi ya Simba kesho na kutinga fainali.

Sehemu ya pili inayompa presha Pluijm ni kwenye kikosi chake na timu hiyo imesajili wachezaji wasiopungua 18 wapya hivyo kuwapanga na kupata kikosi cha kwanza ni ngumu na hapo hapo kuna wachezaji wa mabosi.

Hapa Pluijm kama hatachanga vyema karata zake ataanza kuona rangi ya pili ya Singida na viongozi wake.

Tatu ni timu hiyo kutotaka kuishi kwa mazoea, licha ya kuwa Pluijm ni kocha pendwa kwa baadhi ya viongozi wa juu wa timu hiyo, lakini msimu huu hawataki kuishi kwa mazoea na tayari ameambiwa kama hatotimiza malengo ikiwemo kutwaa Ngao ya Jamii, maisha yake yatakuwa mafupi kwa walima alizeti hao.

Singida msimu huu imesajili wachezaji wapya 18, Beno Kakolanya, Yahya Mbegu, Gadiel Michael, Kelvin Kijiri, Kharid Ugego, Habibu Kyombo, Dickson Ambundo, Thomas Ulimwengu,  Amos Kadikilo, Ibrahim Rashid, Laurian Makame, Joash Onyango, Duke Abuya, Nicholaus Wadada, Enock Atta, Morice Chukwu na Marouf Tchakei.