Rekodi kibao hatua ya makundi Kombe la Dunia U-17
Muktasari:
- Takwimu hizo zinaonyesha namna mashindano hayo yalivyokuwa na ushindani mkubwa hasa kwa washambuliaji kutikisa nyavu, huku baadhi ya timu na wachezaji wakitengeneza rekodi ambazo zitakumbukwa kwa muda mrefu katika historia ya michuano hiyo.
HATUA ya makundi ya Kombe la Dunia la vijana chini ya miaka 17, michuano inayofanyika nchini Qatar, imehitimishwa kwa kuweka rekodi mpya baada ya kufungwa mabao 268, idadi iliyoipiku ya awali mabao 250 iliyowekwa katika mashindano ya 2025.
Takwimu hizo zinaonyesha namna mashindano hayo yalivyokuwa na ushindani mkubwa hasa kwa washambuliaji kutikisa nyavu, huku baadhi ya timu na wachezaji wakitengeneza rekodi ambazo zitakumbukwa kwa muda mrefu katika historia ya michuano hiyo.
Kwa mujibu wa takwimu, mabao 40 yalifungwa katika Kundi H pekee, huku Hispania ikiwa timu iliyofunga mabao mengi zaidi ambayo ni 22 ikicheza mechi tatu dhidi ya China, Fiji na Morocco.
Hispania ilianza kwa ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya China, ikaifumua Fiji mabao 15-0 na kumalizia kwa kuifunga Morocco 2-0, matokeo yaliyoifanya kumaliza hatua ya makundi ikiwa na rekodi ya mabao 22.
HISPANIA YATISHA
Miongoni mwa matokeo yaliyoacha alama kubwa ni ushindi wa Hispania wa mabao 15-0 dhidi ya Fiji, ambao ulikuwa ushindi wa pili kwa ukubwa katika historia ya mashindano hayo.
Rekodi hiyo inafuata ushindi wa Morocco wa mabao 16-0 dhidi ya New Caledonia katika mashindano ya 2025.
Katika mchezo huo, Rafael Cruz aliandika rekodi baada ya kufunga mabao matano, idadi ambayo haijawahi kufikiwa na mchezaji mmoja katika mechi ya Kombe la Dunia la U-17 la wanaume.
Cruz alifunga dakika ya tano, 10, 21, 57 na 65, huku Roberto Tomás na Guillermo Trujillano kila mmoja akifunga matatu.
Upekee wa mchezo huo ni kwamba kwa mara ya kwanza katika historia ya fainali za dunia za wanaume za soka, wachezaji watatu kutoka timu moja walipata mpira wa kumbukumbu baada ya kufunga hat-trick katika mechi moja.
HAT-TRICK TISA
Hatua hiyo ya makundi pia imeweka rekodi ya hat-trick tisa, idadi iliyovunja rekodi ya awali ya hat-trick sita zilizofungwa katika mashindano ya 2025.
Wachezaji waliofanikiwa kufunga hat-trick ni Jona Benkotic na Toni Ruso wa Croatia, Kim Jiwoo (Korea Kusini), Maki Kitahara (Japan), Owen Mukisa (Uganda) na Sukhrob Sadirjanov (Uzbekistan).
Wengine watatu walitoka Hispania, ambao ni Rafael Cruz, Guillermo Trujillano na Roberto Tomás, walioandika historia yao katika ushindi wa mabao 15-0 dhidi ya Fiji.
ARGENTINA, CHILE ZAGEUZA MECHI
Mbali na rekodi za mabao, hatua ya makundi ilishuhudia mechi zilizogeuka ndani ya muda mfupi na kuonyesha namna ushindani ulivyokuwa mkali.
Argentina ilifanya mabadiliko makubwa dhidi ya Denmark baada ya kuwa nyuma kwa mabao 2-0. Giovanni Baroni alianza kurejesha matumaini kwa kufunga dakika ya 58, kabla ya Juan Cruz Policella kusawazisha dakika ya 62.
Alan Alcaraz alikamilisha mabadiliko hayo dakika ya 68 kwa bao lililoifanya Argentina kuongoza, ingawa Denmark ilirejea na kusawazisha dakika ya 78 na mchezo kuisha kwa sare ya mabao 3-3.
Chile nayo ilionyesha uwezo wa kupambana baada ya kutoka nyuma kwa mabao 2-0 na kuifunga Algeria 4-2. Timu hiyo ilihitaji dakika 14 pekee kufunga mabao matatu na kugeuza matokeo.
TANZANIA YAONDOKA NA HISTORIA
Kwa upande wa Tanzania, jina la Faraji Kayanda litaendelea kukumbukwa baada ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao la Serengeti Boys katika historia ya Kombe la Dunia la U-17 la wanaume.
Kayanda aliandika historia hiyo katika mchezo dhidi ya Costa Rica uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2, akifunga mabao mawili yaliyoiwezesha Tanzania kupata pointi moja katika mashindano hayo.
Pia Tanzania ilikuwa miongoni mwa mataifa matatu yaliyofunga bao katika ushiriki wao wa kwanza kwenye Kombe la Dunia la vijana chini ya miaka 17 la wanaume, pamoja na Msumbiji na Montenegro.
MSUMBIJI YATISHA MECHI YA KWANZA
Msumbiji nayo ilianza kwa kishindo katika historia yake ya mashindano hayo baada ya kuifunga Denmark mabao 4-0 katika mchezo wake wa kwanza.
Ushindi huo uliifanya kuwa sawa na Mali, ambayo iliifunga New Zealand katika mashindano ya Misri 1997, kwa kuwa timu mpya zilizofanikiwa kupata ushindi mkubwa zaidi katika hatua hiyo.
Katika tukio lingine la kipekee, Ecuador ilipata mabao mawili ya kujifunga katika mchezo dhidi ya Korea Kusini uliomalizika kwa ushindi wa Korea wa mabao 3-2.
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza tangu New Zealand ilipofaidika na mabao mawili ya kujifunga katika mchezo mmoja dhidi ya Qatar katika Kombe la Dunia la U-17 la mwaka 2017.