Polisi,Yanga keaho ni vita ya Pointi tatu Ushirika
Muktasari:
- Yanga inaingia kwenye mchezo huo ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 25 baada ya kucheza mechi 10, ikisaka ushindi utakaoiwezesha kupunguza pengo la pointi tano dhidi ya vinara Simba wenye pointi 30.
VITA ya pointi tatu inatarajiwa kupamba moto kesho Ijumaa, Novemba 20, wakati Polisi Tanzania itakapoikaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi, huku kila timu ikiwa na kiu ya kuhitaji ushindi.
Yanga inaingia kwenye mchezo huo ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 25 baada ya kucheza mechi 10, ikisaka ushindi utakaoiwezesha kupunguza pengo la pointi tano dhidi ya vinara Simba wenye pointi 30.
Kwa upande wa Polisi Tanzania, yenyewe ipo nafasi ya sita ikiwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi 11, hivyo ushindi wa nyumbani utakuwa muhimu katika kuongeza alama na kujiimarisha kwenye msimamo wa ligi.
Takwimu zinaonyesha Yanga imekuwa na mwenendo mzuri zaidi baada ya kushinda mechi nane, kutoka sare moja na kupoteza moja kati ya 10 ilizocheza, wakati Polisi imeshinda nne, sare tatu na kupoteza nne katika mechi 11.
Wananchi wanaingia kwenye pambano hilo wakiwa na morali baada ya kushinda michezo miwili mfululizo, kwanza wakiichapa Mashujaa FC mabao 2-1 Oktoba 27, kabla ya kuifunga Kagera Sugar mabao 4-0.
Ushindi huo umekuja katika kipindi cha mabadiliko ya benchi la ufundi, huku Kocha Fadlu Davids akiendelea kuingiza falsafa zake baada ya kujiunga na timu hiyo.
Hata hivyo, Polisi nayo imeonyesha kuwa haitakuwa mteja rahisi, ikirejea kwenye ushindi baada ya kuichapa Geita Gold bao 1-0 Novemba Mosi, kufuatia kupoteza kwa Namungo bao 1-0 Oktoba 29.
Kocha wa Polisi, Mbwana Makata, amesema anaiheshimu Yanga kutokana na ubora wa kikosi chake, lakini amepanga kutumia dakika za mwanzo kumchunguza Fadlu kabla ya kufanya mabadiliko ya kimkakati.
"Tumeshamuona akiwa na Simba. Hata sisi tutaingia kwa tahadhari, dakika tano, 10 au 20 tutaangalia ni kitu gani kipya amekileta ndani ya Yanga, kisha tunaweza kubadilika kulingana na hali ya mchezo," amesema Makata.
Kocha huyo amesema wachezaji wake wengi wako fiti isipokuwa majeruhi wawili au watatu, huku akisisitiza kuwa nidhamu ya kiufundi itakuwa silaha muhimu katika kuwadhibiti wapinzani wao.
Kwa upande wa Yanga, kocha wa mipira ya kutenga, Kagisho Dikgacoi, amesema kikosi kimejiandaa vizuri baada ya kuweka kambi Zanzibar na wachezaji kuitikia vyema mbinu mpya za Fadlu.
Dikgacoi amekiri kuwa Polisi ni timu ngumu, hasa kutokana na ushindi wake dhidi ya Geita Gold, lakini akasema lengo lao ni kupata pointi tatu ili kuendelea kuisakama Simba kileleni.
Amesema wachezaji wanafahamu umuhimu wa kushinda kila mchezo uliosalia badala ya kujishughulisha na mwenendo wa wapinzani wao.
Katika vita ya makipa, Christopher Nyakanda maarufu Masapta wa Polisi ametamba kuwa hana hofu ya kukabiliana na Yanga, akisema anataka kufanya vizuri zaidi ya siku zote.
Nyakanda amesema rekodi ya Yanga kupata wakati mgumu kwenye Uwanja wa Ushirika inawapa hamasa ya kupambana ili kuendeleza matokeo mazuri nyumbani.
"Ukifuata rekodi, kweli Yanga wanapata taabu sana katika Uwanja wa Ushirika. Sisi tunachukulia hilo kama hamasa ya kupambana ili tupate matokeo na kuendeleza rekodi iliyokuwepo," amesema.
Hata hivyo, kipa wa Yanga, Hussein Masalanga, amesema historia ya matokeo ya timu hiyo Ushirika haitawapa presha, akisisitiza kuwa wamejiandaa kukabiliana na mazingira yoyote.
Masalanga amesema licha ya mabadiliko ya benchi la ufundi, wachezaji wanaendelea kuzingatia malengo ya timu na wanaamini maandalizi waliyofanya yatawasaidia kupata matokeo.
"Uwanja wowote tunaokwenda ni mgumu kwa sababu sisi ni mabingwa watetezi. Tumejipanga kukutana na kila hali katika mazingira yoyote tunayopangiwa kucheza," alisema.
Rekodi ya Uwanja wa Ushirika Moshi
Mbali na msimamo wa ligi, historia ya timu hizo kwenye Uwanja wa Ushirika inaongeza ladha ya pambano hilo, baada ya kukutana mara ya mwisho kwenye uwanja huo Februari 18, 2020 na kutoka sare ya bao 1-1.
Katika mchezo huo, Yanga ilipata bao kupitia Tariq Seif Kiakala dakika ya 40, kabla ya Polisi kusawazisha kwa bao la kichwa lililofungwa na Sixtus Sabilo dakika ya 70.
Sasa, Yanga inahitaji kuvunja historia ya matokeo yasiyoridhisha kwenye uwanja huo ili kuendelea na mbio za ubingwa, wakati Polisi ikitaka kutumia nguvu ya nyumbani kuzuia Wananchi wasiondoke na pointi tatu.