Picco: Nilimchukia Chuji alipojiunga Simba
Muktasari:
- Picco, ambaye ni shabiki mkubwa wa Yanga, amesema alikuwa akimkubali Chuji tangu wakiwa Dodoma, walikokuwa wakicheza soka pamoja mitaani. Hata hivyo, uamuzi wa Chuji kujiunga na Simba ulimuumiza kutokana na ushindani wa jadi kati ya timu hizo mbili.
MSANII wa Bongo Fleva, Amani Habibu Mohamed, maarufu Picco, amefichua jinsi alivyomchukia aliyekuwa nyota wa Simba na Yanga, Athuman Idd ‘Chuji’, baada ya kujiunga na Simba, licha ya kuwa walikuwa wakifahamiana tangu walipokuwa wakicheza soka la mtaani.
Picco, ambaye ni shabiki mkubwa wa Yanga, amesema alikuwa akimkubali Chuji tangu wakiwa Dodoma, walikokuwa wakicheza soka pamoja mitaani. Hata hivyo, uamuzi wa Chuji kujiunga na Simba ulimuumiza kutokana na ushindani wa jadi kati ya timu hizo mbili.
“Nilipoona kwenye vyombo vya habari kwamba kaka yangu wa mtaani, Chuji, amejiunga na Simba, nilichukia sana siku hiyo. Kuna raha fulani unapomwona mshikaji wako akipiga hatua kubwa katika kipaji chake, lakini ushabiki wa Simba na Yanga ndio ulikuwa changamoto kwangu,” amesema Picco.
Amesema licha ya tofauti hiyo ya kiushabiki, aliendelea kumfuatilia Chuji baada ya kujiunga na Yanga, akihakikisha hapitwi na mechi zake.
“Baada ya kuhamia Yanga, nilikuwa natenga muda wa kumwangalia Chuji akicheza. Ilipotokea sijabahatika kuona mechi, nilihakikisha namwangalia kwenye marudio.
“Kitu kingine, nilikuwa naumia sana nikiona Chuji hajapangwa kwenye mechi, kwa sababu ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa. Simkubali kwa sababu tu alicheza Yanga, timu ninayoipenda,” amesema.
Kwa upande wake, Chuji amesema Picco alikuwa mdogo kwao, lakini walizoeana sana kwa kuwa walikuwa wakifuatana katika shughuli zao na kucheza soka la mtaani.
“Japokuwa tulimtangulia, tuliishi kama ndugu. Harakati za kutafuta maisha zilitutenganisha; yeye akachagua muziki, mimi nikachagua mpira wa miguu. Najua jinsi alivyokuwa akinikubali, hivyo nilijua kujiunga kwangu na Simba si jambo alilolipenda,” amesema Chuji.
Amemshauri Picco kuthamini nafasi aliyoipata katika muziki na kuzingatia ushauri wa watu wenye uzoefu ili aendelee kufanya vizuri katika tasnia hiyo.
“Ninachomshauri ni kuthamini nafasi aliyopata na kuzingatia ushauri wa waliomtangulia ili aendelee kusalia juu. Muziki anaweza kuufanya hata akiwa mzee, tofauti na soka ambalo lina muda wake.
“Ninapompigia simu huwa anafurahi, na namwona akifanya vizuri. Katika miaka yake 30 ya Bongo Fleva, kile kilichomkwamisha mwanzoni akiepuke,” amesema Chuji.