Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Soka la Wanawake Kilimanjaro kuanza ukurasa mpya Ligi Kuu

KILIMANJARO Pict

Muktasari:

  • Leo Jumatano, Kilimanjaro itashuhudia mchezo wa kihistoria wa Ligi Kuu ya Soka Wanawake Tanzania Bara, wakati Kilimanjaro Wonders Queens itakapovaana na Simba Queens kwenye Uwanja wa Ushirika uliopo Moshi, tangu mkoa huo uanzishwe mwaka 1963.

Baada ya miaka mingi ya Kilimanjaro kujijengea historia katika soka kupitia timu na wachezaji waliowahi kutamba hapa nchini, sasa macho yanaelekezwa kwa Kilimanjaro Wonders Queens, inayotarajiwa kufungua ukurasa mpya kwa mkoa huo itakapomenyana na Simba Queens, leo Jumatano Oktoba 28, 2026 katika Ligi Kuu ya Soka Wanawake Tanzania Bara.

Pambano hilo litakalopigwa kwenye Uwanja wa Ushirika uliopo Moshi, ni zaidi ya vita ya pointi tatu kwa wenyeji, kwani ni fursa ya kuutambulisha mkoa huo katika jukwaa la juu la soka la wanawake hapa nchini, huku wakikabiliana na mabingwa watetezi wanaotaka kuanza msimu kwa ushindi.

Kilimanjaro Wonders Queens inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kiu ya kuandika historia, huku Simba Queens ikitaka kuendeleza ubabe wake baada ya kutwaa ubingwa msimu uliopita bila kupoteza mchezo, ikitoka sare tatu pekee.

Mkurugenzi wa Kilimanjaro Wonders, Laurent Kinabo, amesema wamejiandaa vizuri kwa mchezo huo ambao utakuwa wa kwanza kwa timu hiyo kushiriki Ligi Kuu ya Wanawake, akieleza kuwa maandalizi yamekuwa yakifanyika tangu wachezaji walipoingia kambini.

“Tunajua ni mchezo ambao unaenda kututambulisha sisi na kuwajumuisha watu wote wadau wa Mkoa wa Kilimanjaro kuja kuona kwamba Kilimanjaro Wonders Queens wako uwanjani kupambana na Simba Queens,” amesema Kinabo.

Amesema uongozi umekamilisha mahitaji muhimu ya timu na unaamini wachezaji watatoa ushindani mkubwa, huku akiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kuipa sapoti.

Kinabo amesema lengo lao ni kuondoka na pointi zote tatu na kuweka historia kwa kuifunga Simba Queens, ambayo ni miongoni mwa timu zenye uzoefu mkubwa katika soka la wanawake Tanzania.

Kocha wa Kilimanjaro Wonders Queens, Wilbad Pacho, amesema kikosi chake kimejiandaa vizuri na kina morali ya kutosha, licha ya kuwa na majeruhi wachache, akisisitiza kuwa lengo lao ni kuanza ligi kwa ushindi.

Pacho amesema wanaiheshimu Simba Queens, lakini wameichambua baada ya kuitazama katika Ngao ya Jamii ili kubaini mbinu za kukabiliana nayo kwani hawajawahi kukutana.

Naye mshambuliaji wa timu hiyo, Ladosho Shiligenda, amesema wachezaji wameelewa maelekezo ya benchi la ufundi na wako tayari kupambana, akisisitiza kuwa wanaelewana vizuri ndani ya kikosi chao.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amewataka wachezaji wa Kilimanjaro Wonders Queens kutotishwa na majina ya Simba Queens na Yanga Princess, akisema wanapaswa kuingia uwanjani kwa kujiamini na kuonyesha ubora wao.

“Ninataka niwaambie wachezaji wetu wa Kilimanjaro Queens kwamba wasitishike na timu hizo, sijui Yanga Queens, Simba Queens. Haya ni majina, lakini inawezekana vijana wetu wakawa na ubora zaidi kuliko hao wanaokuja kucheza,” amesema Babu.

Babu amewataka wakazi wa Kilimanjaro kujitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Ushirika kuishangilia timu hiyo, akiahidi kuwa miongoni mwa mashabiki watakaoiunga mkono.

Amesema kucheza nyumbani ni fursa kwa kilimanjaro Wonders Queens, hivyo wananchi wanapaswa kuwa nyuma ya timu hiyo ili kuwapa wachezaji hamasa ya kupambana na kutafuta ushindi.

Kwa upande wa Simba Queens, kocha wa timu hiyo, Musa Mgosi, amesema wamejipanga kuendeleza walipoishia msimu uliopita kwa kushinda kila mchezo katika kampeni ya kutetea ubingwa wao.

Mgosi amesema licha ya kutwaa taji bila kupoteza mchezo msimu uliopita, sare tatu walizopata zimewafanya kuweka mkazo zaidi katika kutafuta pointi tatu kila wanaposhuka dimbani.

“Kauli yetu ni kwamba tunaenda kuanza pale tulipoishia. Msimu uliopita tulikuwa mabingwa, kwa hiyo tuna malengo ya msimu huu na tunahitaji kupata pointi tatu kwenye kila mechi,” amesema Mgosi.

Amesema wanatambua kuwa ligi itakuwa ngumu na yenye ushindani, lakini wamejipanga kuichukulia kila mechi kama fainali ili kufanikisha azma ya kutetea taji.

“Tunaamini ligi itakuwa ngumu na yenye ushindani, lakini tumejiandaa kwa sababu kila mechi ni fainali.Tunahitaji pointi tatu ili kusonga mbele,” amesema kocha huyo.

Kilimanjaro ina historia ya muda mrefu katika michezo, hasa soka la wanaume, kupitia timu zilizowahi kutamba kama TPC ya Kilimanjaro, Nyerere, Tembo, Panone, Mabo Stars, Pasua Rangers na Kibo Paper.

Hata hivyo, wadau wa soka wamekuwa wakieleza namna kupungua kwa viwanda na udhamini kulivyoathiri maendeleo ya mchezo huo mkoani humo.
 
Viwanda vilikuwa na mchango katika kutoa ajira kwa wachezaji, kugharamia timu na kusaidia miundombinu ya michezo.

Mkoa wa Kilimanjaro ulianzishwa mwaka 1963 kupitia Tangazo la Serikali Na. 450 la mwaka huo.

Sasa, kuibuka kwa Wonders Queens katika Ligi Kuu ya Wanawake kunatoa nafasi ya kupanua historia hiyo na kuongeza ushiriki wa wanawake katika soka la ushindani.

Pambano la leo linatarajiwa kuwa kipimo cha kwanza kwa Kilimanjaro Wonders Queens katika ligi hiyo, huku Simba Queens ikilenga kuanza kampeni yake kwa ushindi.

Kwa wenyeji, matokeo mazuri yatakuwa mwanzo wa safari yenye matarajio ya kuipa Kilimanjaro nafasi mpya katika ramani ya soka la wanawake nchini.