Clara amwachia msala Opah Saudia
Muktasari:
- Uhamisho huo unamfanya Opah kuwa miongoni mwa wachezaji wa Tanzania wanaocheza Ligi Kuu ya Saudi Arabia, akifuata nyayo za Clara Luvanga aliyewahi kuitumikia Al Nassr, Enekia Lunyamila aliyepita Eastern Flames na Julitha Singano wa Al Nassr.
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania na nahodha wa Twiga Stars, Opah Clement ameendelea kuandika historia katika soka la wanawake baada ya kujiunga na Al Ula SC inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Saudi Arabia, akitokea SD Eibar ya Hispania.
Uhamisho huo unamfanya Opah kuwa miongoni mwa wachezaji wa Tanzania wanaocheza Ligi Kuu ya Saudi Arabia, akifuata nyayo za Clara Luvanga aliyewahi kuitumikia Al Nassr, Enekia Lunyamila aliyepita Eastern Flames na Julitha Singano wa Al Nassr.
Kinachofanya safari ya Opah iwe ya kipekee zaidi ni historia yake ya kucheza katika ligi tano tofauti ndani na nje ya Tanzania.
Kabla ya kutua Saudi Arabia, mshambuliaji huyo amewahi kucheza Simba Queens ya Tanzania, Kayseri Kadın FK na Beşiktaş za Uturuki, Henan Jianye ya China, FC Juárez ya Mexico na SD Eibar ya Hispania.
Safari hiyo pia inamfanya Opah kuwa miongoni mwa wachezaji wa Tanzania waliopata nafasi ya kucheza katika mazingira tofauti ya soka duniani, akipita katika ligi zenye ushindani na mifumo tofauti ya uendeshaji.
Kutua Saudi Arabia kunakuwa sura nyingine katika safari yake, baada ya kuzunguka Uturuki, China, Mexico na Hispania kabla ya sasa kuhamia Mashariki ya Kati.
Kutua Saudi Arabia pia kunaweza kuwa deni kwa Opah, kutokana na ukweli Tanzania tayari imekuwa na mshambuliaji mwingine aliyeacha alama kubwa kwenye ligi hiyo.
Clara alikuwa mmoja wa wachezaji waliotegemewa zaidi kwenye safu ya ushambuliaji ya Al Nassr, akitengeneza rekodi iliyoweka kiwango ambacho Opah sasa anaingia kwenye ligi hiyo akiwa na jukumu la kujaribu kukifikia au hata kukivuka.
Clara alianza msimu wake wa kwanza 2023/24 akifunga mabao 11 na asisti saba, msimu wa 2024/25 alifunga mabao 21 na kutoa asisti saba. Msimu wa 2025/26 akaibuka mfungaji bora akiweka kambani mabao 24, rekodi iliyomfanya aendelee kuwa miongoni mwa washambuliaji waliokuwa na ushawishi mkubwa katika ligi hiyo.
Sasa swali ni je, Opah ataifikia rekodi ya Clara ambaye ametimkia Washington Spirit ya Marekani au atakwenda mbali zaidi. Huo ndiyo mtihani unaomsubiri mshambuliaji huyo .