Nyota JKT Tanzania aweka mikakati mipya
Muktasari:
- Magata ana rekodi ya kupandisha timu mbili kwenda Ligi Kuu kutokea Championship, akianza na Mbeya Kwanza msimu wa 2021-2022, kisha Mtibwa Sugar msimu wa 2024-2025, aliyoifungia mabao tisa na asisti 21, akihusika na mabao 30, kati ya 58.
KIUNGO mshambuliaji wa JKT Tanzania, Fredrick Magata, amesema ushindani wa nafasi katika kikosi hicho cha maafande ni tofauti na msimu uliopita wa 2025-2026, kutokana na aina ya wachezaji wengi na wazuri aliokutana nao kwenye timu hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Magata amesema licha ya yeye mwenyewe kuonyesha kiwango bora msimu uliopita, ila kujiunga na JKT Tanzania itakuwa ni tofauti, kwa sababu aina ya wachezaji alionao ni wazuri na wenye ushindani zaidi kikosini humo.
"Mtibwa Sugar nilikuwa napata zaidi nafasi ya kucheza mara kwa mara kikosi cha kwanza, hali ni tofauti na JKT kwa sababu kila mtu anajituma ili ashawishi benchi la ufundi liweze kumtumia, kwangu inanipa morali ya kupambana," amesema Magata.
Aidha, Magata amesema licha ya ushindani uliopo kikosini, ila atahakikisha kila anapozidi kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara aonyeshe kiwango kizuri, kwa ajili ya kuisaidia timu hiyo ifanye vizuri katika mashindano mbalimbali msimu huu.
Nyota huyo alijiunga na kikosi hicho cha maafande wa JKT Tanzania, Julai 15, 2026, baada ya kuachana na Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro, iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara hadi Ligi ya Championship, kutokana na mwenendo usioridhisha.
Msimu wa 2025-2026, kiungo huyo alichangia mabao saba ya Ligi Kuu Bara kati ya 25, yaliyofungwa na kikosi hicho kizima, baada ya kufunga matano akiwa ndiye aliyeongoza kikosini humo na kuchangia pia mengine mawili kwa maana ya kutoa asisti.
Magata ana rekodi ya kupandisha timu mbili kwenda Ligi Kuu kutokea Championship, akianza na Mbeya Kwanza msimu wa 2021-2022, kisha Mtibwa Sugar msimu wa 2024-2025, aliyoifungia mabao tisa na asisti 21, akihusika na mabao 30, kati ya 58.