Mayanga anavyoipambania heshima Mbeya City
Muktasari:
- Mbeya City inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya, ilipanda Ligi Kuu msimu wa 2013/14 huku ikiweka rekodi na historia ya kumaliza nafasi ya tatu kwa mara ya kwanza ikicheza ligi hiyo.
MBEYA; BAADA kupitia kipindi kigumu, Mbeya City imeanza kurejesha taratibu heshima yake kufuatia mwanzo mzuri walionao kwenye Ligi Kuu, huku nyuma yake akiwepo Kocha Mkuu, Salum Mayanga anavyoisuka timu hiyo.
Mbeya City inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya, ilipanda Ligi Kuu msimu wa 2013/14 huku ikiweka rekodi na historia ya kumaliza nafasi ya tatu kwa mara ya kwanza ikicheza ligi hiyo. Hata hivyo, haikuishia hapo kwani msimu uliofuata ilimaliza nafasi ya nne na kuwa moja ya timu tishio na kuwavuta mashabiki wengi walioiona kama mbadala wa soka la mageuzi nchini.
Kwa takribani misimu 12 timu hiyo ikiwa chini ya aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu, Emanuel Kimbe, ilijikuta ikiwa chaguo la mashabiki wengi wa ndani na nje ya jiji la Mbeya kutokana na soka la ushindani.
Katika msimu wa 2022/23 historia iliandikwa kwa timu hiyo kushuka daraja kupitia play off ilipofungwa jumla ya mabao 3-1 dhidi ya Mashujaa FC iliyokuwa Championship na kuonekana kupoteza mvuto.
Baadaye timu hiyo ikiwa chini ya aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu, Ally Nnunduma iliweza kurejea Ligi Kuu ikiwa na kiwango bora japokuwa kigogo huyo alihamishwa kituo cha kazi na kupandishwa daraja.
Kuondoka kwa kigogo huyo ilionekana kuitikisa timu hiyo kwa kutokuwa na matokeo mazuri kabla ya uongozi kumkabidhi mikoba, John Kilua kuziba nafasi ya Nnunduma, ambapo City iliweza kunusurika kushuka daraja kupitia mchujo (play off).
Matokeo ya jumla katika misimu mitatu mfululizo yalionekana kuwagawa sana mashabiki huku wamiliki wakionekana kuhaha kuona namna ya kurejesha matumaini kwa mashabiki hali ambayo haikuwapa utulivu.
AINUSURU DAKIKA ZA JIONI
Mayanga alianza kuonesha uwezo wake tangu msimu uliopita baada ya kuiongoza kuanzia mechi 11 za mwisho akichukua nafasi ya aliyekuwapo, Mecky Maxime, ambaye naye alirithi mikoba ya Malale Hamsini.
Katika mechi 11 alizoongoza Mayanga alishinda tatu, sare nne na kupoteza nne na kumaliza nafasi ya 14 kwa pointi 30 na kuangukia kwenye mchujo ‘play off’, ambapo alifanikiwa kuibakiza timu salama.
Hata hivyo kuinusuru timu hiyo inakuwa mwendelezo wa historia ya kocha huyo kutoshusha timu akilinda na kuendeleza heshima na rekodi yake kwenye soka nchini na kazi yake hiyo.
MUUNGANIKO, MORALI
Tangu alipotambulishwa kikosini kwa mara ya kwanza msimu wa 2025/26, wakati ikiwa Championship, Mayanga alionyesha kuweka muunganiko kikosini na mwelekeo wa kuirejesha Ligi Kuu.
Hata hivyo zikiwa zimebaki mechi sita pekee, alipata ofa kwa Mashujaa iliyokuwa Ligi Kuu na kuaga nafasi yake ikibebwa na Malale Hamsini aliyeipandisha tena daraja, japokuwa kocha huyo hakuwa na safari ndefu.
Mayanga alirudishwa tena kikosini kubeba zigo lililokuwa limewaelemea makocha wawili, Malale na Maxime, ambapo alitengeneza morali, hamasa na muunganiko kwa wachezaji.
Kupitia falsafa yake ya soka la ushindani, ilimuwezesha kocha huyo kuwa na mafanikio akiinusuru timu hiyo na sasa inaendelea kukiwasha Ligi Kuu na moto wake kila mmoja ameona kwenye mechi sita ilizocheza.
HISTORIA YAKE
Pamoja na ukongwe wake, Mayanga rekodi zake zinashtua kwani licha ya mafanikio aliyopata au kuweka kwenye soka, hajawahi kupandisha wala kushusha timu kwenye Ligi Kuu.
Nyota huyo wa zamani wa Taifa Stars, amefundisha timu nyingi ikiwamo Mtibwa Sugar, Mbao FC, Tanzania Prisons, Mashujaa na Mbeya City, ambazo amefanya kwa mafanikio.
Licha ya ukongwe wake kwenye soka tangu aanze kufundisha ikiwamo Taifa Stars anajivunia kunusuru timu kutoshuka daraja, akifanya hivyo kwa Mtibwa Sugar msimu miwili tofauti, Mbao FC na Mbeya City msimu uliopita.
MOTO MSIMU HUU
Ukiachana na vigogo wa soka nchini, Yanga, Simba, ambao hawajapoteza mchezo wowote Ligi Kuu, Mbeya City ni miongoni mwa timu zilizoanza kwa moto mkali msimu huu na kuwa nafasi nzuri kwenye msimamo.
Katika mechi sita alizoongoza Mayanga, ameshinda tatu na sare moja akipoteza miwili na kuwa nafasi ya sita kwa pointi 10 na kesho Ijumaa watakuwa kibaruani kuwakaribisha Kagera Sugar, kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya.
Pamoja na matokeo mazuri waliyoanza nayo, timu hiyo imekuwa na soka la ushindani kwa mchezaji mmoja mmoja wakiwa na ari, morali na nguvu katika kuonesha ushindani uwanjani.
Tangu kuanza kwa msimu, wachezaji wameonesha kumuelewa na kuendana na falasafa ya kocha huyo, kila mmoja akipambana kuanzia mazoezini hadi mechi za ligi kuipambania timu.
MSIKIE MWENYEWE
Mayanga anasema kuwa licha ya mwanzo mzuri, lakini bado ni mapema japokuwa anahitaji kuona mwendelezo mzuri wa kila mchezaji kupambana na kuhakikisha wanaipa mafanikio timu hiyo.
Kuhusu muunganiko, morali na hamasa uwanjani, Mayanga amesema kuwa anaridhishwa na mwenendo wa nyota wake, akieleza kuwa kila siku wanaonesha kitu kwa kila mmoja kuwa na kiu ya mafanikio.
“Bado ni mapema lakini kwa mwanzo tulionao unatia matumaini, kimsingi ni kuendelea kulinda matokeo haya kuhakikisha hatupati tena presha kama ilivyokuwapo msimu uliopita” anasema Mayanga.
Kocha huyo anaongeza kuwa ushirikiano na sapoti iliyopo kuanzia ndani na nje ya uwanja ni moja ya sababu kubwa inayowapa nguvu kuendelea kupambana akieleza kuwa lolote linawezekana katika vita ya nafasi nne za juu.
Mayanga anakiri kwamba ugumu na ushindani wa ligi, akiwataka nyota wake kutobweteka wala kukata tamaa badala yake wakaze ili kufikia malengo kwakuwa mpira ndio kazi yao inayowapa maisha.
“Ligi ni ngumu muda wote, kila timu inahitaji matokeo mazuri bila kujali nyumbani wala ugenini, lazima wachezaji wajitume na watambue mpira ndio kazi yao, wasikate tamaa wala kubweteka,” anasema kocha huyo.