Ngushi: Ligi ya moto sana
Muktasari:
- Ngushi amesema tofauti ndogo ya pointi katika msimamo wa ligi inaonyesha namna timu zilivyojipanga kupambana msimu huu, huku kila mmoja akiwa na nafasi ya kupata matwokeo mazuri anapocheza kwa kiwango kinachotakiwa.
MSHAMBULIAJI wa Mashujaa, Crispin Ngushi amesema ushindani wa Ligi Kuu Bara msimu huu umekuwa mkubwa kutokana na timu nyingi kuimarika na kujiandaa vizuri, hali inayofanya mbio za kuwania nafasi za juu kuwa ngumu na kutotabirika kirahisi.
Ngushi amesema tofauti ndogo ya pointi katika msimamo wa ligi inaonyesha namna timu zilivyojipanga kupambana msimu huu, huku kila mmoja akiwa na nafasi ya kupata matwokeo mazuri anapocheza kwa kiwango kinachotakiwa.
“Ligi ya moto sana na ngumu na imekuwa bora sana msimu huu. Kila timu ina kiwango bora na wachezaji wake. Hata ukiangalia msimamo, timu hazijapishana pointi, maana timu zimekuwa imara na zimejipanga msimu huu,” amesema Ngushi.
Ameongeza ushindani huo ni ishara nzuri kwa soka la Tanzania kwa sababu unawapa wachezaji nafasi ya kuonyesha uwezo wao, huku timu zikilazimika kuongeza juhudi ili kupata matokeo. Kwa upande wake, mazingira hayo yanampa changamoto ya kuendelea kuboresha kiwango chake na kuongeza mchango wake kwa Mashujaa.
Mbali na kuzungumzia ushindani wa ligi, Ngushi amewapongeza wachezaji wa Tanzania kwa namna wanavyojituma, akimtaja Anuary Jabir kuwa miongoni mwa washambuliaji wanaofanya kazi nzuri akitoa rai kwa mashabiki kuunga mkono juhudi zake ili aendelee kufanya vizuri.
“Kwanza napenda kuwapongeza wachezaji wa Tanzania, wanapambana. Anuary Jabir anafanya kazi nzuri na tunamuombea, na sisi tulio nyuma tuendelee kusukuma gurudumu. Msimu huu inaweza kutokea mshambuliaji kuchukua kiatu, inaweza ikatokea,” amesema.
Hata hivyo, amesema uwezekano wa mshambuliaji wa Tanzania kutwaa kiatu cha ufungaji upo, ingawa mafanikio hayo yatategemea juhudi na mwendelezo wa kiwango.