Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mashujaa FC yazindukia Kigoma, Kagera Sugar hali tete

MASHUJAA

Muktasari:

  • Kagera Sugar ilianza kupata bao dakika ya 38 kupitia Mudathir Said, aliyejiunga na klabu hiyo Agosti 8, 2026 akitokea Mashujaa FC.

BAADA ya kupoteza mechi mbili mfululizo, Mashujaa FC imezinduka na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Kagera Sugar ilianza kupata bao dakika ya 38 kupitia Mudathir Said, aliyejiunga na klabu hiyo Agosti 8, 2026 akitokea Mashujaa FC.

Mudathir alipokea mpira nje ya eneo la 18 na kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa Mashujaa, Adam Oseja, na kuiwezesha Kagera Sugar kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.

MASHU 01

Kipindi cha pili Mashujaa ilirejea ikiwa na kasi na kusawazisha dakika ya 65 kupitia mshambuliaji Mishamo Michael, aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Crispin Ngushi.

Mishamo alifunga baada ya Oseja kushindwa kuudhibiti mpira wakati akijaribu kuuokoa, hivyo kumpa mshambuliaji huyo nafasi ya kurejesha matumaini ya Mashujaa.

Dakika nane baadaye, beki wa kati Haroun Lyawatwa akaikamilishia Mashujaa ushindi muhimu nyumbani kwa kufunga bao la pili kwa kichwa, akimalizia mpira wa kona uliopigwa na Mishamo Michael.

Kagera ilijaribu kusaka bao la kusawazisha, lakini Mashujaa ililinda vizuri uongozi wake hadi dakika za mwisho.

Mashujaa ilipata nafasi ya kuongeza bao la tatu baada ya kupewa penalti kufuatia Mishamo Michael kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari.

Hata hivyo, Salum Kihimbwa alishindwa kutumia nafasi hiyo baada ya penalti yake ya dakika ya 90+3 kupanguliwa na kipa Adam Oseja.

Penalti hiyo ilitokana na kiungo wa Kagera Sugar, Yassin Salehe, kufanya madhambi ndani ya eneo la 18, lakini Kihimbwa akashindwa kuifungia timu yake bao la tatu.

MASHU 02

Ushindi huo unaifanya Mashujaa kufikisha pointi sita, ikiwa imeshinda mechi mbili na kupoteza mbili katika michezo minne, na kukaa nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Mashujaa ilianza msimu kwa kuifunga Coastal Union 1-0 Agosti 15, kabla ya kupoteza kwa matokeo kama hayo dhidi ya Fountain Gate Agosti 18 na kuchapwa 2-1 na Mbeya City Agosti 23.


MASHU 03

KAGERA YAZIDI KUPOROMOKA

Kwa upande mwingine, Kagera Sugar imeendelea kupitia wakati mgumu tangu kurejea Ligi Kuu Bara msimu huu.

Katika mechi nne ilizocheza msimu huu, Kagera imepoteza tatu na kutoka sare moja, ikiwa na pointi moja pekee na kukaa mkiani mwa msimamo.

Ilianza msimu kwa kupoteza 2-0 dhidi ya Simba Agosti 16, ikatoka sare ya 1-1 na Singida Black Stars Agosti 19, kabla ya kuchapwa 6-2 na Geita Gold Agosti 22 na leo kuangushwa tena 2-1 na Mashujaa.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana katika Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, zilitoka sare ya 1-1. Mashujaa ilifunga kwa penalti kupitia Mohamed Mussa dakika ya 87, huku Kagera ikipata bao lake kupitia Tariq Seif dakika ya 30.

Matokeo ya leo yanaifanya Mashujaa kusogea hadi pointi sita, huku Kagera Sugar ikiendelea kushikilia nafasi ya mwisho ikiwa na pointi moja baada ya sare moja na vipigo vitatu.