Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ngorongoro Heroes yavuliwa ubingwa CECAFA

Muktasari:

  • Ngorongoro Heroes, iliyokuwa bingwa mtetezi baada ya kutwaa ubingwa mwaka 2024, ilianza kufungwa dakika ya 93 na Omer Hamdi, kabla ya Abdulnasir Abdallah ‘Casemiro’ kusawazisha dakika ya 113 akimalizia pasi ya Farid Mzalendo. Wachezaji hao wote waliingia wakitokea benchi.

TIMU ya Taifa ya vijana ya Tanzania chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, imepoteza fainali ya michuano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa penalti 4-3 baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Sudan, mchezo uliopigwa leo Alhamisi Septemba 24, 2026 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Ngorongoro Heroes, iliyokuwa bingwa mtetezi baada ya kutwaa ubingwa mwaka 2024, ilianza kufungwa dakika ya 93 na Omer Hamdi, kabla ya Abdulnasir Abdallah ‘Casemiro’ kusawazisha dakika ya 113 akimalizia pasi ya Farid Mzalendo. Wachezaji hao wote waliingia wakitokea benchi.

Tanzania na Sudan, ambazo tayari zilikuwa zimefuzu Fainali za AFCON U-20 zitakazofanyika Ghana mwaka 2027 baada ya kushinda mechi zao za nusu fainali, ziliingia Uwanja wa Uhuru zikiwa na lengo la kumaliza kampeni kwa kutwaa ubingwa wa CECAFA.

Tanzania iliingia fainali ikiwa imeshinda mechi zake zote tatu bila kuruhusu bao, huku Sudan ikiwa imefunga mabao sita katika michezo yake ya mashindano hayo.

Katika mchezo huo, kila upande ulionekana kuwa makini zaidi kutofanya makosa ambayo yangeipa timu pinzani nafasi ya kushambulia. Kocha wa Tanzania, Mario Rivera Campesino, na mwenzake wa Sudan, Salaheldin Ahmed, waliweka mkazo katika kulinda maeneo muhimu na kuzuia mipango ya wapinzani wao kabla ya kuongeza nguvu katika mashambulizi.

Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania U20 Ngorongoro Heroes vkilichoanza kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Sudan.

Tanzania, iliyokuwa imefunga mabao tisa katika mechi tatu zilizopita, haikupata nafasi nyingi za kufunga kama ilivyokuwa katika michezo dhidi ya Rwanda, Ethiopia na Burundi.

Sudan nayo, ambayo ilionyesha uwezo wa kubadilisha mchezo katika ushindi wake wa mabao 3-2 dhidi ya Uganda, ilikutana na Tanzania iliyokuwa makini katika kuzuia mashambulizi.

Hali hiyo ilifanya eneo la kiungo kuwa sehemu muhimu ya mchezo, huku timu zote zikijaribu kutawala mchezo bila kujifungua. Kila upande ulipofanikiwa kuvuka mstari wa kiungo wa mpinzani, safu ya ulinzi ilifanya kazi ya kuzima mashambulizi kabla hayajawa hatari, jambo lililofanya mchezo mwingi uchezwe kwa tahadhari huku kila timu ikisubiri kosa la mpinzani.

Kadiri dakika zilivyokuwa zikisonga, badala ya kuona timu zikifunguka na kushambulia kwa nguvu, mchezo uliendelea kuwa wa kusubiri. Makocha waliendelea kufanya marekebisho ya kiufundi huku kila mmoja akijaribu kumsoma mwenzake na kucheza kwa tahadhari hadi mwamuzi alipomaliza dakika 90 kwa matokeo ya 0-0.

Suluhu hiyo iliifanya fainali kuwa tofauti na mechi mbili za nusu fainali zilizokuwa na mabao mengi, ambapo Tanzania iliifunga Burundi 2-0 na Sudan ikaichapa Uganda 3-2.

Tanzania na Sudan tayari zilikuwa zimehakikisha nafasi za kushiriki AFCON U-20 mwaka 2027 nchini Ghana, hivyo fainali hiyo ilikuwa ni nafasi ya kusaka ubingwa wa CECAFA baada ya tiketi ya AFCON kuwa tayari mikononi mwao.

Kikosi cha timu ya Taifa ya Sudan U20 vkilichoanza kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Tanzania (Ngorongoro Heroes).

UGANDA NAFASI YA TATU

Katika mchezo mwingine wa kuwania nafasi ya tatu, Uganda iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burundi na kutwaa medali ya shaba katika michuano hiyo.

Uganda ilianza kwa kasi na kuonekana kuwa na kiu zaidi ya ushindi, ambapo Derrick Ssozi aliipa timu hiyo bao la kwanza dakika ya 22 baada ya kumalizia pasi ya chini iliyotolewa na Elvis Opakrwoth ndani ya eneo la hatari.

Burundi ilijaribu kusawazisha, lakini safu ya ulinzi ya Uganda pamoja na kipa Adrian Isabirye waliendelea kuzuia mashambulizi hayo. Uganda nayo ilipata nafasi kadhaa za kuongeza bao kabla ya mapumziko, lakini haikuzitumia.

Kyakuwa alifunga bao la pili dakika za mwisho baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Steven Oyirwoth, hivyo kuifungia Uganda ushindi wa mabao 2-0 na kuhakikisha inamaliza mashindano ikiwa nafasi ya tatu.