Kamungo kuivaa Nigeria, mechi yake ya kwanza Taifa Stars
Muktasari:
- Nyota huyo anatarajiwa kuongeza nguvu katika kikosi cha Stars ambacho kiliambulia kichapo cha mabao 3-1 katika mechi ya kwanza iliyopigwa Nigeria, Ijumaa, Novemba 13, 2026.
Mshambuliaji wa FC Dallas ya Marekani, Bernard Kamungo, anategemewa kuwa sehemu ya kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ambacho leo Jumanne, Novemba 17, 2026 kitashuka dimbani kuvaana na Nigeria katika mechi ya marudiano ya kundi L yakuwania kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).
Nyota huyo anatarajiwa kuongeza nguvu katika kikosi cha Stars ambacho kiliambulia kichapo cha mabao 3-1 katika mechi ya kwanza iliyopigwa Nigeria, Ijumaa, Novemba 13, 2026.
Kamungo mwenye umri wa miaka 24 amekuwa akifuatiliwa kwa karibu tangu alipoitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha Taifa Stars, lakini mazingira yasiyoepukika yalimzuia kucheza katika michezo miwili iliyopita dhidi ya Guinea Bissau na Madagascar.
Hata hivyo, baada ya kujiunga na kikosi na kushiriki mazoezi visiwani Zanzibar, Kamungo sasa yupo kwenye nafasi ya kuitumikia Stars huku kocha mkuu Miguel Gamondi akiwa na chaguo jingine katika safu ya ushambuliaji wakati Tanzania ikitafuta matokeo mazuri baada ya kupoteza mabao 3-1 katika mchezo wa kwanza.
Ujio wake unaongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ya Stars, huku akiwa na uzoefu wa kucheza soka la kulipwa nchini Marekani.
Taifa Stars itashuka katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar leo saa 10:00 jioni, leo Jumanne, Novemba 17, 2026, ikisaka ushindi wake wa kwanza katika kundi L.
Ingawa Tanzania tayari imepata tiketi ya AFCON 2027 kwa kuwa ni mwenyeji mwenza wa mashindano hayo, michezo hiyo bado ni muhimu katika maandalizi ya kikosi kuelekea fainali hizo.
Kamungo, ambaye alizaliwa Kasulu, Kigoma na baadaye kuhamia Marekani akiwa na umri wa miaka 14, ujio wake kambini unaashiria mwanzo wa ukurasa mpya katika soka lake la kimataifa akiwa na Taifa Stars.
Nyota huyo aliwahi kuitwa Taifa Stars mwaka 2023, lakini hakufanikiwa kujiunga na kikosi hicho kutokana na tatizo la hati ya kusafiria, jambo lililomzuia kusafiri na kuungana na timu kwa wakati.
Alikuwa ameitwa kwa ajili ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Niger katika mbio za kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) zilizofanyika Morocco.