Ngorongoro Heroes yatawala kikosi Bora CECAFA U-20
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), baada ya kumalizika kwa mashindano hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 15, 2026 na kuhitimishwa Septemba 24, 2026, Ngorongoro Heroes imetoa wachezaji watano ikiwa ni idadi kubwa kuliko taifa lolote lililoshiriki. Sudan inafuatia ikiwa na wanne, huku Burundi na Uganda zikiwa na mmoja.
TIMU ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, imetawala katika Kikosi Bora cha mashindano ya kufuzu AFCON U-20 kwa ukanda wa CECAFA.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), baada ya kumalizika kwa mashindano hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 15, 2026 na kuhitimishwa Septemba 24, 2026, Ngorongoro Heroes imetoa wachezaji watano ikiwa ni idadi kubwa kuliko taifa lolote lililoshiriki. Sudan inafuatia ikiwa na wanne, huku Burundi na Uganda zikiwa na mmoja.
Wachezaji watano wa Ngorongoro Heroes katika kikosi hicho ni kipa Shabani Bakari, mabeki wa kati Evastus Lukanima na Abubakar Nizar Othman 'Ninju'. Eneo la kiungo yupo Bashir Salum Kibaila na Juma Abushiri 'Chuga Boy'.
Kikosi hicho kilichowekwa katika mfumo wa 4-3-3, kipo hivi; kipa Shabani Bakari (Tanzania); Mabeki: Samaan Amin Koda (Sudan), Osama Amen Abdalla (Sudan), Evastus Lukanima (Tanzania) na Abubakar Nizar Othman (Tanzania).
Viungo watatu wanaocheza kati ni Rudwan Yahya Mohamed (Sudan) akiwa kiungo wa chini, juu yake wapo Isima Magala (Uganda) na Bashir Salum Kibaila (Tanzania).
Kule juu kwenye ushambuliaji, Mazin Fadul Albahli wa Sudan anatokea upande wa kushoto, wakati Juma Abushiri kutoka Tanzania akiwa upande wa kulia, huku Amini Nshimirimana wa Burundi akisimama mshambuliaji wa mwisho. Kumbuka mshambuliaji huyo ameacha alama katika michuano hiyo baada ya kufunga mabao manne katika michezo miwili ya hatua ya makundi akiwa ndiye mfungaji bora.
Ngorongoro Heroes ilifanya vizuri katika mashindano hayo sambamba na Sudan ambazo zilitinga fainali na kujikatia tiketi ya kushiriki Fainali za AFCON U-20 mwakani nchini Ghana.
Hata hivyo, Ngorongoro Heroes ilivuliwa ubingwa wa CECAFA U-20 kufuatia kupoteza fainali kwa penalti 4-3 dhidi ya Sudan baada ya mechi hiyo kuchezwa kwa dakika 120 matokeo yakiwa sare ya 1-1.