Ndoa ya Alikiba, bado utata mtupu
KAMA ni umbea ndio kwanza umeanza kunoga katika sakata la mwimbaji wa muziki wa kizazi kipya nchini, Ali Kiba kuachana na mke wake Amina kabla ya saa chache kukanusha hadharani.
Kwa zaidi ya miezi miwili, umbea wa kuacha kwa Ali Kiba na mke wake uliteka hisia za mashabiki mitandaoni, wakihoji bila kuwa na ushahidi wa moja kwa moja.
MCL Digital leo Septemba 20, 2019 ilifunga safari hadi nyumbani kwa Ali Kiba Tabata Segerea, jijini Dar es Salaam ili kujua ukweli ni upi kuhusu sakata hilo lakini haikuwa bahati baada ya kuelezwa ametoka.
Hata hivyo, Mwandishi wa MCl Digital hakutaka kuondoka mtupu, aliamua kupiga soga na majirani wa Kiba kuhusu ukaribu wake, walikuwa na haya ya kusema:
“Ukweli Ali Kiba sasa hivi tuseme amebadilika sana tangu ameoa, kwani amekuwa mtu wa kuonana na majira kila wakati na anatusaidia sana pindi mtu anapokuwa na shida, tofauti na hapo mwanzo alikuwa haonekani kila akipita amefunga vioo tinted na wala hasalimii, ila kiukweli anaishi vizuri na sisi huenda labda ‘ubachela’ ulikuwa unamsumbua."
“Kuhusu ndoa yake kuvunjika hilo siwezi kuthibitisha ila nachojua sijamuona mke wake Amina kama mwezi mmoja uuliiopita,” alisema Hanifa Maulidi jirani wa Kiba
“Kiba ni mtu wa watu kwani kwetu majirani anaishi tu vizuri nasi, hilo la kuishi na watu nyumbani kwake kiukweli sio kweli ila tunachojua sisi majirani hapa nyumbani kwa Kiba huwa tunaona magari ya aina tofauti tofauti yakiingia na kutoka hapo ndani kwake,ila suala muhimu tunamkubali sana jinsi anavyojichanganya nasi,” alisema baba James jirani wa Kiba.
Hata hivyo Kiba mwenyewe amesema hajaachana na mkewe bali amemruhusu arejee kwao Kenya kufanya kazi kama alivyomuomba.
Akihojiwa na Cloluds jana katika kipindi cha Ala za Roho, alisema licha ya uamuzi wake huo, siku za hivi karibuni walikuwa na mgogoro lakini wameumaliza.
"Mimi ninasafiri mara kwa mara na mke wangu huwa anabaki mwenyewe. Mara ya mwisho nilikuwa naenda Ulaya, hakufurahishwa na akaniuliza ninaonaje akarudi kazini kwa kuwa amesoma na ana vyeti vyake."
"Nikaona isiwe tabu nimruhusu kwani anachoongea kina ukweli. Sasa atakaa tu bila kufanya kazi hadi lini, hivi ninavyoongea yupo kwao Mombasa lakini bado tunawasiliana vizuri tu," amesema msanii huyo.
Amesema ukweli huo wa asilimia moja ni kuwa hivi sasa haishi na mkewe, ulitokea mgogoro kati yao lakini wameumaliza.
"Katika kila ndoa hakukosi mgogoro, na kwangu ndivyo ilivyotokea lakini namshukuru Mungu tuliyamaliza na sasa tupo sawa hata leo (jana) nimeongea naye na sijawahi kumpa talaka licha ya changamoto zilizotokea hapo katikati."