Nchi 48 kuziona Simba na Yanga
Rooney ameanza kurudi katika hali yake ya kawaida
MWANDISHI WETU MECHI ya Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya watani wa jadi; Simba na Yanga itaonekana karibu bara lote la Afrika. Mechi hiyo, ambayo itafanyika katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Machi 5 itaonyeshwa na kituo cha Supersport cha Afrika Kusini. Naibu Mwenyekiti wa Kampuni ya Sahara Media Group, Samweli Nyalla amekiri kuwa wamekubaliana na kituo hicho cha Afrika Kusini kuonyesha mechi hiyo kwa pamoja mwezi ujao. Nyalla, ambaye kampuni yake inamiliki Radio Free Africa (RFA) na televisheni ya Star tv, alisema lengo lao ni kukuza wigo wa michezo. "Lengo letu tunataka kukuza wigo wa kuonyesha michezo ya Tanzania nje ya nchi, tutaonyesha mechi nyingi zaidi ambazo tunadhani ni kubwa. Huu ni mwanzo tu," alisema Nyalla jana Jumatatu. Kuonyeshwa kwa mechi hiyo kupitia kituo hicho cha Supersport ina maana kuwa wachezaji wa Simba na Yanga wataonekana moja kwa moja katika nchi 48 za Afrika ambako kituo hicho cha televisheni kinapatikana. Hiyo ni habari nzuri kwa Mbwana Samatta wa Simba ambaye yupo katika kiwango cha juu kuonekana katika nchi ambazo zipo juu kisoka kwani iwapo atafanya vizuri zaidi anaweza kupata soko zuri.