Nabi: Tulieni mpate raha
YANGA leo itashuka uwanjani katika mchezo wa Kundi D la Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji wao, Real Bamako jijini Bamako nchini Mali, huku kocha wa timu hiyo, Nasreddine Nabi akiwataka mashabiki wa klabu hiyo kutokuwa na presha kwani wamejiandaa kuwapa raha.
Yanga itashuka katika Uwanja wa Machi 26, kuanzia saa 10:00 jioni (saa za Mali, sawa na saa 1:00 usiku kwa Afrika Mashariki), huku ikiwa na kumbukumbu ya mabao 3-1 iliyoyapita kwa kuifumua TP Mazembe ya DR Congo katika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Na Nabi akizungumzia ma-shindano hayo alisema licha ya mechi hiyo kuwa ngumu, lakini wamejiandaa kushinda.
Kocha huyo aliyeleta furaha kwa misimu miwili sasa ndani ya klabu hiyo alisema Real Bamako ni timu ngeni kwa Yanga, kwani haijawahi kukutana nayo katika mashindano wala michezo ya kirafiki, lakini ameifuatilia kwa siku chache na kubaini kuwa ni timu ya aina gani na amewaweka sawa vijana wake kuhakikisha wanaendeleza furaha Jangwani waliyoanza kuipata kwa Mazembe kwani wanaitaka robo fainali.
“Haitakuwa mechi rahisi. Ni timu ngeni na tumepata muda mfupi sana kuisoma, lakini bado tunaamini kwa aina ya kikosi tulichonacho tutapambana kutoka na ushindi wa kwanza ugenini katika kundi letu,” alisema Nabi na kuongeza:
“Nimezungumza na wachezaji na wanaonyesha kuwa na kiu ya kupata matokeo ugenini, hivyo naamini dakika 90 watapambana kutoka na matokeo mazuri. Mechi hii na ile ya nyumbani ni muhimu kwetu katika kujua mwelekeo wa kundi baada ya kupoteza mechi ya kwanza ugenini.”
Yanga katika mchezo wa kwanza ilipoteza kwa US Monastri ya Tunisia kwa mabao 2-0.
Hata hivyo, Nabi alisema hatarajii mabadiliko makubwa ya kikosi kilichocheza na TP Mazembe, japokuwa alisisitiza kwamba uamuzi wa mwisho utapatikana kwenye mazoezi ya mwisho ya leo (Jumamosi).
Awali, kocha huyo aliyeweka rekodi ya kuiongoza Yanga kwenye mechi 49 za Ligi Kuu Bara bila kupoteza na pia kuivusha timu hiyo hadi hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuifunga Club Africain ya Tunisia ikiwa kwao, alisema anatarajia kuwatumia washambuliaji wawili Fiston Mayele na Kennedy Musonda kama alivyofanya kwa TP Mazembe na mpango huo kutiki kwa kushinda 3-1, huku wote wakihusika na mabao.
Musonda alifunga bao la kuongoza na kuasisti bao la pili lililofungwa na Mudathir Yahya, huku Mayele akiasisti bao la tatu la timu hiyo lililofungwa na Tuisila Kisinda na kuifanya Yanga kuandika rekodi ya kuwafunga Wakongomani hao kwa mara ya kwanza kwenye michuano ya CAF.