Nabi ateta na mastaa Yanga, aitaja Simba
YANGA imeshtushwa na kasi ya Simba katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara, baada ya watani wao kuendelea kugawa dozi na fasta benchi la ufundi la timu hiyo liliitisha kikao kizito na mastaa wao, kisha kukubaliana kwa pamoja kuanzia sasa kazi ni moja tu ya kushinda kwa mabao mengi.
Simba juzi usiku iliifyatua Singida Big Stars kwa mabao 3-1 na kuzidi kuibana Yanga kileleni, huku ikiwa na hazina kubwa ya mabao ikifunga 54 katika mechi 22, jambo hilo limefanya benchi la Yanga kushtuka na kusema hata wao wanapaswa kufanya kweli kama wanataka kutetea taji lao.
Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi aliliambia Mwanaspoti, kiwango kilichoonyeshwa na Simba katika mechi zao hakimnyimi usingizi sana, lakini amelazimika kuzungumza na mastaa wake kuhakikishia wanapambana kwenye mechi zao ili kutimiza lengo walilojiwekea.
Nabi alisema katika kikao chake na wachezaji, aliwaambia ushindi inayoupata Simba unamaanisha kwamba ligi bado haijamalizika na kwamba wao wanaongoza ligi tu, hivyo lazima wajipange na kuwa na kazi moja ya kupata matokeo mazuri yanayoenda sambamba na idadi ya mabao.
Nabi alisema hadi sasa Yanga haina uhakika wa kutetea taji, ila kutaka kutetea taji ni uamuzi wa timu hiyo kupitia mastaa wake kwa namna watakavyopambna kwenye mechi zao zilizosalia.
“Sote tunaona Simba inashinda mechi zake, hata sisi tuna ubora wa kushinda mechi zetu, hii nimewaambia wachezaji wangu kwamba hakuna nafasi ya kujiona tumemaliza kazi,” alisema Nabi ambaye analitafuta taji la pili mfululizo la Ligi Kuu Bara msimu huu na kuongeza:
“Acha washinde mechi zao, lakini nasi tunatakiwa kuendelea kucheza kwa ubora wetu huku tukipata matokeo bora tunayoyataka yatakayotusaidia mwishoni mwa msimu mbele ya wapinzani wetu.”
Nabi alisema anafurahia kiwango cha wachezaji wake na kwamba kila kitu kipo sawa katika kuendelea kukusanya pointi zaidi na kuongeza kwamba ushindani unaongezeka pia unawasaidia wachezaji wake kukaa makini na mechi zao ili wasikwame.
“Sisi kama makocha tunafurahia juhudi za wachezaji wetu mazoezini, kuna ushindani mkubwa sana kwa sasa katika uwanja wa mazoezi, ila hii haitoshi inatakiwa kuendana na ushindi kwenye mechi zetu,” alisema Nabi aliyeiongoza Yanga kwenye mechi 58 za ligi na kupoteza mbili.
“Presha ya namna hii naipenda naona hata wachezaji wetu wanaona ushindani uliopo hata wao wanataka mafanikio watapigania furaha yao na ile ya mashabiki wetu ambao wanatupenda wakiwa wanajaa viwanjani kokote tunakocheza.”
Yanga jana ilikuwa ikicheza mechi ya 22 ya ligi kwa msimu huu, kabla ya keshokutwa kusafiri kwenda Tunisia kuwahi pambano la Kundi D la Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Monastir.