Mzize aibua matumaini mapya
Muktasari:
- Mastaa hao wanaona endapo Mzize akirudi kwenye kiwango chake kama zamani, anaweza akafuata nyayo za aliyekuwa nahodha wa Simba, John Bocco.
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Clement Mzize, amewaibua mastaa mbalimbali baada ya kufunga bao moja katika ushindi walioupata wa 2-1 dhidi ya Mashujaa, mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Oktoba 27, 2026 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Mastaa hao wanaona endapo Mzize akirudi kwenye kiwango chake kama zamani, anaweza akafuata nyayo za aliyekuwa nahodha wa Simba, John Bocco.
Msimu uliopita wa 2025-2026, Mzize alikuwa nje ya uwanja akiuguza majeraha, baada ya juzi kufunga bao hilo, mastaa mbalimbali wanaamini akirudi kwenye kiwango chake lazima atatajwa katika tano bora ya wafungaji wenye mabao mengi, pia wanatarajia atakuwa na muendelezo wa kufunga kama alivyokuwa anafanya Bocco tangu akiwa Azam na kuendelea ndani ya Simba.
Staa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Peter Tino, amesema isingekuwa majeraha ambayo yalimuweka nje, Mzize ni namba tisa ambaye alikuwa anakuja kwa kasi kama ambavyo alikuwa Bocco.
"Japokuwa mchezaji akitoka kuuguza majeraha kwa muda mrefu, inamchukua muda kidogo kurejesha makali yake, lakini kwa kuwa amefunga inamjengea kujiamini zaidi," amesema Tino na kuongeza;
"Mzize alionyesha uwezo wake wa kufunga tangu alipopandishwa kutoka kikosi B cha Yanga, kwani kabla ya kuumia misimu iliyofuata aliendelea kufunga, ndivyo alivyokuwa anafunga Bocco,hakuna msimu ambao ulipita bila kufunga."
Staa mwingine aliyemzungumzia Mzize ni mshambuliaji wa Tanzania Prisons inayocheza Ligi ya Championship, Jeremiah Juma aliyesema: "Mbali na Feisal Salum ambaye yupo kwenye fomu, kilichokuwa kimemrudisha nyuma Mzize ni majeraha, lakini alikuwa mfungaji mzuri, kurejea kwake kunatia matumaini kwamba atafanya vizuri zaidi."
Kwa upande wa staa wa zamani wa Yanga, Said Bahanuzi, amesema Mzize alianza vizuri na alikuwa na muendelezo wa kufunga kila msimu kabla ya kuumia.
"Baada ya kustaafu kwa Bocco, kwa namba tisa aliyekuwa anakuja kwa kasi ni Mzize, ingawa wapo wazawa wengi wanaofanya vizuri kama Mudhathir Yahya, Fei Toto na wengine wengi," amesema Bahanuzi.
Mbali na wanasoka waliyomchambua Mzize, msanii wa Bongo Fleva, Jay Melody amesema kabla ya nyota huyo wa Yanga kuumia, alikuwa anaona namna ambavyo alikuwa akiandikwa kutakiwa na timu za nje, jambo ambalo lilikuwa linamshawishi kumfuatilia.
"Kuna wakati pesa zilizokuwa zikitajwa zinawekwa mezani kumtaka Mzize hadi unashituka, unaona jamaa lazima atakuwa mtu wa kazi, hicho kilifanya nimfuatilie na baada ya juzi kufunga naamini atarejea kwenye piki, kuhusu ushabiki wa timu za hapa Bongo sijijui mimi napenda timu gani, inayoshinda ndiyo naisapoti."
Kati ya timu ambazo Mzize aliwahi kuhusishwa nazo ni Zamalek ya Misri, Umm Salal SC ya Qatar, Wydad AC ya Morocco, JS Kabylie ya Algeria, Kaizer Cheifs ya Afrika Kusini, Al-Ittihad ya Libya.
Mzize ambaye msimu wa 2023-2024, alifunga mabao sita na asisti saba, kisha 2024-2025 akapachika mabao 14 na asisti tano akiibuka kuwa mfungaji namba mbili, nyuma ya aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua aliyemaliza na 16. Msimu huu wa 2026-2027 ana bao moja.
Kwa upande wa Bocco ambaye alistaafu na sasa ni kocha wa Simba B, rekodi yake ya mabao akiwa Azam inaonyesha alifunga 84, Simba alikuwa na mabao 70, huku ndani ya JKT Tanzania akiwa na mabao manne.