Mwinyi aanza na rekodi Ligi Daraja la Kwanza Pemba
Muktasari:
- Timu nyingine za kundi hilo ni Jamhuri, Wawi Star, Maendeleo United, Small Fighter, Chake Chake, Umeme na New Star.
MSHAMBULIAJI wa timu ya New Stone Town, Khatib Mwinyi ameandika historia ya kufunga mabao matatu (ha-trick) katika Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Pemba.
Mabao hayo alifunga katika mchezo dhidi ya Tekeleza iliyomalizika kwa New Stone Town kushinda mabao 3-2.
Mwinyi alianza kufunga bao dakika ya kwanza ya mchezo huo akiongeza la pili dakika ya tano huku Yassin akiiandikia bao Tekeleza dakika ya 19 kabla ya Mudathir Rashid hajaongeza la pili dakika ya 61. Kabla ya hapo, Mwinyi alihitimisha hat trick yake katika dakika ya 53.
New Stone Town inashiriki Ligi Daraja la Kwanza Pemba baada ya msimu uliopita kushuka daraja, hivyo inatafuta tiketi ya kurudi Ligi Kuu Zanzibar.
Baada ya ushindi huo, New Stone Town inaongoza msimamo wa Kundi A, ikiwa na pointi sita ikifuatiwa na Dar Sports yenye pointi tano.
Kundi hilo linaundwa na timu tisa ikiwemo, New Stone Town, Dar Sports, El-legado, Machomane, Bubujiko, Tekeleza, Maendeleo Manta Eleven Boys na Mila.
Kwa upande wa Kundi B, Junguni yenye pointi sita inaongoza msimamo wa kundi hilo sawa na ilizonazo Vijana Mapinduzi iliyopo ya pili.
Timu nyingine za kundi hilo ni Jamhuri, Wawi Star, Maendeleo United, Small Fighter, Chake Chake, Umeme na New Star.