Ligi ya viziwi ilivyoacha somo Zanzibar
Muktasari:
- Hope City Deaf imeibuka mabingwa wa ligi hiyo baada ya kuifunga Wakombozi Deaf bao 1-0 katika fainali iliyochezwa Uwanja wa Mao B, Mjini Unguja, huku Wakombozi ikimaliza nafasi ya pili.
LIGI ya Viziwi Zanzibar imeshatamatika baada ya kuchezwa kwa siku 10, kuanzia Septemba 17 hadi 27, 2026, ikishirikisha timu nne za Vuka Deaf, Wakombozi Deaf, Zan Deaf na Hope City Deaf, zote kutoka Unguja.
Hope City Deaf imeibuka mabingwa wa ligi hiyo baada ya kuifunga Wakombozi Deaf bao 1-0 katika fainali iliyochezwa Uwanja wa Mao B, Mjini Unguja, huku Wakombozi ikimaliza nafasi ya pili.
Ligi hiyo imekuwa hatua muhimu kwa soka la viziwi Zanzibar, huku timu kutoka Pemba zikishindwa kushiriki kutokana na gharama za usafiri.
Baada ya kumalizika kwa ligi hiyo, wachezaji walioonyesha kiwango kizuri watachaguliwa kuunda timu itakayo representisha Zanzibar katika Mashindano ya Afrika ya Viziwi yatakayofanyika Desemba 2026 nchini Ethiopia, yakitarajiwa kushirikisha timu 17 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.
Pamoja na kumalizika kwa ligi hiyo, Mwanaspoti imezungumza na baadhi ya makocha na wadau wa soka la viziwi kufahamu mambo mbalimbali, ikiwemo changamoto zinazolikabili soka hilo, ambalo kwa mara ya kwanza ligi yake imechezwa Zanzibar.
CHANGAMOTO
Kocha wa Zan Deaf, Zuberi Zuberi, anasema ukosefu wa viwanja maalumu na vinavyokidhi mahitaji ya mazoezi ni miongoni mwa sababu zinazowafanya wachezaji kushindwa kufikia kiwango kizuri cha ushindani.
Anasema hata maeneo wanayotumia kwa ajili ya mazoezi hayatoshi, hali inayowafanya wachezaji kushindwa kuwa na pumzi ya kutosha wakati wa mechi.
“Changamoto tuliyokuwa nayo ni kutokuwa na viwanja vya kufanyia mazoezi. Vilivyopo havitoshelezi wala havikidhi mahitaji yetu, ndiyo maana wachezaji wanakosa pumzi wakati wa mchezo,” anasema.
Kwa upande wake, Kocha wa Vuka Deaf, Abdalla Omary, anasema makocha ambao si viziwi hukumbana na changamoto kubwa ya mawasiliano wanapotoa maelekezo wakati mchezo ukiendelea, ambapo hali hiyo inamlazimu kocha kusubiri hadi mapumziko ili kutoa maelekezo au kutumia mchezaji mmoja anayefahamu anachotakiwa kufanya, kisha awaelekeze wenzake. “Unapowapa maelekezo hawakusikii, hivyo unalazimika kusubiri hadi mapumziko ili uwaelekeze au umpate mmoja ambaye anaweza kuelewa unachotaka, kisha awaambie wengine. Kinyume na hapo inakuwa ngumu,” amesema.
Abdalla analipongeza Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) kwa kuanzisha ligi hiyo na kuwapa fursa wachezaji viziwi kuonyesha vipaji vyao, huku kocha wa Hope City Deaf, Rashid Yahya akidai licha ya ligi hiyo kuchezwa kwa mara ya kwanza, imekuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote hadi kufikia hatua ya fainali. Rashid anasema ubingwa huo umetokana na uwezo wa timu yake kuwadhibiti wapinzani katika mchezo wa fainali, huku akieleza matumaini ya kupewa nafasi ya kuinoa timu ya Taifa ya Viziwi ya Zanzibar itakayoundwa.
JINSI WAAMUZI WANAVYOWASILIANA
Mkalimani na Ofisa Habari wa Shirikisho la Viziwi Zanzibar (SHIMIVIZA), Ismail Amir, anasema kutokana na wachezaji kuwa na ulemavu wa kusikia, waamuzi hutumia filimbi na vibendera ili kuwasiliana nao wakati mchezo ukiendelea.
Anasema linapotokea jambo linalohitaji mchezo kusimamishwa, mwamuzi hupuliza filimbi na kutumia kibendera kuwaashiria wachezaji waliopo uwanjani kuacha wanachofanya na kuangalia maelekezo ya mwamuzi. Ismail anasema tofauti na mchezo wa kawaida ambao waamuzi wasaidizi hutumia vibendera viwili, katika soka la viziwi waamuzi wote watatu hutumia vibendera kwa ajili ya kutoa ishara mbalimbali uwanjani.
SHIMIVIZA YATOA NENO
Katibu wa SHIMIVIZA, AbdulAzizi Mohammed Mahfoudh, anaishukuru ZFF kwa kuwaunga mkono na kuwapa fursa wachezaji viziwi kuonyesha vipaji vyao kupitia ligi hiyo.
Anasema baada ya ligi hiyo kumalizika, tayari timu 12 zimeonyesha nia ya kushiriki msimu ujao, hivyo akatoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kuwaunga mkono.
AbdulAzizi anasema wapo wachezaji wengi wenye ulemavu wa aina hiyo ambao wana vipaji, lakini kwa muda mrefu walikosa sehemu ya kuonyesha uwezo wao na kwamba, kuanzishwa kwa ligi hiyo kumefungua fursa kwa wachezaji hao kuonyesha vipaji vyao na kuwapa mashabiki nafasi ya kufurahia soka la viziwi.
Katibu Mkuu wa ZFF, Hussein Ahmada Vuai anasema wamefurahishwa na namna walivyoweza kusimamia mashindano hayo hadi kufikia tamati.
Amesema ZFF iliona umuhimu wa kurudisha furaha kwa jamii ya viziwi kupitia michezo, jambo lililosababisha kuanzishwa kwa ligi hiyo ili kuwapa wachezaji nafasi ya kushiriki, kuonyesha vipaji na kufurahia soka. Timu ya Zan Deaf FC ilianza na ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa mwanzo wa mashindano hayo, huku Majaaliwa Haji akiwa mchezaji wa kwanza kufunga bao kwenye ligi hiyo.
LIGI ya Viziwi Zanzibar iliendelea kushika kasi kisiwani hapa baada ya mchezo kati ya Vuka na Wakombozi kumalizika kwa sare ya bao 1-1. Katika mchezo wa pili zilipokutana timu hizo, Zan Deaf ilipokea kipigo cha kufungwa mabao 4-1 kutoka kwa Hope City Deaf na kutangulia fainali ya ligi hiyo.
Vuka Deaf ilipoteza matumaini mara baada ya Wakombozi kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mechi ya marudio na hatimaye kuchuana na Hope City Deaf, iliyoibuka bingwa wa mashindano hayo.
Katika mzunguko wa kwanza, Hope City Deaf ilifungwa mabao 2-1 na hatimaye mzunguko huo ikaambulia kipigo. Na Hope City ndizo zilizofungua mashindano, zikianza na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya timu ya Hope City Deaf FC.