Mwamuzi afungiwa, mchezaji atoka kifungoni
Muktasari:
- Katika hatua nyingine, Kiongozi wa Raskazone, Mohamed Hilal ‘Bwax’ amefungiwa kuhudhuria mchezo wowote wa Ligi Kuu Zanzibar na Ligi Daraja la Kwanza kwa mizunguko 10 na kutozwa faini Sh1 milioni kwa kosa la kutoa lugha chafu dhidi ya waamuzi na viongozi wa Bodi.
MWAMUZI wa Abubakar Khatib ‘Kilupi’ amefungiwa kwa kipindi cha miezi mitatu huku mchezaji wa Muembe Makumbi, Ibrahim Samwel akifutiwa kadi ya njano ya pili aliyoonyeshwa katika mchezo wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL).
Mchezo huo namba 52 uliochezwa Oktoba17, 2026 kwenye Uwanja wa Mao A kisiwani Unguja ukizikutanisha Muembe Makumbi dhidi ya KMKM, ulimalizika bila kufungana. Katika taarifa iliyotolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi ya Bodi ya Ligi Zanzibar, Kilupi amefungiwa kwa kosa la kushindwa kuzitafsiri vyema sheria 17 za mpira wa miguu.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa, kitendo hicho kilisababisha kuonekana upungufu katika mchezo huo ambapo ni kosa kwa mujibu wa sura ya 27 kanuni ya tatu ya mashindano ya 2026.
“Kamati imeifuta kadi ya pili ya njano aliyoonyeshwa mchezaji wa Muembe Makumbi, Ibrahim Samwel na adhabu inayotokana na kadi hiyo ikiwemo kukosa mchezo unaofuata kutokana na kutolewa nje kwa kadi nyekundu, uamuzi huo ni kwa mujibu wa sura ya saba na kanuni ya nane ya mashindano,” ilieleza taarifa hiyo.
Pia, Kamati hiyo imewapa onyo waamuzi wasaidizi wawili, Ismail Massoud na Zagalo David kwa kosa la kuchelewa katika michezo waliyopangiwa bila sababu zinazokubalika.
Vilevile, Kamati hiyo imemuondoa Mwamuzi Haji Nyonje kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitatu kwa kushindwa kusimamia ipasavyo sheria ya 17 za mpira katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza Unguja kati ya Bridge Star na Taifa Jang’ombe, kitendo ambacho ni kinyume cha sura 27 ya kanuni ya tatu ya mashindano.
Katika hatua nyingine, Kiongozi wa Raskazone, Mohamed Hilal ‘Bwax’ amefungiwa kuhudhuria mchezo wowote wa Ligi Kuu Zanzibar na Ligi Daraja la Kwanza kwa mizunguko 10 na kutozwa faini Sh1 milioni kwa kosa la kutoa lugha chafu dhidi ya waamuzi na viongozi wa Bodi.
Aidha, mchezaji Hassan Ali Makame wa Bridge Star inayoshiriki Ligi Daraja Kwanza Unguja, amefungiwa kutocheza michezo miwili kutokana na mchezo usio wa kiungwana, huku Taifa Jang’ombe ikitozwa faini Sh500,000 kwa kosa la mashabiki wake kurusha chupa uwanjani na kutoa lugha ya matusi dhidi ya waamuzi.