Muya afichua siri KMC FC
Muktasari:
- Katika mechi saba ilizocheza KMC FC msimu wa 2026-2027, imeshinda nne na kutoka sare tatu, ikiongoza kwenye msimamo na pointi zake 15, huku safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho ikifunga mabao 15 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano.
KOCHA Mkuu wa KMC FC, Mohamed Muya amesema sababu ya mwenendo mzuri wa kikosi hicho hadi sasa, ni kutokana na maandalizi bora kabla ya msimu (Pre Season), yaliyoipa timu hiyo nafasi nzuri ya kujiandaa kwa takribani wiki tatu jijini, Arusha.
Akizungumza na Mwanaspoti, Muya amesema haikuwa rahisi kuwaunganisha wachezaji wa timu hiyo kwa muda mfupi, ingawa, wiki tatu ambazo waliweka kambi ya kujiandaa jijini, Arusha zilitosha kutengeneza muunganiko wa kiuchezaji kwa kikosi hicho.
“Ni mapema sana kwa sababu hata raundi ya kwanza hatujaimaliza, ila kuna maendeleo mazuri ya kiuchezaji na kimfumo kwa ujumla, ninachojaribu kufanya kwa sasa ni kutoa nafasi kwa kila mmoja kuonyesha kipaji chake alichonacho,” amesema Muya.
Aidha, Muya aliyewahi kufundisha timu mbalimbali za Fountain Gate, Geita Gold na Coastal Union, amesema malengo yake kwa ujumla ni kukipambania kikosi hicho kirejee kucheza Ligi Kuu Bara, baada ya kushuka daraja msimu uliopita wa 2025-2026.
Katika mechi saba ilizocheza KMC FC msimu wa 2026-2027, imeshinda nne na kutoka sare tatu, ikiongoza kwenye msimamo na pointi zake 15, huku safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho ikifunga mabao 15 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano.