Kachwele: nimekuja kuiokoa FC Kryvbas
Muktasari:
- Kachwele, mwenye umri wa miaka 21, amejiunga na Kryvbas kama mchezaji huru akitokea Halifax Wanderers ya Canada, akisaini mkataba wa miaka minne ambao unatamatika hadi mwaka 2029.
MSHAMBULIAJI wa Tanzania, Cyprian Kachwele, amesema amejiunga na FC Kryvbas ya Ukraine akiwa na dhamira ya kuisaidia klabu hiyo kutoka kwenye kipindi kigumu inachopitia na kuirejesha kwenye matokeo mazuri.
Kachwele, mwenye umri wa miaka 21, amejiunga na Kryvbas kama mchezaji huru akitokea Halifax Wanderers ya Canada, akisaini mkataba wa miaka minne ambao unatamatika hadi mwaka 2029.
Akizungumza kuhusu kujiunga na timu hiyo, Kachwele amesema ni heshima kubwa kwake kucheza katika klabu kubwa nchini Ukraine, akieleza kuwa ana furaha kupata nafasi hiyo ya kuonyesha uwezo wake.
“Ninafurahi sana kuwa hapa. Kryvbas ni klabu kubwa nchini Ukraine, kwa hiyo kwangu ni heshima kubwa kujiunga na timu,” amesema mshambuliaji huyo wa Tanzania.
Kachwele amesema kabla ya kuhamia Kryvbas alikuwa akifuatilia mechi za timu hiyo, hivyo alifahamu changamoto iliyokuwa ikiikabili na kuaamua kujiunga nayo akiwa na dhamira ya kusaidia kubadilisha hali hiyo.
“Nilitazama mechi kabla ya kuhamia. Sasa timu inapitia kipindi kigumu, kwa hiyo nilikuja hapa kupigania, kusaidia klabu na kubadilisha hali hiyo kuwa bora,” amesema Kachwele.
Timu hiyo ipo mkiani mwa msimamo wa ligi yenye timu 16, kwenye mechi saba za ligi timu hiyo imeshinda moja tu ikitoa sare mbili na kupoteza nne. Mbali na kutaka kuisaidia timu hiyo mpya, mshambuliaji huyo amesema uamuzi wa kuhamia Ukraine ni sehemu ya mipango yake ya kukuza kiwango na kupiga hatua katika taaluma yake ya soka, akiamini mazingira mapya yatampa nafasi ya kujifunza na kuimarika zaidi.
“Kwangu hii ni fursa nzuri ya kukua kama mchezaji na kusonga mbele katika kazi yangu,” amesema Kachwele.