Mtihani wa Ngorongoro AFCON U-20
Muktasari:
- Katika safari yake ya CECAFA, Ngorongoro ilikutana na timu zinazofahamika katika ukanda huo kama Kenya, Uganda, Djibouti na Sudan, huku kikosi hicho kikionyesha uimara mkubwa, hasa kwenye safu ya ulinzi.
TIMU ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, imefanikiwa kukata tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa Vijana (AFCON U-20) mwaka 2027 zitakazofanyika nchini Ghana, lakini kufuzu huko si mwisho wa safari. Badala yake, ni mwanzo wa mtihani mkubwa unaosubiri kikosi hicho katika hatua inayofuata.
Baada ya kufanya vizuri katika michuano ya ukanda wa CECAFA U-20, Ngorongoro Heroes sasa inatakiwa kugeuza uzoefu huo kuwa nguvu itakayoiwezesha kushindana na timu kutoka maeneo mbalimbali ya Afrika.
Katika safari yake ya CECAFA, Ngorongoro ilikutana na timu zinazofahamika katika ukanda huo kama Kenya, Uganda, Djibouti na Sudan, huku kikosi hicho kikionyesha uimara mkubwa, hasa kwenye safu ya ulinzi.
Kuanzia hatua ya makundi hadi nusu fainali, Ngorongoro iliendelea kucheza bila kuruhusu bao, jambo lililoonyesha nidhamu ya kikosi na uwezo wa kukabiliana na presha ya wapinzani.
Muhimu zaidi, Ngorongoro ilipata tiketi ya AFCON U-20 baada ya kufika hatua ya fainali, ni kutokana na ukweli kwamba CECAFA U-20 ilikuwa na nafasi mbili za kuiwakilisha katika fainali za AFCON U-20, hivyo kufika fainali kulitosha kuhakikisha Tanzania na Sudan kupata nafasi hizo.
Hivyo, fainali iliyozikutanisha Ngorongoro na Sudan ilikuwa ya kuwania ubingwa wa CECAFA U-20, huku tiketi ya AFCON U-20 ikiwa tayari imepatikana.
Hata hivyo, Ngorongoro ilishindwa kumaliza safari hiyo vizuri baada ya kupoteza dhidi ya Sudan kwa mikwaju ya penalti 4-3.
Matokeo hayo yanaweza kuwa somo muhimu kwa kikosi hicho, hasa ikizingatiwa mafanikio ya mwaka 2022, wakati Tanzania ikiwa mwenyeji katika uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam, ilipotwaa ubingwa baada ya kuifunga Uganda bao 1-0.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), baada ya kumalizika kwa mashindano hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 15, 2026 na kuhitimishwa Septemba 24, 2026, Ngorongoro Heroes imetoa wachezaji watano ikiwa ni idadi kubwa kuliko taifa lolote lililoshiriki. Sudan inafuatia ikiwa na wanne, huku Burundi na Uganda zikiwa na mmoja.
Wachezaji watano wa Ngorongoro Heroes katika kikosi hicho ni kipa Shabani Bakari, mabeki wa kati Evastus Lukanima na Abubakar Nizar Othman ‘Ninju’. Eneo la kiungo yupo Bashir Salum Kibaila na Juma Abushiri ‘Chuga Boy’.
Kikosi hicho kilichowekwa katika mfumo wa 4-3-3, kipo hivi; kipa Shabani Bakari (Tanzania); Mabeki: Samaan Amin Koda (Sudan), Osama Amen Abdalla (Sudan), Evastus Lukanima (Tanzania) na Abubakar Nizar Othman (Tanzania).
Viungo watatu wanaocheza kati ni Rudwan Yahya Mohamed (Sudan) akiwa kiungo wa chini, juu yake wapo Isima Magala (Uganda) na Bashir Salum Kibaila (Tanzania).
Kule juu kwenye ushambuliaji, Mazin Fadul Albahli wa Sudan anatokea upande wa kushoto, wakati Juma Abushiri kutoka Tanzania akiwa upande wa kulia, huku Amini Nshimirimana wa Burundi akisimama mshambuliaji wa mwisho. Kumbuka mshambuliaji huyo ameacha alama katika michuano hiyo baada ya kufunga mabao manne katika michezo miwili ya hatua ya makundi akiwa ndiye mfungaji bora.
GHANA NI MTIHANI MWINGINE
Sasa macho yanaelekezwa Ghana, AFCON U-20 itakuwa mtihani wa kiwango kingine kwa Ngorongoro. Huko, haitakutana na wapinzani kutoka ukanda mmoja pekee, bali timu zenye mitindo, falsafa na uzoefu tofauti wa soka kutoka sehemu mbalimbali za Afrika.
Katika ukanda wa Magharibi, Ngorongoro inaweza kukutana na timu kama Ghana, Nigeria na Ivory Coast, ambazo zinatoka katika mazingira yenye ushindani mkubwa wa soka.
Kutoka Kusini mwa Afrika, kuna timu kama Afrika Kusini, Botswana na Zimbabwe, huku upande wa Kaskazini ukiwa na nchi kama Misri na Morocco. Hii ina maana kwamba kiwango cha ushindani kitabadilika.
Kufanya vizuri dhidi ya Kenya, Uganda au Djibouti ni jambo moja, lakini kukabiliana na timu zenye uzoefu mkubwa wa mashindano ya bara ni changamoto nyingine.
Ngorongoro itahitaji kuwa tayari kukabiliana na kasi tofauti za mchezo, ubora wa wachezaji, mbinu mbalimbali pamoja na presha inayoweza kuambatana na mashindano makubwa.
URITHI WA WALIOPITA
Kikosi hiki pia kinaingia Ghana kikiwa na jukumu la kuendeleza heshima iliyoachwa na timu za vijana zilizowahi kutangulia.
Tanzania imewahi kuwa na vikosi vya vijana vilivyoshiriki AFCON na kutumia mashindano hayo kama daraja la kufikia hatua kubwa zaidi, ikiwemo kupata tiketi ya kucheza Kombe la Dunia.
Hivyo, kwa kizazi hiki, Ghana haitakiwi kuwa safari ya kushiriki na kurudi nyumbani.
Ni nafasi ya wachezaji hawa kuandika historia yao wenyewe na kuonyesha kwamba wanaweza kushindana zaidi ya mipaka ya ukanda wa CECAFA.
KOMBE LA DUNIA LINASUBIRI
Uzito wa safari hii unaongezeka zaidi kutokana na fursa ya kufuzu Kombe la Dunia U-20.
Katika mashindano hayo, timu mbili zitakazofika fainali zitapata nafasi ya moja kwa moja ya kushiriki Kombe la Dunia. Hii inaifanya AFCON U-20 ya Ghana kuwa zaidi ya mashindano ya kawaida kwa Ngorongoro, ni jukwaa ambalo linaweza kuwapa wachezaji nafasi ya kujitangaza, kuonyesha uwezo wao na wakati huohuo kuisogeza Tanzania karibu na hatua kubwa zaidi ya kimataifa.
SASA KAZI NI HII
Ngorongoro Heroes imeshafanya sehemu yake CECAFA U-20, imefuzu, imepata uzoefu na imeonyesha kuwa inaweza kucheza kwa nidhamu. Kabla ya kufikiria fainali au Kombe la Dunia U-20, kazi ya kwanza ni maandalizi ya kutosha.
Maandalizi hayo yanahitaji kiwango kinachoendana na changamoto itakayokutana nayo Ghana. Kikosi kinahitaji umakini, nidhamu, kujiamini na uwezo wa kubadilika kulingana na mpinzani, ni muhimu wachezaji kutumia kila mchezo kama nafasi ya kujifunza na kuboresha mapungufu yaliyoonekana katika safari ya CECAFA.
Lakini ardhi ya Ghana ndiyo itakayotoa picha pana zaidi ya uwezo wa kizazi hiki.
Tiketi ipo mfukoni, lakini kazi kubwa sasa ni kuonyesha kwamba Tanzania haiendi Ghana kushiriki tu, bali kwenda kushindana na kutafuta hatua kubwa zaidi.