Mtihani kwa Gamondi, Stars ikihitaji kulipa kisasi
Muktasari:
- Hiyo ndiyo picha ya mechi ya leo kati ya Taifa Stars na Nigeria, itakayopigwa saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, ukiwa ni wa nne kwa timu hizo katika harakati za kuwania nafasi kwenye kundi hilo.
BAADA ya Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars Novemba 13, 2026 kupokea kichapo cha mabao 3-1 dhidi ya Nigeria kwenye mechi ya Kundi L kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), ina kibarua kingine kwenye mechi ya marudiano leo Jumanne kuipa uhai wa ushindani kwenye kundi hilo.
Hiyo ndiyo picha ya mechi ya leo kati ya Taifa Stars na Nigeria, itakayopigwa saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, ukiwa ni wa nne kwa timu hizo katika harakati za kuwania nafasi kwenye kundi hilo.
Taifa Stars inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa na mtihani mkubwa hususani kwa Kocha Mkuu, Miguel Gamondi, ambaye anahitaji kuonyesha mabadiliko ya kiwango cha kikosi hicho baada ya mwenendo usioridhisha katika mechi zake zilizopita.
Kwenye mechi tatu Taifa Stars ilipoteza kwa Nigeria 3-1, ikatoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Madagascar na ile ya kwanza ilipopoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Guinea Bissau.
Pamoja na Tanzania kuwa mwenyeji wa fainali hizo za AFCON 2027 kwa kushirikiana na Kenya na Uganda jambo linaloifanya kufuzu moja kwa moja, bado mechi hizo zina umuhimu mkubwa katika kujenga ushindani na kuonyesha timu inaweza kusimama wapi mbele ya mataifa makubwa ya Afrika.
Safari hii, mazingira ni tofauti kwa Stars, ambayo itakuwa na faida ya kucheza mbele ya mashabiki wake Zanzibar, jambo linalopaswa kutumiwa kuongeza nguvu ya kupambana na kuhakikisha inaleta picha nzuri kwa waandaaji.
Hata hivyo, changamoto kubwa ipo kwenye namna kikosi hicho kitakavyoweza kujipanga na kuhimili ubora wa Nigeria, hasa katika eneo la ushambuliaji ambalo limekuwa na wachezaji wenye uwezo wa kubadili matokeo ya mechi wakati wowote.
Presha nyingine ipo kwa Gamondi, ambaye katika mechi tisa alizokiongoza kikosi hicho amepata ushindi mmoja pekee, sare tatu na vipigo vitano, takwimu zinazoonyesha kazi aliyonayo katika kukijenga upya kikosi hicho.
Ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Macau kwenye mashindano ya FIFA Series 2026 nchini Rwanda ndio pekee alioupata, huku matokeo mengine yakionyesha timu hiyo bado inahitaji kufanya kazi kubwa katika maeneo ya beki na ushambuliaji.
Katika mechi hizo tisa, Stars imefunga mabao 13 na kuruhusu idadi hiyo hiyo ya mabao, jambo linaloonyesha kuwa bado haijapata uwiano mzuri wa kiushindani.
Hivyo, mchezo wa leo ni nafasi ya Gamondi kuonyesha kama ameanza kupata majibu ya changamoto hizo, hasa katika kuhakikisha Stars inakuwa imara zaidi inapokuwa haina mpira na yenye makali inapopata nafasi za kushambulia.
Ni vita ya pointi, heshima na kulipiza kisasi, huku macho yakielekezwa kwa Gamondi kuona kama ataweza kutumia vyema faida ya kucheza nyumbani na kuipa Tanzania matokeo inayoyahitaji dhidi ya moja ya miamba ya soka la Afrika.
Akizungumza na Mwanaspoti, mfungaji wa bao kwenye mechi iliyopita, Alphonce Mabula, amesema: “Mashabiki wajitokeze kwa wingi kuja kutusapoti, najua hatukufanya vizuri mechi iliyopita lakini tunawahakikishia kuonyesha kiwango bora nyumbani.”
Akizungumzia kuhusu bao lake la kwanza tangu aanze kuitumikia Taifa Stars mwaka 2025, amesema: “Namshukuru Mungu ni kitu kikubwa kwangu nimeingia kwenye historia pia nimeifunga moja ya timu kubwa Afrika ndio inafanya zaidi kuwa kitu maalum na kumbukumbu yangu ya milele.”