Mtego mzito Yanga
Muktasari:
- Hakuna ubishi kwamba Yanga ndio Baba Lao kwenye soka la Bongo. Hata kama we hutaki, lakini namba daima huwa hazidanganyi. Yanga imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara 27, ikiwa ndio kinara. Pia kwenye Ligi Kuu ya Muungano nako si haba. Hata kwenye michuano ya Kombe la FA ambayo kwa sasa ni maarufu kama Azam Sports Federations Cup (ASFC) nako ni balaa zaidi.
HAKUNA ubishi kwamba Yanga ndio Baba Lao kwenye soka la Bongo. Hata kama we hutaki, lakini namba daima huwa hazidanganyi. Yanga imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara 27, ikiwa ndio kinara. Pia kwenye Ligi Kuu ya Muungano nako si haba. Hata kwenye michuano ya Kombe la FA ambayo kwa sasa ni maarufu kama Azam Sports Federations Cup (ASFC) nako ni balaa zaidi.
Rekodi zinaonyesha tangu michuano hiyo ilipoasisiwa mara ya kwanza mwaka 1967, Yanga wametwaa mara tano.
Ilitwaa mwaka 1967 kwa kuifunga Liverpool, kisha michuano ikapotea hadi mwaka 1974 Vijana wa Jangwani wakabeba tena kwa kuinyoa Simba, wakaja wakaibuka tena 1999 na 2001 wanabeba tena kwa kuinyoosha Moro United.
Kombe la FA lilichezwa mara ya mwisho 2002 pale JKT Ruvu walipobeba, kisha ikapita muda mrefu bila michuano hiyo kuchezwa tangu 2003 hadi 2015.
Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), chini ya Jamal Malinzi ikarejesha michuano hiyo mwaka 2015 likiwa na jina jipya la Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).
Michuano hiyo iliporejeshwa tena, Yanga kama kawaida wakalibeba tena taji hilo kwa kuinyoa Azam FC na tangu hapo haijawahi tena kubeba kombe la michuano hiyo.
Juzi kati Yanga imepenya nusu fainali ya michuano hiyo kwa kuinyoa Mwadui ya Shinyanga kwenye mchezo mtamu uliopigwa Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Mabao mawili ya Deus Kaseke ndiyo yaliyoivusha Yanga kutinga hatua hiyo na sasa inavaana na Biashara United iliyotangulia mapema kwa kuinyuka wana fainali wa msimu uliopita, Namungo FC. Yanga ina mtego mmoja tu kuvuka nusu fainali hii. Mwanaspoti linakuletea rekodi tata za Yanga kwenye hatua ya nusu fainali na kama haitajipanga vizuri isitarajie kupenya kwenda fainali ili kulirejesha taji hilo kwa mara yao ya sita na kufuta ukame wa miaka karibu mitano iliyopita.
VITA NA WAGOSI
Msimu michuano ya FA iliporejea ikiwa na jina la ASFC, Yanga ilipenya fainali kwa mbinde mbele ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union walipovaana katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga. Kwa wanaokumbuka pambano hilo, lilijaa ubabe na vurugu kubwa ikiwamo kupigwa kwa mwamuzi wa pembeni, aliyelalamikiwa na Wagosi kuwabeba Yanga ambao walishinda mabao 2-1.
Hiyo ndiyo iliyokuwa nusu fainali ya kwanza kwa Yanga kuivuka salama kwenda fainali na hatimaye kubeba ubingwa kwa kuwafumua Azam kwa mabao 3-1,yaliyofungwa na Amissi Tambwe aliyetupia mawili na jingine la Deus Kaseke. Kwani baada ya hapo kama hujui ni kwamba Yanga imekuwa ikikwamia hatua hiyo na wakati mwingine kukumbana na aibu isiyotarajiwa katika nusu fainali ambayo kwa sasa inajiandaa kucheza na Biashara.
MBAO YAWATIBULIA
Msimu wa pili wa ASFC, Yanga ilicheza kama watetezi wa taji na ilionekana kama vijana hao wa Jangwani wangelitetea taji na kuandika rekodi. Ndio katika michuano hiyo hakuna timu iliyowahi kutetea taji, lakini Yanga wakaonekana kama wanaenda kufanya kweli. Hata hivyo bao la kujifunga la beki wake wa kati, Vincent Dante kwenye mchezo mkali uliopigwa CCM Kirumba, jijini Mwanza liliiing’oa Yanga mbele ya wageni wa Ligi Kuu Bara wakati huo, Mbao FC ya Mwanza. Yanga ilianza mkosi wake wa kung’olewa hatua ya nusu fainali kwa kulala bao 1-0 na kuliacha taji likienda kubebwa na watani wao, Simba waliowafunga kwa mbinde Mbao kwa mabao 2-1 katika mchezo uliopichezwa kwa dakika 120 jijini Dodoma.
SINGIDA YAWAHARIBIA ZAIDI
Katika msimu wa 2017-2018, huenda Yanga haina hamu nao, kwani mambo yaliwaendea kombo, kipindi hicho ikiwa majalala. Yanga ilikuwa na majanga!
Kwanza ilikuwa ilitafunwa na ukata mkali wa kifedha, lakini hata uwanjani mambo yalienda halijojo, kwani ilitema ubingwa wa Ligi Kuu Bara iliyokuwa ikiushikilia kwa misimu mitatu mfululizo.
Taji la Ligi Kuu Bara lilinyakuliwa na Simba, lakini kwenye Kombe la ASFC waliishia robo fainali baada ya kutibuliwa na Singida United katika mechi kali iliyopigwa Uwanja wa Namfua, mjini Singida. Yusuph Mhilu aliyekuwa akikipiga Jangwani enzi hizo, aliitangulia Yanga kwa bao la dakika ya pili tu, lakini kiungo fundi, Kenny Ally alisawazisha bao na goma kwenda kwenye penalti na Yanga kung’oka.
LIPULI YAIZIMA KIBABE
Baada ya kukwama kutinga nusu fainali, Yanga ilirejea tena kwenye michuano hiyo kibabe na kuonekana kama ingeenda kubeba ubingwa wa michuano.
Hata hivyo, Wanapaluhengo, Lipuli FC waliwazima kwa kuwafunga mabao 2-0 katika mchezo wa nusu fainali iliyopigwa Uwanja wa Samora, mjini Iringa.
Katika mechi hii, Yanga ilienda Iringa ikiwa na kumbukumbu ya kushinda kwenye uwanja huo katika mechi ya Ligi Kuu, lakini mabao mawili ya kipindi cha kwanza ya kina Paul Nonga na Jimmy Shonji yaliyotosha kuing’oa kwenye michuano hiyo. Huku lawama zikienda kwa mabeki wa Jangwani na kipa wao wa wakati huo Klaus Kindoki.
Msimu huo wa 2018-2019 Yanga ilijikuta ikitoka kapa kwa kushindwa kurejesha ubingwa wa Ligi Kuu Bara uliobebwa tena na Simba na Kombe la ASFC lilitwaliwa na Azam FC walioitungua Lipuli katika fainali kwa bao la Mzambia Obrey Chirwa.
AIBU ILIKUWA HAPA!
Hakuna asiyejua Kariakoo Derby inavyochukuliwa kwa uzito mkubwa, bila kujali huwa ni mechi ya michuano gani.
Msimu uliopita ndio uliokuwa wa aibu kwa Yanga, kwani baada ya kupenya salama robo fainali ya Kombe la ASFC dhidi ya Kagera Sugar, ikajikuta inakutana na watani wao, Simba iliyowavua ubingwa Azam kwa kuifumua mabao 2-0.
Yanga wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 katika Ligi Kuu Bara dhidi ya watani wao, bao lililotupiwa kambani kwa mkwaju wa friikiki ya Bernard Morrison, ilishuka Uwanja wa Taifa (sasa Benjamin Mkapa) na kuchapika.
Yanga ilifumuliwa 4-1 na kun-g’olewa kwenye hatua ya nusu fainali na kuwaacha wapinzani wao wakienda kulibeba taji kwa mara ya pili kwa kuitungua Namungo ya Lindi kwa mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliopigwa Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga, Rukwa.
Katika mchezo huo wa nusu fainali uliokuwa mkali, Simba ilipata mabao kupitia Mbrazil Gerson Fraga, Clatous Chama, Luis Miquissone na Mzamiru Yasin, huku la kufutia machozi la Yanga lilifungwa na Feisal Salum.
MSIMU HUU WATATOBOA?
Yanga inakutana na Biashara katika mechi ambayo haitakuwa ya kwanza kukutana nao kwenye michuano hiyo. Misimu miwili iliyopita, Yanga ilishakutana na Biashara United katika ASFC hatua ya 32 Bora uliopigwa Uwanja wa Taifa (sasa Mkapa) na Yanga walishinda kwa mbinde mabao 2-1.