Mtani! Tripu hii sikuachi...
KUNA mambo mawili kwenye mechi ya leo Jumapili saa 11 kamili jioni kwenye Uwanja wa Mkapa. Achana na ishu ya Moses Phiri kupania kuifunga Yanga kwa mara ya kwanza. Au Aziz Ki kutaka kuweka heshima katika dabi kama Tuisila Kisinda alivyopania kupata penalti mbele ya safu ya ulinzi ya Simba.
La kwanza, Fiston Mayele amepania kwa namna yoyote ile kuwafunga Simba bao la kwanza kwenye Ligi huku Simba na wenyewe wakiapa kwa kauli zote kwamba wamechoka kufungwa na mtani kwenye Ligi. Utakumbuka Simba ilimfunga Yanga kwenye Ligi mara ya mwisho Februari 16,2019 akitupia bao Meddie Kagere.
Mabenchi ya ufundi kazi ni ngumu ya kuandaa mpango bora wa mechi utakaobebwa na ufundi na juhudi za wachezaji ambao utafanya timu moja iwe bora zaidi kuliko nyingine ndani ya uwanja kupata matokeo mazuri yatakayofanya ijiimarishe kileleni mwa msimamo wa ligi na kupata heshima dhidi ya mtani wake.
Baada ya mwanzo mzuri wa kila upande katika Ligi Kuu msimu huu, mchezo huo hapana shaka ni kipimo tosha cha namna gani makocha wa kila upande wanaweza kutoa mbinu na mikakati bora zaidi inayoweza kutumiwa na wachezaji kuipatia timu matokeo katika mazingira magumu na yenye presha kubwa.
NABI NA YANGA YAKE
Staili ya kumiliki mpira kwa kupiga pasi nyingi kuelekea langoni mwa timu pinzani imekuwa ndio ikitumiwa na Yanga kwa muda mrefu tangu kocha Nasreddine Nabi alipoanza kuinoa timu hiyo.
Ubora na uwezo wa viungo wa Yanga katika kumiliki mpira na kupiga pasi umeifanya timu hiyo kutegemea zaidi eneo la katikati kuwa mhimili wa kuichezesha timu, kupika mabao na kuipa ulinzi timu.
Utajiri wa kundi kubwa la wachezaji wanaomudu staili hiyo, umemfanya kocha Nabi kutokuwa na kikosi cha kwanza cha kudumu na badala yake amekuwa akitoa nafasi kwa wachezaji wengi tofauti kutegemeana na aina ya mpinzani wanayekutana naye na namna mechi ilivyo.
Kutokana na hilo, hapana shaka ni vigumu kutabiri ni nani na nani ambao Nabi atawatumia katika kikosi chake cha kwanza kwenye mechi ya kesho dhidi ya Simba kutokana na mabadiliko ambayo amekuwa akiyafanya mara kwa mara kwenye kikosi chake.
Ukiondoa kipa Djigui Diarra, beki wa kulia, Djuma Shaban na mshambuliaji wa kati Fiston Mayele, kumekuwa na mabadiliko ya wachezaji wengine katika nafasi mbalimbali kutegemeana na mechi husika.
Kibwana Shomari amekuwa akitumika upande wa beki ya kushoto ambao pia kocha Nabi amekuwa akimpanga Joyce Lomalisa na mabeki wa kati wa-mekuwa wakicheza Dickson Job na Yannick Bangala ambaye anaweza kusogezwa katika nafasi ya namba sita, kisha nafasi ya beki akapangwa Bakari Mwamnyeto.
Siku kadhaa zilizopita, Mwamnyeto alionekana kufanya makosa ya kiulinzi ambayo yalikuwa mara kadhaa yakiigharimu timu ingawa Nabi alisimama hadharani kumtetea na hata kumpanga katika baadhi ya mechi.
“Wakati nafika hapa nimemkuta Mwamnyeto anacheza kikosi cha kwanza akiwa katika ubora mkubwa, wakati huohuo alikuwa mchezaji muhimu katika ukuta wa timu ya taifa kila mchezo wa timu hiyo alicheza bila kupumzika, huyu ni binadamu anachoka, tulipaswa kuwa naye pamoja kila wakati na sio kumchoka,” alinukuliwa Nabi.
Kama Bangala atacheza namba sita, anaweza kupangwa sambamba na Khalid Aucho katika mfumo wa 4-2-3-1, jambo litakalofanya Aziz Ki apangwe katika nafasi ya winga kisha Feisal Salum asimame nyuma ya mshambuliaji wa kati na hapo inabakia nafasi moja ya winga ambayo, Nabi anaweza kumpanga ama Farid Musa, Ducapel Moloko ama Tuisila Kisinda.
SIMBA YA MGUNDA
Chini ya kocha Juma Mgunda, Simba imeonekana kuwa na mabadiliko kadhaa ya wachezaji na ya kiuchezaji ambayo yameonekana kuwa chachu ya mafanikio ya timu hiyo katika mechi zake.
Simba imeonekana kupiga pasi chache na kutumia mipira mirefu pindi inapojenga mashambulizi kuelekea langoni mwa timu pinzani ikiwatumia zaidi viungo washambuliaji wake wenye uamuzi wa haraka akiwamo Moses Phiri.
Kumuondoa Mohamed Ouattara na kumtumia Joash Onyango katika nafasi ya beki wa kati, kumeongeza kasi na unyumbulifu kwa Simba katika safu ya ulinzi ya Simba jambo linalofanya uimara uongezeke zaidi langoni mwao.
Nafasi ya viungo wawili wa ulinzi, amekuwa akitumika Mzamiru Yassin badala ya Jonas Mkude, akicheza sambamba na Sadio Kanoute, mabadiliko ambayo yameisaidia safu yake ya ulinzi kutofikiwa mara kwa mara kutokana na uwezo mkubwa wa wawili hao katika kuziba mianya na kupora mipira kwa wapinzani.
Augustine Okrah ambaye hakuwa tegemeo chini ya kocha Zoran Maki, amefanywa kuwa mmoja kati ya wasanifu wakuu wa mashambulizi ya Simba kwa kushirikiana na Clatous Chama ambaye amekuwa akipangwa nafasi ya nyuma ya mshambuliaji wa kati.
Nafasi pekee ambayo Mgunda anaonekana kutopata jibu la moja kwa moja ni ile ya wingi moja ambapo kuna nyakati amekuwa akimtumia Pape Sakho na muda mwingine humapnga Kibu Denis.
“Wachezaji wote wapo kwa ajili ya kuitumikia Simba. Jambo la muhimu ni timu kufanya vizuri na kila mmoja anapaswa kujituma pindi anapopewa nafasi,” alisema Mgunda.
SILAHA ZA AKIBA
Achana na mastaa 11 watakaoanza katika kila upande, kutakuwa na wengine baadhi ambao hapana shaka makocha wa timu hizo watawategemea kwenda kuokoa jahazi, kusaka au kulinda ushindi wakitokea benchi.
Nyota hao kwa upande wa Yanga ni Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Denis Nkane, Farid Musa na Heritier Makambo wakati kwa upande wa Simba ni Peter Banda, Pape Sakho, John Bocco na Kennedy Juma.
Kocha wa Simba, Juma Mgunda alisema mchezaji yeyote aliyemo katika kikosi chake anaweza kutumika kulingana na mahitaji.
“Kila mchezaji ni muhimu na ana mchango wake. Wachezaji wote watakaokuwepo kikosini, kila mmoja maana yake ana utayari wa kucheza mechi husika,” alisema Nabi.
REFA WA SARESARE
Refa Ramadhan Kayoko hana rekodi inayoumiza kwa timu zote mbili kwani amezichezesha timu hizo mara tatu ambapo hakuna moja iliyopata ushindi dhidi ya mwenzake mara nyingi.
Kati ya mara hizo tatu ambazo Kayoko kazichezesha timu hizo kongwe na kubwa nchini, Yanga imeibuka na ushindi mara moja, Simba imeshinda moja huku mara moja zikitoka sare.
WAO KWA WAO
Kumbukumbu ya mechi 10 zilizopita za Ligi Kuu baina ya timu hizo, inaonyesha hakuna mbabe kati yao na hapana shaka mchezo huo unaweza kutoa mtemi au ikashindikana iwapo zitatoka sare.
Timu hizo katika mechi 10 zilizopita za Ligi Kuu, kila moja imeibuka na ushindi mara mbili huku zikitoka sare mara sita.
KIPINDI CHA PILI PRESHA
Umakini wa hali ya juu unapaswa kuwepo kwa safu za ulinzi za kila tmu katika kipindi cha pili zaidi kutokana na takwimu za mechi tano ambazo kila upande umeshacheza hadi sasa kwenye ligi, kuonyesha Yanga na Simba zimekuwa zikifunga mabao mengi muda huo kulinganisha na kipindi cha kwanza.
Kati ya mabao 11 ambayo Yanga imefunga hadi sasa, mabao saba imepachika kipindi cha pili na manne ndio imefunga katika kipindi cha kwanza.
Ni kama ilivyo kwa Simba ambayo katika mabao 11 iliyofunga kwenye mechi tano, mabao sita imeyapata kipindi cha pili na matano kwenye kipindi cha kwanza.
Kipindi hicho cha pili pia ndio muda ambao timu hizo zimeonekana kuruhusu nyavu zao kutikiswa ambapo Simba mabao yote mawili iliyofungwa yalikuwa ni ya kipindi cha pili huku Yanga yenyewe, kati ya mabao manne iliyoruhusu, mawili ni ya kipindi cha kwanza na mengine mawili ni ya katika dakika 45 za pili.
Dakika 30 za mwisho ndio huwa hatari zaidi kwani ndio muda ambao timu hizo zimekuwa zikifunga sana ambapo Yanga katika muda huo imepachika mabao matano huku Simba ikifumania nyavu mara sita.
Pamoja na takwimu hizo, kiungo wa zamani wa timu hizo, Athuman Iddi ‘Chuji’ alisema kuwa hazitoi muelekeo wa moja kwa moja wa matokeo.
“Zinapokutana timu hizi mbili, ile iliyo vizuri siku husika ndio inafanya vizuri. Takwimu na historia zipo lakini ni nadra sana kuiamua hii mechi hivyo sio za kuzitegemea sana,” alisema.
HII USIMWAMBIE MTU
Hizi ni habari za ndani kabisa. Mwanaspoti linajua yeyote atakayepoteza kesho jioni kuna jambo litamkuta.Yanga wakipoteza mchezo huo huenda mabadiliko makubwa na yakushtua yakatokea kwenye benchi la ufundi hata kabla mshahara wako wa mwezi huu haujaingia.
Lakini kama Simba itapoteza mchezo wa kesho, huenda ikarudi kwenye mafaili yao haraka na kumleta jijini Dar es Salaam kocha mpya wa kigeni ambaye atakuwa bosi wa Juma Mgunda na mwenzake Seleman Matola.