Mrithi wa Okwi huyu hapa
Muktasari:
Huyo ni Mbrazili wa tatu baada ya straika Wilker Henrique Da Silva na beki wa kati Gerson Fraga Vieira waliosaini mikataba mapema ili kukipiga Simba kwa msimu ujao.
HUKO mtaani mashabiki wamekuwa wakiuponda uongozi wa Simba kwa kitendo cha kumuacha James Kotei, huku ikielezwa pia hata Emmanuel Okwi, yule straika wa Uganda anayesumbua kwenye Fainali za Afcon 2019 kule Misri naye wanaachana naye kwa msimu ujao.
Hata hivyo, ni kama vile mabosi wa Msimbazi walikuwa wakiwalia taimingi, huku wakifanya mambo yao ya kuleta majembe mapya ya kuchukua nafasi ya nyota wa kigeni inayoachana naye akiwamo Kotei aliyetimkia Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kimyakimya.
Katika kudhihirisha kuwa, mabosi hao hawatanii wameshusha mchana nyavu mmoja matata kutoka TP Mazembe anayetajwa huenda ndiye akawa Okwi mpya Msimbazi kama watamalizana naye na kumsainisha mkataba.
Licha ya kuleta mashine hiyo mpya ambayo tayari ipo jijini Dar es Salaam, jana Ijumaa mchana Simba ilimtambulisha beki mwingine mpya ambaye ni Mbrazili wa tatu kusajiliwa na klabu hiyo kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.
Mbrazili huyo mpya, Tairone Santos da Silva amesaini mkataba wa miaka miwili kuchezea Msimbazi, ikiwa ni wiki moja tu tangu Mwanaspoti lilipomfichua baada ya kumuibukia kininja kwenye hoteli aliyokuwa amefichwa na mabosi hao wa Msimbazi.
Beki huyo alifichwa sambamba na Msudan Shiboub Sharaf Eldin na Mwanaspoti kunyaka taarifa hizo na kuimuibukia mafichoni, huku Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori akiwaka alipobaini timu ya Mwanaspoti iliweza kuwabaini nyota hao wapya.
Hata hivyo, katika kuonyesha Mwanaspoti halikurupuki, jana mabosi wa Msimbazi walimtambulisha Tairone amejiunga na akitokea Klabu ya Atlético Cearense ya kwao Brazili tayari kukinukisha Simba msimu ujao sambamba wa nyota wengine.
Huyo ni Mbrazili wa tatu baada ya straika Wilker Henrique Da Silva na beki wa kati Gerson Fraga Vieira waliosaini mikataba mapema ili kukipiga Simba kwa msimu ujao.
MKONGO MPYA
Wakati Mbrazili huyo wa tatu akitambulishwa na kuifanya Simba kufikisha wachezaji wanane wapya iliyowasajili mpaka sasa wakiwamo kipa Beno Kakolanya, Miraj Athuman, Kennedy Juma, Msudan sambamba na Ibrahim Ajibu ambaye hata hivyo, bado hajatambulishwa, Simba imemtumia tiketi mshambuliaji wa TP Mazembe, Deo Kanda aliyetua jana Ijumaa, huku pia ikizungumza na Mtogo Serge Alainnogue ili kuona kama itawasajili ama la!
Ujio wa nyota hao una lengo la kuboresha kikosi cha Simba, lakini inaelezwa Deo Kanda ndiye anayekuja kuwa Okwi mpya Msimbazi kama watamalizana naye kwani ni mzuri zaidi anapocheza nafasi ya straika wa pili (namba 10) ama winga.
Kanda mwenye umri wa miaka 29 ubora wake umeifanya TP Mazembe kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya ndani na kimataifa, kwani ni mkali wa kufumani nyavu tangu alipoanza kuichezea 2009 na 2013 alitimka kwenda Raja Casablanca ya Morocco aliyocheza kwa msimu mmoja.
Alirudi DR Congo na kuichezea AS Vita msimu mmoja wa 2014-2015, akatimkia tena Ugiriki alipojiunga na AEL, lakini hakudumu kwani msimu huo huo alirejea Mazembe akiichezea mpaka sasa na Simba ilimuona walipovaana na Mazembe katika mchezo wa robo fainali wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.
Kwa upande wa Mtogo Serge mwenye uwezo wa kucheza nafasi zote za winga pamoja na namba 10, alitumiwa tiketi na Simba wiki iliyopita na kufichwa jijini Dar akiendelea na majadiliano.
Dogo huyo mwenye miaka 18, anatoka Klabu ya Glory, alitua na Ndege ya Shirika la Ethiopia, ingawa taarifa zilizonaswa jana ni kwamba anaendelea kujifua akiwa na KMC kwa vile Simba kwa sasa haijaanza maandalizi na hataki kushusha kiwango chake.
Inaelezwa Simba inataka kumsajili mchezaji huyo ambaye kulingana na umri wake malengo yao ni kumwendeleza kama ilivyowahi kufanya kwa Okwi alipotua kwa mara ya kwanza au kama ilivyokuwa kwa Mnigeria Eme Ezechukwu aliyesajiliwa mwaka 2008.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi alifichua kuwa, usajili wao unafanywa kwa mapendekezo ya kocha wao, Patrick Aussems na kama mahitaji yao yatatosha zoezi kwa wageni litaishia walipofikia sasa, lakini kama matahitaji kwa wachezaji hao hayatatosha wanaweza kuwasajili wengine.