Mpira wa Simba, Yanga na uungwana wa fedha-3
Muktasari:
- Mabadiliko ya kocha ambayo nadhani yalikuwa ni maamuzi ya kiutawala zaidi kuliko fedha, yaliiathiri timu mwanzoni mwa ligi lakini wakalifanyia marekebisho kwa kumrudisha Stewart Hall.
WIKI iliyopita katika sehemu ya pili tuliona jinsi mambo yanavyoendeshwa kwenye ligi yetu na hali ya fedha kwenye klabu, endelea na sehemu ya tatu...
Simba
Hata hivyo, Simba ilianza msimu kwa kushinda mechi mfululizo na kwa bahati nzuri mechi zake za kwanza zilikuwa Uwanja wa Taifa hivyo si tu ilikusanya pointi mapema lakini vilevile ilikusanya pesa ya mapema kabla ya kuanza kusafiri mikoani.
Ilipoanza kusafiri, mambo yakaanza kuharibika, suala la kuuzwa kwa Emmanuel Okwi kwa klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia kulichangia si tu kuidhoofisha timu bali pia kuleta hali ya kutokuelewana klabuni.
Kuna walioamini kwamba pesa ndefu ya mauzo ya Okwi ilichukuliwa na uongozi ambao uliendelea kusisitiza kwamba aliuzwa kwa mali kauli na kwa namna moja au nyingine hii ilichangia kupunguza morali wa matajiri ndani ya Simba.
Wengi wa wachezaji wetu, hawajui kutenganisha kati ya fedha ya motisha na fedha iliyotajwa kwenye mkataba, hivyo hata kama klabu ilikuwa bado na uwezo wa kulipa mishahara, motisha ilipungua. Suala la nidhamu likaingia na wachezaji kadhaa wakafungiwa na timu ikaishia nafasi ya tatu.
AZAM FC
Nathubutu kusema kwamba hii ni klabu pekee ambayo imekuwa na uchumi endelevu angalau kwa viwango vya Kiafrika, ni wazi kwamba klabu hii kama zilivyo nyingi za Kusini mwa Sahara (isipokuwa Afrika Kusini) isingeweza kupita kwenye chujio la Uefa.
Matumizi bado ni makubwa kuliko mapato lakini klabu hii ina chanzo cha uhakika kifedha. Hata ukiangalia mabadiliko katika kikosi, timu haikupoteza wachezaji wake muhimu walioipa nafasi ya pili msimu uliotangulia.
Mabadiliko ya kocha ambayo nadhani yalikuwa ni maamuzi ya kiutawala zaidi kuliko fedha, yaliiathiri timu mwanzoni mwa ligi lakini wakalifanyia marekebisho kwa kumrudisha Stewart Hall.
Tuhuma za kupokea rushwa kwa wachezaji (Iwe ni kweli au si kweli) ziliathiri kwa kiasi fulani kasi ya timu hii kuelekea ubingwa. Ukiangalia majina ya wachezaji waliofungiwa kwa tuhuma hizo walikuwa na umuhimu kwa kikosi cha Azam.
AFRICAN LYON
Ilianza msimu kwa mguu mbaya kibiashara na nadhani ni kutokana na uzoefu wa mmiliki wake, Zamunda kwa ligi ya Marekani Kaskazini (MLS) na biashara ya michezo katika bara hilo uliomfanya kujikuta anakuwa mbele (nje) ya utaratibu wa TFF. Migogoro ya klabu hii na TFF ilikuwa katika suala la ratiba ya ligi, udhamini na jezi. Hata hivyo moto mkubwa ulikuwa kwenye jezi na udhamini.
Kwa miaka kadhaa African Lyon imekuwa na ukaribu na klabu za Vancouver White Caps (Canada) na Seattle Sounders (Marekani) vyote vya ligi ya Marekani Kaskazini (MLS).
Msimu ulipoanza African Lyon wakavaa jezi za Seattle Sounders kitu ambacho TFF ilikipinga kwani pamoja na kutokuwepo kanuni halikuwa jambo la kawaida kwa timu kuvaa jezi ya timu nyingine. Lyon walijaribu kutafuta muafaka kwa kuomba kuondoa nembo ya Seattle Sounders.
Kabla hilo halijapoa, Lyon ikapata udhamini mnono wa Kampuni ya Simu ya Zantel. Udhamini huo wa timu ya vijana na ile ya wakubwa ukapigiwa chapuo kama moja ya mafanikio katika biashara ya michezo.
Uzinduzi ukafanyika, kama ilivyokuwa kwenye Seattle, udhamini huu nao ukakataliwa na TFF kwani hawakupenda kuwaudhi Vodacom ambao wana biashara ya simu za mkononi.
Vodacom walikuwa wamemaliza muda wao wa udhamini lakini bado walikuwa na nafasi ya kuendeleza na kisheria ni kama Lyon hawakufanya kosa lolote lakini wakawa muhanga wa hali halisi (victims of the situation).
Kwa kiasi kikubwa, kufeli kwa udhamini huu kulichangia kushuka daraja kwa timu hii. Inaweza kuwapo sababu nyingine za kiutawala lakini kwa vile makala hii inachambua zaidi masuala ya kifedha sitaweza kuyagusia hayo mengine.
Lyon ilimaliza ikiwa na pointi 19 ikishinda mechi tano, sare nne na kupoteza 17.
TOTO AFRICAN
Ni klabu kongwe katika mji wa Mwanza lakini haijawahi kuwa salama katika ligi na haijawahi kufikia mafanikio ya klabu ya Pamba, ni klabu inayoendeshwa kwa kutegemea michango ya wanachama na wapenzi.
Imehusishwa na kuwa na upande katika mvutano wa klabu kubwa, hali hii imechangia baadhi ya wapenzi wa mpira wa Mwanza kuiona kama inatokea Kariakoo kuliko Kishamapanda hivyo kutokuwa tayari kusaidia.
Toto ilishiriki ligi kwa tabu na hata ukiangalia ushindi wake ulikuwa dhidi ya timu zenye uchumi mdogo isipokuwa ushindi wa bao I-0 dhidi ya Simba. Ilishinda 5, sare 10 na kupoteza 11.
POLISI MOROGORO
Kama zilivyo timu nyingi zinazomilikiwa na taasisi za umma, Polisi inayomilikiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani haina msingi imara wa mashabiki. Kwa hiyo vyanzo vyake vikuu vya fedha ni kutoka hazina ya serikali.
Na kutokana na utitiri wa klabu za serikali yawezekana timu hii haikuweza kuangaliwa kama ambavyo kungekuwa na klabu chache au moja ya serikali. Mara nyingi klabu hizi zinakuwa ni biashara ya kila mmoja, ni biashara isiyo na mwenyewe, haikushangaza kuiona Polisi Morogoro ikikimbilia kwenye njia ilikoshukia daraja Polisi Dodoma. Kama Toto, ilishinda tano, sare 10 na kupoteza 11.
NAFASI YA FEDHA
Kama tulivyoona hapo awali, fedha imekuwa na nafasi kubwa katika kuamua mafanikio ya klabu. Kuwa na fedha katika maisha ni kitu kizuri ila kuwa na uadilifu na uungwana katika matumizi ya fedha ni kitu cha muhimu zaidi. Hii inatokana na ukweli kwamba hata klabu isiyokuwa na uchumi mkubwa huchangia uchumi wa klabu kubwa.
Mathalani iwapo klabu ya Arsenal ingekuwa inacheza dhidi ya timu tajiri pekee katika Ligi Kuu ya England isingeweza kupata nafasi ya kushiriki mashindano tajiri duniani ya Ligi ya Mabingwa. Kwa nini? Kwa sababu pointi zake nyingi zimetoka kwa timu ndogo. Na hapo ndipo unapokuja umuhimu wa kutengeneza mazingira sawia katika matumizi ya fedha.
Ni wazi klabu kama walivyo watu haziwezi kulingana mapato na matumizi lakini mazingira sawia kuhusu vyanzo, mapato na matumizi huleta hisia ya usawa katika mashindano. Vilevile ikumbukwe kwamba wawekezaji makini hawatii pesa yao katika ligi ambayo fedha zake zina utata na kanuni zake kuhusu matumizi ya pesa haziko wazi. Mfano mzuri ni klabu ya Sunderland ya England ambayo hivi karibuni ilivunja mkataba wa zaidi ya pauni 20 milioni na Kampuni ya Mafuta ya Tullow kwa lengo la kusafisha jina lake.
Tullow ambayo ilianzisha Shirika lisilokuwa la Kiserikali la ‘Invest in Africa’, iligundulika kujihusisha na ufisadi katika kujipatia mikataba katika sekta ya mafuta nchini Uganda hivyo Sunderland ikajitoa kusafisha jina lake. Kufuatia hilo kiongozi mmoja wa Sunderland alijiuzulu akidai ni kupinga ajira ya Kocha Di Canio lakini wachunguzi wa nyuma ya pazia wanasema alikwepa kashfa ya ‘Invest in Africa’.
Mwisho.
Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu wa zamani Yanga.