MPAKA HOME : Utampenda tu, soka mguuni, akili kichwani

Beki Said Morad.
Muktasari:
Morad moja ya mabeki hodari akijaliwa akili, nguvu na wakati mwingine ubabe wa mtaani, kiasi baadhi ya mashabiki wanamchukulia poa.
BEKI, Said Morad maarufu kama Mweda hajasajiliwa na klabu yoyote msimu huu. Yupo nyumbani tu baada ya Azam FC kushindwa kumwongezea mkataba mpya na sasa amekuwa mtu wa kupiga ‘dili’ kitaa na siku zikisonga mbele.
Morad moja ya mabeki hodari akijaliwa akili, nguvu na wakati mwingine ubabe wa mtaani, kiasi baadhi ya mashabiki wanamchukulia poa.
Lakini sasa kama hujui, huyu jamaa ni mjanja sana. Licha ya kwamba hana timu msimu huu, lakini alikuwa ameshajitengenezea msingi mzuri wa maisha yake. Morad amewekeza fedha zake alizovuna kwenye soka katika ardhi. Amejenga nyumba ambayo sasa ni msaada, licha ya kutopata mshahara, hana presha hadaiwi kodi ya nyumba, anachotafuta ni pesa ya kula na kulipa umeme tu.
Morad, ambaye kwa mwonekano na historia ya maisha yake ni fundisho kwa vijana kutokana na changamoto alizopitia, kwani alishawahi kuwa kondakta wa daladala, machinga wa kuuza mitumba hadi kutamba katika soka akipitia timu kadhaa zikiwamo Ashanti United, Kagera Sugar, Simba, Azam na Taifa Stars. Mwanaspoti ilipomtembelea kwa mara ya kwanza, alikuwa amepanga vyumba viwili maeneo ya Ilala, lakini sasa mambo yake safi.
Mjengo anaokaa, upo Chamazi Magengeni mtaa wa Msufini, Dar es Salaam si mchezo.
Kama una safari ya huko, ukiwa maeneo ya Chamazi Shule ya Msingi au Zahanati ukiuliza kwa Morad tu, hata mtoto mdogo anakupeleka kwani, jamaa anakubalika sana mtaani.
Katika mjengo huo ambao kwa haraka haraka thamani yake ni zaidi ya Sh. 80. milioni, una vyumba vinne vya kulala, kimoja ‘master’, jiko, choo, sebule kubwa na sehemu ya kulia chakula za kisasa ambazo zimepambwa kwa marumaru. Morad anaishi katika mjengo huo na mdogo wake, Ally Ibrahim.
Mdogo wake huyo ndiyo amekuwa akimwachia nyumba kwa kipindi akiwa kwenye majukumu yake ya kisoka, lakini hapo huwezi kuona kibaka yoyote anasogelea kwa sababu kuna ulinzi wa maana tu.
Amefuga mbwa mkubwa wa kisasa aitwaye Bobby ni mkali kwelikweli. Huwa anashinda ndani tu kwenye chumba maalumu na hufunguliwa ndani ya uzio huo nyakati za usiku tu, tena anakuwa ndani ya uzio, mtu atakayekatiza karibu na maeneo hayo bila mwenyeji lazima utoke nduki kwa jinsi anavyofoka na kubweka kwa hasira akitamani kulianzisha.
Mbali na nyumba hiyo, Morad amejenga nyumba nyingine maeneo ya Chanika, Nguvukazi karibu na Magengeni, nayo ni kubwa lakini bado haijakamilika na mpango mpango wake, itakapokamilika apangishe na anayo ardhi ya shamba maeneo ya Jarilo.
Mwandishi ilijionea yote baada ya kutia timu katika maeneo hayo na kujionea vilivyomo na kitu cha kufurahisha zaidi, Morad amekuwa mwingi wa shukrani kwa klabu ya Azam aliyoichezea kwa takribani misimu mitano kwa kuwa ndio imemwezesha kupata mafanikio yote hayo na kamwe hawezi kuisahau.
NYUMBANI
Mwanaspoti: Hodi!
Morad: Karibu hapa ndiyo nyumbani kama unavyoona tupo wawili tu, naishi na mdogo wangu Ally. Huyu amekuwa ndiyo msaada mkubwa hapa nyumbani kutokana na namna anavyonisaidia kazi za hapa, ninapokuwa sipo ndiyo mwangalizi wa kila kitu.
Mwanaspoti: Kwa nini uliamua kuja kujenga huku na ilikuwaje?
Morad: Ni kwa sababu yalikuwa maeneo ya karibu na kazini kwangu pale Uwanja wa Chamazi.
Kwangu ilikuwa rahisi kuwahi mazoezini na hata tukitoka nafika kwa urahisi na kupumzika.
Sikununua kiwanja, hapa nilinunua nyumba ambayo ilikuwa bado haijaisha na kubadilisha vitu ambavyo havikunivutia na kuikarabati kama unavyoiona.
Aliyenionyesha hapa ni jamaa yangu anaitwa, Uweso ndiyo nilikuwa nazunguka naye kutafuta, maana nilipopata pesa tu, mbali na watu kunishawishi mwenyewe nilijipanga kuhakikisha sifanyi makosa kama unavyojua maisha ya soka huwa na muda, kipindi unacho na kuna kipindi unakosa kama ilivyo kwangu sasa hivi.
Sipati mshahara, lakini sina presha kwa sababu sina mtu anayenisumbua kwa madai kama kodi ya nyumba na mambo mengine maana hiyo ndiyo huwa inaumiza, sasa hivi ninachotafuta ni pesa tu ya chakula na kuweka umeme basi ambazo nikipiga dili zangu mtaani sikosi, hayo mambo ya starehe yapo tu.
Mwanaspoti: Pesa za kujengea ulipata wapi na sehemu gani ya nyumba yako unayopenda kutumia muda mwingi?
Morad: Kusema kweli nina kila sababu ya kuishukuru Azam FC maana ndiyo imefanikisha kila kitu kwangu. Mshahara wangu wa Azam ndiyo nimejenga na kufanya yote haya hapa mjini, ingawa kwa ile nyumba ya Chanika, pesa niliyonunulia kiwanja, ilikuwa ni usajili wangu kwenda Kagera.
Ninapokuwa hapa nyumbani, muda wangu mwingi huwa nautumia kukaa sebuleni kuangalia televisheni. Naangalia zaidi soka la hapa nyumbani na nje ya nchi, sinema za kihindi na muziki.
UKONDA, UMACHINGA
Mwanaspoti: Katika maisha yako kitu gani cha historia?
Morad: Maisha yangu yana mikasa sana, hivi leo naishi namna hii ni jambo la kumshukuru Mungu. Historia yangu, mara baada ya kumaliza shule, nijiingiza kwenye kazi ya kuuza mitumba pale Tandale nakumbuka ilikuwa mwaka 2000.
Nilikuwa naitia mnada ule wa ‘beba beba, mia tano’, kazi ambayo niliifanya kwa takribani miaka miwili na baada hapo, nilihamia kwenye ukonda wa daladala ambako nilipiga debe hapo kwa miaka mitatu.
Nilianza kazi ya daladala mwaka 2003 daladala ilikuwa inapiga ruti ya Sinza, Tandika na nilikuwa maarufu sana.
Wanafunzi walikuwa wananipenda sana kwa sababu sikuwa nawakataa, pia sikuwa mkorofi, mtu akiomba msaada hana kitu namwacha anakwenda.
Hayo ndiyo maisha niliyopitia na yalikuwa na changamoto sana kwa sababu kama kazi ya ukonda, kuna kipindi mnafanya kazi ngumu, pesa inaingia kwenye hesabu ya tajiri tu na nyinyi mnarudi nyumbani hamna kitu.
Mwanaspoti: Kitu gani unathamini katika maisha yako na ulikuwa na gari umeipeleka wapi?
Morad: Ninachokiamini ni kusaidia yatima na watu wenye uhitaji, huwa nafanya hivi, ninapopata pesa huwa naigawa kwao napeleka kwenye vituo tofauti kimoja wapo kipo Kariakoo, pia kuwapa zawadi watoto wadogo.
Kuhusu gari, niliisogeza (kuuza), pesa nilifanyia marekebisho yaliyokuwa yamesalia kwenye nyumba hii, pia kama unavyojua gari ni gharama, niliona ni bajeti nyingine kwa sababu kipindi hiki niko tu nyumbani, nikiamua kutoka ni mara chache.
MAPENZI
Mwanaspoti: Ulikuwa na mwanamke mbali na mkeo Fatna, mbona sasa unaishi msela, imekuwaje?
Morad: (Anacheka) Yule bwana alinikimbia hata sijui yuko wapi, alikuwa mtu wangu tu sikuwa nimemwoa, aliniaga anaenda kwao Moshi ndiyo mpaka leo hajarudi. Na Bi Fatna ndiyo kama vilevile nipo msela tu kwa sasa.
Mwanaspoti: Nini mpango wako sasa juu ya mahusiano?
Morad: Nataka kutulia tu nichakarike na mambo mengine, siwezi kukaa na mtoto wa watu kipindi hiki nikamsumbua, atataka kula, kuvaa na mambo mengine na mimi itanichanganya, ngoja nitulie kwanza hayo mambo yapo tu.
MAISHA YA SOKA
Mwanaspoti: Kwa sasa huna timu nini mpango wako?
Morad: Ndiyo imeshakuwa, chochote kitakachotokea kwangu poa, nasubiri hilo dirisha dogo timu yoyote itakayonihitaji nikiona inanifaa nitajiunga nao, kikubwa maslahi.
Pia, licha ya kuwa Azam wameniacha, sitawasahau naishukuru sana kwa sababu mpango mzima wa maisha yangu ni juu yao.
Mwanaspoti: Historia yako ya soka kwa ufupi iko vipi?
Morad: Kwa mara ya kwanza nilianza kuichezea Ashanti 2006 na aliyenishawishi ni Mkufunzi wa African Star anaitwa Father.
Klabu nyingine nilizopita ni Manyema 2007, Kagera 2008, Simba 2009 na 2011 nilijiunga na Azam hadi msimu uliopita.