Prime
Moto wa Yanga unaanzia hapa
MSIMU uliopita mashabiki wengi wa Yanga walikuwa wakiangalia mechi za timu hiyo roho mkononi, wakiomba dakika 90 zimalizike kutokana na kiwango kisichoridhisha, huku utimamu wa mwili ukitajwa kuwa tatizo kubwa. Hali hiyo ilimuweka kwenye presha kubwa kocha wa mazoezi ya viungo, Chyna Mokaila wakitaka jamaa atimuliwe.
Ghafla msimu huu mambo yamebadilika, wachezaji wa timu hiyo wanaonekana wako fiti huku kocha akibaki yuleyule kumbe zimefichuka siri zilizobadilisha mambo hayo na kuirudishia timu hiyo ubora ambao unawasaumbua timu nyingi.
Yanga kwenye mechi zake tatu zilizopita za Ligi Kuu Bara ongeza ule mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, imeonyesha uimara mkubwa wa wachezaji wake kuwa na pumzi ya kutosha, ikiwasaidia kuwazima wapinzani huku yenyewe ikishambulia kwa nguvu.
Kama ulikuwa hufahamu, wakati kocha wa Yanga, Manqoba Mngqithi akikubali ajira hiyo, aliamua kumbakisha Mokaila akiwaambia mabosi wa timu hiyo kuwa raia huyo wa Botswana anamfahamu vizuri na kazi yake na kwamba abakishwe.
INACHOFANYA SASA
Yanga ikiwa mazoezini chini ya Manqoba, kocha huyo amekuwa akimuachia muda wa kutosha wa dakika 30-35 kocha huyo wa mazoezi ya viungo kwa kuwapa mazoezi makali tofauti ya kupandisha ufiti wa mwili.
Ratiba hiyo imekuwa tofauti na kile kilichokuwa kinafanyika kwa makocha waliopita ambapo walikuwa wanampa Mokaila dakika 15-20 za kuwaandaa na kupandisha ufiti wa miili ya wachezaji wa kikosi hicho, hatua ambayo ilishusha nguvu ya kikosi hicho.
Ukiacha hilo kocha Manqoba alishataka kuongezwa kocha mwingine wa mazoezi ya viungo anayesaidiana na Mokaila akiletwa mzawa Abdulwahid Abdallah maarufu kwa jina la Ekkoto ambaye kila mmoja ana jukumu lake.
Wakati ukimuona Mokaila kwenye mechi za timu hiyo basi tambua kwamba ile siku ambayo Yanga inacheza asubuhi yake wale wachezaji ambao hawapo kwenye mpango wa mechi na hawana majeraha, wanakuwa na Ekkoto kwenye ratiba ya mazoezi siku hiyo asubuhi.
Akili ya Manqoba ni kwamba wale wachezaji ambao hawachezi, nao wanatakiwa kuendelea na ratiba ya mazoezi na sio kwenda kukaa na familia zao huku pia jioni siku hiyohiyo ya mchezo wanatakiwa kuwa uwanjani kuangalia namna wenzao wanavyocheza.
Kitu kingine ambacho Manqoba amebadilisha ni kwamba kila mechi inapomalizika wale wachezaji ambao waliingia kipindi cha pili kuanzia dakika 45 za kumalizia mpaka 90, mchezo ukimalizika wanaungana na wale ambao walikuwa benchi na hawakupata nafasi ya kucheza wakipewa mazoezi kwa dakika zisizopungua 30, kabla ya kuendelea na ratiba ya siku inayofuata, mazoezi hayo akiachiwa Mokaila.
MSIKIE MANQOBA
Akizungumzia hilo, kocha Manqoba amesema anaridhiswa na kazi ambayo inafanywa na wasaidizi wake ambapo falsafa ya soka lake inahitaji wachezaji waliokuwa tayari kuhimili kasi na nguvu wakati wote wa mchezo.
Manqoba amesema ili mchezaji wa timu hiyo apate nafasi ya kucheza anatakiwa kuwa tayari katika vitu hivyo ambapo anafurahishwa na namna wachezaji wake na hata wasaidizi wake hao wanavyohakikisha hilo linakuwa sawa.
“Ninafurahishwa na kazi ambayo wasaidizi wangu wote wanavyofanya lakini nikwambie namjua Mokaila kwa muda mrefu, najua ubora wake, niliposikia yupo hapa nikawaambia viongozi huyo nataka nimkute, nadhani kila kitu kinakwenda vizuri,” amesema Manqoba.
“Soka ambalo tunataka lichezwe hapa kila mchezaji anatakiwa kuwa na kasi na nguvu kwa kiwango kikubwa, hivi vitu viwili vitamsaidia wakati wa kutengeneza mashambulizi lakini pia wakati tumepoteza mpira, wengi wamefanikiwa kushika hili ndio maana tunafanya mambo kwa ubora mkubwa.”