Mnigeria aamsha morali Dodoma Jiji
Muktasari:
- Mchezaji huyo aliyejiunga na Dodoma Jiji msimu huu baada ya kuachana na New Kings FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar, bado hajapata nafasi ya kucheza katika mechi za Ligi Kuu Bara, japo, Mashami amefurahishwa na anachokionyesha mazoezini.
KOCHA Mkuu wa Dodoma Jiji, Vincent Mashami amesema licha ya winga wa timu hiyo, Mnigeria Adetunji Oyeyode kutocheza hadi sasa kutokana na kutokamilika kwa vibali vya kazi (Work Permit), ila amefurahishwa na maendeleo ya nyota huyo kikosini.
Mchezaji huyo aliyejiunga na Dodoma Jiji msimu huu baada ya kuachana na New Kings FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar, bado hajapata nafasi ya kucheza katika mechi za Ligi Kuu Bara, japo, Mashami amefurahishwa na anachokionyesha mazoezini.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mashami amesema baada ya mapumziko ya Kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kila kitu kitakuwa kimekamilika, huku akifurahishwa na kiwango bora anachoendelea kukionyesha wakati wa mazoezini na wenzake.
"Ni miongoni mwa wachezaji wazuri sana na tulianza kuona kipaji chake tangu msimu uliopita akiwa na kikosi cha New Kings FC, matumaini yetu hadi Ligi Kuu Bara itakaporudi kila kitu kiwe kimekamilika ili aanze kucheza rasmi," amesema Mashami.
Aidha, Mashami amesema baada ya mechi ya mwisho na Coastal Union iliyoisha suluhu (0-0), Oktoba 31, 2026, alitoa siku tano za mapumziko kwa wachezaji, kisha kikosi hicho kirejee kwa ajili ya kufanyia tathimini ya kilichotokea hadi sasa.
"Baada ya siku tano wachezaji wote watarudi kambini kwa ajili ya kujiandaa na mechi dhidi ya Fountain Gate, Novemba 21, 2026, lengo la kutoa mapumziko mafupi ni kutaka kufanyia kazi eneo la ushambuliaji na la kujilinda," amesema Mashami.
Kocha huyo raia wa Rwanda, ameiongoza Dodoma Jiji msimu huu katika mechi 10, za Ligi Kuu, ambapo kati ya hizo ameshinda nne, sare nne na kupoteza mbili, ikishika nafasi ya tano na pointi 16, huku ikifunga mabao manane na kuruhusu matano.